Mtoto wa Afrika

Siku ya Mtoto wa Afrika.

Ni leo tarehe 16 mwezi Mei siku ambayo Tanzania na nchi zingine za Afrika zinaungana kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika. 

Kauli mbiu ya mwaka huu ni  "Maendeleo Endelevu 2030: Imarisha Ulinzi na Fursa Sawa kwa Watoto” Kauli mbiu hii inawahimiza wazazi, walezi, jamii, Serikali na wadau wengine kuzingatia wajibu wetu katika kuimarisha mifumo ya ulinzi na maendeleo ya Mtoto ili aweze kudhibiti changamoto ya ongezeko la vitendo vya ukatili nchini pamoja na kutoa haki sawa kwa watoto wote bila ubaguzi wa aina yoyote.

Awali ya yote, chimbuko la Maadhimisho haya ni Azimio lililopitishwa na uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1990 kwa lengo la kuwakumbuka watoto wa kitongoji cha Soweto nchini Afrika ya Kusini waliouawa tarehe 16 Juni, 1976 kutokana na ubaguzi wa rangi.

Watoto hao walikuwa wakidai haki zao za kutobaguliwa pamoja na haki nyingine za kibinadamu ikiwemo haki ya kupata elimu bora na hivyo kupinga mifumo ya elimu ya kibaguzi. Kufuatia tukio hili, OAU iliazimia kuwa tarehe 16 Juni ya kila mwaka iwe Siku ya Mtoto wa Afrika.

Hivyo uwepo wa maadhimisho haya ni kutupa nafasi ya kurejea na kutathmini mazingira ya watoto wa Afrika kwenye kila sekta. Kwa haraka haraka, changamoto za yule mtoto wa Afrika ya Kusini 1976 bado zipo kwa kwa mtoto wa 2023 nchini Tanzania.

Ni kweli kila jamii duniani ina matabaka, lakini yatupasa kama jamii tuungane kuhakikisha matabaka yaliyopo kwenye jamii yetu hayazuii mtoto kupata haki zake. Mfano matabaka ya kiuchumi yamepelekea mtoto kutoka tabaka la chini kiuchumi kutoweza kupata elimu bora na mazingira bora ya kujifunzia.
Ni masikitiko yetu mfuko wa bima ya afya ulifuta Bima ya Afya ya watoto (Toto Afya Kadi) bila kuja na mbadala wenye unafuu kwa wazazi na walezi kuweza kuwapatia  watoto wao bima za afya.

Tunaweza kutumia wiki nzima kuelezea changamoto na maumivu ya watoto katika afya na elimu. Na tutahitaji mwezi mzima kuelezana juu ya machozi ya watoto katika malezi hususani ongezeko la unyanyasaji dhidi yao na kupungua kwa uwajibikaji wa wazazi. 

Mbali na uwepo wa changamoto nyingi serikali inajitahidi kuweka mambo sawa. Kwa mfano, kuhimiza huduma ya chakula mashuleni, kukataza shule zisisajili wanafunzi wadogo kukaa bweni na ujenzi na maboresho ya shule na vituo vya afya. Japo kuna jitihada inabidi kuongezwa kwenye malezi na kupambana na unyanyasaji wa watoto kama kaulimbiu ya Mtoto wa Afrika 2023
Fasmo Tanzania tunaungana na watoto na wadau wengine katika maadhimisho haya kwanza, kuhamasisha malezi bora ya mtoto. Wazazi wajifunze namna nzuri za kuadhibu mtoto pale anapokosea na kumpa hamasa pale anapopatia na sio kulea watoto kwa mazoea au namna walivyolelewa wao. 
Sambamba na hilo pia wazazi watilie maanani mahusiano yoyote yale lazima yajengeke kwenye misingi ya mawasiliano. Vitu hivi vitasaidia sana malezi bora na ulinzi wa mtoto. Kwa kuwa mtoto atapewa malezi mazuri na atakuwa mwepesi kusema changamoto anazopitia kwa kuwa jamii ipo tayari kumsikiliza na kumsaidia.

Jamii nzima tuna wajibu wa kuijenga jamii bora.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa mitandao.

Fasmo Tanzania. 
www.fasmoorg.com 

Comments

Popular posts from this blog

Mitindo Yetu Ya Ulaji.

Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.

MADHARA YA UTENGANO WA KIJAMII YALIYOSABABISHWA NA COVID19