KIFUA KIKUU. UPO KAMA HAUPO.
KIFUA KIKUU. UPO KAMA HAUPO.
Kifua kikuu ni nini?
Watanzania wengi huutambua ugonjwa wa kifua kikuu kama TB, neno ambalo ni kifupisho cha Tuberculosis. Jina la Kiswahili la ugonjwa huu ni kifua Kikuu ambao ni ugonjwa wa kuambukiza unaoathiri mapafu na kusababishwa na bakteria (waitwao Mycrobacterium tuberculosis). Bakteria/ Vimelea vinavyosababisha ugonjwa wa kifua kikuu huishi katika mapafu na kushambulia mfumo wa upumuaji.
Ugonjwa huu husambazwa kwa njia ya hewa wakati watu walioambukizwa wanapokohoa, kupiga chafya au kutema mate. Dalili zake huanza kuonekana siku chache baada ya mtu kuambukizwa, hivyo ni rahisi kueneza ugonjwa huu kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. Kikohozi cha muda mrefu kinachoweza kuhusisha kukoha damu, Maumivu kifua, uchovu wa mwili, kupungua uzito, Homa, Kutokwa na jasho wakati wa usiku ni baadhi ya dalili za ugonjwa huu.
Ikumbukwe kwamba, kuna watu wana maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu lakini hawaoneshi dalili zozote, hawajaisikii kuumwa na hawaambukizi watu wengine. Hali hii hufaamika kama ni hatua ya kifua kikuu kilicholala (latent TB). Bila kupatiwa matibabu, watu hawa hupatwa na ugonjwa wa kifua kikuu na kuonesha dalili zote.
Kuna Imani katika jamii zetu kwamba kila mtu ana vimelea vya kifua kikuu ambavyo humsababishia mtu ugonjwa pale ambapo kinga ya mwili wa mtu husika ikishuka. Je, hujawahi kusikia hili?
Maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani
Historia inatueleza kuwa, neno kifua kikuu au “Tuberculosis” liliasisiwa na Johann Schӧnlein mwaka 1834 ingawa ugonjwa huu umekuwepo katika historia ya mwanadamu kwa kipindi kirefu kabla ya hapo tangu miaka ya 1600.
Maadhimisho ya siku hii duniani kama sehemu ya kuhamasisha mapambano dhidi ya ugonjwa huu yametokana na siku ambayo ugunduzi wa vimelea vinavyosababisha ugonjwa huu ulitokea. Ilikuwa ni tarehe 24 Machi 1882, siku ambayo Dr. Heinrich Hermann Robert Koch aliweza kutambulisha ugunduzi wa vimelea hivi. Ugunduzi huu ulipelekea kuongezeka kwa mbinu za matibabu za ugonjwa huu na kumfanya mwanasayansi huyu mbobezi katika masuala ya maikrobaiolojia kutunikiwa tuzo ya Nobel katika fiziolojia mwaka 1905.
Kila mwaka tarehe 24 Machi, ulimwengu wote huadhimisha siku ya Kifua Kikuu duniani kama sehemu ya kuhimiza na kuongeza mapambano dhidi ya ugonjwa huu hatari unaoambukiza ambao unatatiza sehemu kubwa ya nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.
Kauli mbiu ya mwaka 2025 inasema kwa Pamoja tunaweza kutokomeza kifua kikuu: azimia, wekeza, timiza ambayo ni ishara ya matumaini, jitihada za haraka zinazohitajika na uwajibikaji katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu. Aidha kauli mbiu hii inahamasisha umoja katika jitihada za kutokomeza ugonjwa huu hatari na kutukumbusha kuweka malengo mahususi kama wadau wa afya ili kuwezesha mafanikio katika mapambano haya.
Tangu mwaka 2000 duniani kote, kwa jitihada jumuishi, takribani watu milioni 79 wameokolewa kutoka katika ugonjwa huu hatari. Maana yake watu hawa walipona baada ya kuathiriwa. Mwaka 2023 pekee, takribani watu milioni 11 waliugua ugonjwa huu wakati watu milioni 1.25 walifariki kutokana na ugonjwa huu na kufanya kifua kikuu kuwa ugonjwa wa kuambukiza unaoongoza kusababisha vifo katika jamii.
Shirika la afya duniani linadhamiria kupunguza kutokea kwa visa vipya vya kifua kikuu kwa 80% wakati likilenga kupunguza vifo vitokanavyo na kifua kikuu kwa 90% hadi kufikia mwaka 2030.
