MAJI NA AFYA ZETU
Maji ni afya, maji ni kinga. Kuna faida lukuki kwa unywaji wa maji.
Je wajua sehemu kubwa ya mwili wa binadamu imetengenezwa kwa maji, kwa maana kwamba viungo na tishu mbalimbali mwilini vimeundwa kuhusisha maji..kwa mfano damu, misuli na hata mafuta mwilini yana maji kwa kiasi chake pia.
Karibu asilimia 60 hadi 75 uzito wa mwili wa binadamu ni maji ingawa kunakuwa na tofauti za kiasi cha maji kulingana na jinsia, umri, mazingira, aina za shughuli mtu anafanya nakadhalika
Dalili zinazoonesha mtu kapungukiwa maji mwilini
1. Harufu mbaya ya kinywa
2. Ngozi kuwa kavu
3. Maumivu ya kichwa (ingawa sio kila maumivu ya kichwa ni upungufu wa maji)
4. Kizunguzungu (ingawa sio kila hisia za kizunguzungu husababishwa na upungufu wa maji mwilini)
5. Uchovu wa mwili
6. Midomo kuwa mikavu (watu wengi huonesha dalili hii na huonekana sehemu ya nje ya midomo - lips)
7. Kutopata choo mara kwa mara au kupata choo kigumu na kwa shida (constipation)
Kuna baadhi ya dalili hapo juu zinahusiana na vitu vingine tofauti na kupungukiwa maji mwilini hivyo ni vyema kuzitilia maanani dalili hizi na kuchukua hatua stahiki ili kuepukana na shida zinazoweza kujitokeza baadae..
Lakini ni muhimu kukumbuka kwamba uonapo dalili mojawapo kati ya hizi ni vizuri kukumbuka kunywa maji ya kutosha.
Jinsi ya kuuongezea mwili maji :
**Kunywa maji kama yalivyo ndio njia kuu na rahisi ya kurudisha maji yaliyopotea mwilini, ambapo inashauriwa mtu kunywa angalau glasi nane (ujazo wa mls 250) za maji kila siku au zaidi ili kuupatia mwili kiasi unachohitaji kwa ajili ya shughuli mbalimbali za mwili**
Njia zingine za kuongeza maji mwilini (hasa kwa watu wavivu kunywa maji kama yalivyo)
1.kahawa na chai ( ni vema kutumia kwa kiasi vinywaji hivi kwa sababu vina kemikali inayoitwa kafeini ambayo ikizi inaweza kufanya kupungua kwa maji mwilini...kiasi cha milligram 250 hadi 300 za kafeini hufanya mwili kupungukiwa maji)
2. Maziwa yaliyotolewa krimu au yenye mafuta kidogo (skimmed or low fat milk)
Sehemu kubwa ya maziwa ni maji lakini pia Maziwa huwa na madini kama sodiamu na potassiamu ambayo husaidia kuweka vizuri balansi ya maji mwilini.
3. Mbogamboga na matunda
Mfano tikitimaji, machungwa, kabeji, spinachi na karoti
4. Kunywa juisi za matunda halisi kama vile machungwa, maembe, mapera, maepo na kadhalika
5. Kula vitu vyenye mchuzi kama vile supu ( za nyama mbalimbali na mboga za majani)
** Ni vyema kuepuka matumizi (kwa wingi) ya vyakula vyenye chumvi nyingi, sukari nyingi, kafeini nyingi pamoja na vilivyoandaliwa kwa mafuta mengi kwani ni baadhi ya vyakula ambavyo hupelekea mwili kupoteza maji au kuhitaji maji zaidi**
Yote kwa yote nnywaji wa maji unachochewa na vitu vingi. Kuna mazingira/hali ya hewa, watu wa mikoa ya baridi kama Mbeya na Njombe unywaji wao wa maji si sawa na wale wa maeneo ya joto kama Dar es salaam na Pwani. Pia kuna mahitaji ya mwili, kuna watu miili yao inahitaji maji mengi kutokana na maumbile au hali zao za kiafya hivyo hujikuta wanakunywa maji kwa wingi mfano watu wenye kisukari.
Pamoja na yote hayo unywaji wa maji kwa wingi tunaweza sema ni tabia ya mtu aliyojijengea. Utamkuta mtu yeye awe kwenye mazingira yeyote ya baridi au ya joto bado atakunywa maji lita mbili na mwingine yeye akiwa Mbeya na akiwa Dar unywaji wake wa maji hauridhishi ni ndogo sana bila kujali Dar inamuhitaji anywe maji mengi.
Maji ni muhimu kwa mwili na afya zetu. Ukipata shida au uvivu kunywa maji kama maji, jitahidi kutumia njia nyepesi zilizoainishwa hapo juu.
Na
Innocent Sanga
Mwanalishe
Fasmo Tanzania
0688301558
Comments