Hali ya kifua kikuu Tanzania
Tanzania imepiga hatua katika kupunguza vifo na visa vipya vya ugonjwa wa kifua kikuu. Jitihada za serikali na wadau zimewezesha Tanzania kupunguza visa vipya vya ugonjwa huu kutoka wagonjwa 306 kwa kila watu 100,000 mwaka 2015 hadi wagonjwa 183 kwa kila watu 100,000 mwaka 2023. Aidha vifo vitokanavyo na ugonjwa huu vimepungua kutoka 58,000 mwaka 2015 hadi 18,400 mwaka 2023. Jitihada hizi zinaiweka Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 3 zenye mzigo mkubwa wa ugonjwa wa kifua kikuu kuwa katika mwelekeo sahihi wa kufikia malengo ya kupunguza vifo na visa vipya vya ugonjwa huu ifikapo mwaka 2025. Aidha, mafanikio katika matibabu ya ugonjwa huu yamefikia 96% kwa visa vipya vyote vya kifua kikuu vinavyotambuliwa ambayo ni zaidi ya lengo la zaidi ya 90% la kitaifa na shirika la afya duniani.
Kwa mujibu wa takwimu za ugonjwa wa kifua kikuu nchini Tanzania mwaka 2023, mikoa inayoongoza kupatikana kwa visa vipya vya ugonjwa huu nchini ni Dodoma, Temeke, Tanga, Mwanza and Morogoro wakati mikoa iliyoonesha visa vipya vichache ni Pemba, Kigamboni, Unguja, Katavi na Ilala.
Katika maeneo yote nchini na duniani, watu walio katika hatari ya kupata magonjwa haya ni wachimbaji wadogo wa madini, wavuvi, wafungwa, watu wanaoishi katika makazi holela. Hii ina maana kwamba juhudi za ziada zinatakiwa kuchukuliwa ili kuwezesha kutokomeza ugonjwa huu.
Tukumbuke nini kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu
Kujikinga na ugonjwa huu
Kuhakikisha Watoto wote wanaozaliwa wanapewa chanjo ya kuwakinga na ugonjwa huu. Mtoto hupewa chanjo hii ndani ya mwezi mmoja baada ya kuzaliwa. Nchini Tanzania chanjo hii hujulikana kama Ndui na mtoto huchomwa katika bega la kulia.
Kupata matibabu kamili yanayoambatana na kutambua dalili za ugonjwa mapema. Ni muhimu serikali kushirikiana na wadau kutoa elimu kwa jamii nzima ili kuhakikisha watu wanaweza kuchukua hatua stahiki mapema pindi tu wanapojitambua kuwa na dalili zinazoweza kuhisiwa kuwa ni kifua kikuu.
Ikiwezekana watu wahimizwe kuepuka maeneo yenye misongamano ya watu wengi na mzunguko mdogo wa hewa kama vile sehemu za masoko yenye watu wengi, makazi ambayo hajapangiliwa na nyumba zenye mifumo ya hewa hafifu.
Lishe na kifua kikuu
Lishe ni sehemu muhimu sana ya afya ya kila mmoja wetu. Kushuka kwa kinga ya mwili ni kisababishi kikuu cha kuendelea kwa kasi kwa ugonjwa huu Pamoja na kutokea kwa magonjwa mengine nyemelezi. Masuala muhimu ya kutambua na kuzingatia kuhusu lishe na ugonjwa kifua kikuu;
Lishe duni ni moja kati ya visababishi vikuu vinavyopelekea kuongezeka kwa uwezekano wa mtu kupata ugonjwa wa kifua kikuu. Hivyo lishe bora ni njia sahihi ya kuzuia na kusaidia katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu hatari. Lishe bora huzingatia ulaji wa vyakula vya aina mbalimbali, kwa viwango na muda unaotakiwa kulingana na mahitaji ya mtu. Kwa ujumla, wanalishe wanashauri wanajamii kuzingatia kula vyakula vyenye virutubishi kwa wingi kutoka katika makundi yote 6 ya vyakula kulingana na muongozo wa ulaji wa Tanzania bara.
Maandalizi sahihi ya chakula yanaweza kusaidia kuzuia kuenea kwa kifua kikuu kutoka kwa wanyama hasa Ng’ombe (kupitia maziwa) kwani kuna vimelea ambavyo vinaweza kusambaa kutoka kwa mnyama hadi kwa binadamu. Hii husababishwa na kunywa maziwa yaliyotoka kwa mnyama aliye na maambukizi ambayo hayajachemshwa vizuri.
Matumizi ya bidhaa maalumu zenye virutubisho kwa wingi kwa waathirika wa ugonjwa huu huweza kusaidia kwa haraka na ufanisi, kuboresha hali ya lishe ya mgonjwa. Bidhaa hizi ni kama vile chakula dawa kilicho tayari kwa matumizi (RUTF) na bidhaa zingine zilizo na wingi wa virutubishi kama vile protini, vitamini na madini kwa wingi. Bidhaa hizi huweza kumsaidia mgonjwa kupata virutubishi anavyohitaji kwa njia rahisi na haraka akiwa katika hatua za kupambana na ugonjwa huu mwilini.
Ufuatiliaji wa hali ya lishe kwa watu wote hasa mgonjwa wa kifua kikuu, ni afua muhimu katika kuwezesha utambuzi wa mapema wa upungufu wa virutubishi mwilini na hivyo kuwezesha uchukuaji wa hatua mapema ili kutatua changamoto ya mgonjwa husika. Ni vyema kutumia njia zaidi ya moja ili kupata uelewa mpana wa hali ya lishe ya mtu (mgonjwa wa kifua kikuu). Njia zinazoweza kutumika ni kama vile kupima sehemu za nje za mwili wa binadamu kama vile urefu na uzito, kupima wingi wa virutubishi kwenye damu na majimaji mwilini, kufuatilia ulaji wa mtu Pamoja na kuangalia viashiria vya ugonjwa vinavyoweza kuonekana mwilini.
Usugu wa vimelea na dawa za kutibu kifua kikuu
Dhana ya usugu wa vimelea imekuwa ni kitu cha kawaida sana katika masikio ya walio wengi siku hizi, hasa katika muktadha wa matumizi ya dawa mbalimbali katika huduma za afya. Katika ugonjwa wa kifua kikuu, kutokamilisha matumizi ya dawa elekezi kama sehemu ya matibabu ya ugonjwa huu ni kisababishi kikubwa kinachopelekea vimelea vya ugonjwa huu kutengeneza usugu kwa madawa yanayotumika katika matibabu. Kuambukizwa vimelea vyenye usugu na matumizi ya dawa zilizo chini ya viwango ni sababu zingine zinazopelekea kutokea kwa wagonjwa wenye usugu wa dawa za kutibu kifua kikuu.
Maendeleo katika matibabu ya kifua kikuu yamewezesha kuwepo kwa mbinu bora zaidi zinasaidia matibabu ya ugonjwa huu hatari katika mazingira ya usugu wa vimelea.
Ni vyema kwa wananchi wote kufuata ushauri wa kitaalamu katika matibabu ya ugonjwa huu ili kusaidia kupunguza matatizo yanayojitokeza kutokana na usugu wa vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu. Tuzingatie kutumia dawa kikamilifu na kufuata ushauri tunaopewa na wataalamu wa afya.
Kifua kikuu na magonjwa mengine
Watu walioambukizwa vimelea vya kifua kikuu na kuonekana kuwa na viashiria vingine vya hatari kama vile walio na kinga ya mwili hafifu, watumiaji wa tumbaku, maambukizi ya virusi vya UKIMWI, utapiamlo na magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari wapo katika hatari kubwa zaidi ya kupata na kushambuliwa na ugonjwa huu wa kifua kikuu. Viashiria vyote hivi hudhoofisha kinga ya mwili na kuufanya kuwa katika hali ya kuweza kuathirika kirahisi. Taarifa za ufuatiliaji wa magonjwa nchini huthibitisha hili kwani, wagonjwa wengi wa kifua kikuu wasiofuata taratibu za kitaalamu za matibabu huishia kuugia magonjwa mengine nyemelezi.
Shirika la Family Smile Organization (FASMO) linaungana na wadau wote ulimwenguni kuhamasisha jamii juu ya kujikinga na ugonjwa huu hatari ili kupunguza madhara yanayotokea kwa mtu mmoja mmoja, kaya, familia, jamii, nchi na duniani kwa ujumla.
Pamoja tunaweza kutokomeza kifua kikuu: azimia, wekeza, timiza.
Je, una maoni. Tungependa kusikia kutoka kwako msomaji wetu.
Inasemekana mtu akipata TB mara tatu humpelekea kupata UKIMWI, Je una maoni gani juu ya hili? Toa maoni yako huru kwa kutuandikia kupitia eneo la maoni.
Na mwanalishe,
Sanga Innocent Osward
Comments