TUNAWEZA ISHI BILA TUMBAKU.

Tarehe 31 Mei ya kila mwaka ni siku ya kupinga matumizi ya sigara na bidhaa za Tumbaku Duniani (World No Tobacco Day). Siku hii iliasisiwa na Shirika La Afya Duniani (WHO) mwaka 1987. Hii ni kutokana na madhara ya bidhaa hizo kwa watumiaji na watu wanaowazunguka kiafya na kimazingira. Madhumuni ya siku hii ni kuhamasisha watu na kutoa elimu juu ya madhara yatokanayo na uvutaji na utafunaji wa tumbaku.
Utengenezaji na uvutaji wa sigara ni  halali hapa nchini kwetu Tanzania. Utafiti unaonyesha kwa siku duniani watu takribani 500 hufariki dunia kutokana na matumizi ya tumbaku. Tumbaku inaweza kuzalisha aina mbalimbali za saratani, magonjwa ya moyo, kiharusi, vidonda vya tumbo na magonjwa sugu ya kifua.
Utafiti uliofanywa hapa nchini unaonyesha asilimia 40 hadi 50 ya watu wanaougua ugonjwa wa saratani ya mapafu unatokana na uvutaji wa tumbaku. Katika hilo hata wasiotumia tumbaku wamekuwa wakiathirika zaidi kutokana na kuvutishwa bila ridhaa yao, kutokana na ukweli kwamba hakuna udhibiti wowote dhidi ya wavutaji wa sigara.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoridhia sheria ya kudhibiti uvutaji wa sigara kwenye ofisi za umma na katika mikusanyiko ya watu. Sheria ya Tanzania ya Usimamizi wa Bidhaa za Tumbaku, sura ya 121 TL, ya mwaka 2003 katika kipengele cha 12 (1) cha sheria hiyo, kinapiga marufuku matumizi ya bidhaa zote za tumbaku kwenye maeneo ya umma. Kwa mujibu wa sheria hiyo, watu wote wanaovuta sigara wanatakiwa kupunguza au kuacha kabisa matumizi ya tumbaku na pia jamii itambue madhara yatokanayo na matumizi ya bidhaa za tumbaku kuwa ni hatari kwa afya ya binadamu.
Bahati mbaya ni kwamba pamoja na kuwepo sheria na miongozo ya kuthibiti uvutaji wa sigara kwenye ofisi za umma na mikusanyiko ya watu. Bado udhibiti wa matumizi ya sigara umekuwa mdogo. Watu mbalimbali wamekuwa wakivuta sigara masokoni, kwenye stendi za mabasi, kwenye maduka makubwa na sehemu zingine zenye mikusanyiko. Mbaya zaidi baadhi ya wazazi wamekuwa wakivuta sigara wakiwa wamewabeba watoto wao, hata madereva wa daladala wamekuwa wakifanya hivyo wakiwa na abiria bila kujari wanaopokea moshi ndiyo wanaathirika zaidi.

Hali ya uvutaji wa sigara kwenye ofisi za umma na mikusanyiko imekuwa ikiendelea kuwa kawaida kama vile hamna sheria inayowabana. Lakini hii pia ni kutokana na watu wengi kutokuwa na uelewa wa madhara ya uvutaji wa sigara na madhara ya moshi wa sigara ukivutwa na asiyemtumizi wa sigara. 
Pili kukosekana kwa maeneo yaliyotengwa maalumu kwa kuvutia sigara ili wavutaji sigara wakihisi kiu waende kwenye maeneo hayo wakavute kwa raha zao bila kuathiri wengine. Pamoja na hayo pia kuna mapungufu katika usimamizi  wa sheria iliyopo kwa kutotolewa kwa adhabu kwa wavunjifu wa sheria hiyo.
Kama elimu itatolewa, sheria itasimamiwa kikamilifu na mazingira yakiwekwa rafiki idadi ya wagonjwa wa saratani ya mapafu na magonjwa mengine yanayotokana na uvutaji wa sigara YATAPUNGUA kwakuwa watu watapunguza uvutaji na watu hawatavutishwa moshi wa sigara.
Vipi kuhusu wakulima na viwanda vya sigara?
Ni kweli kabisa kuna watu na makampuni mengi wamewekeza hela nyingi kwenye zao na biashara ya tumbaku. Kwa hali ya ubinadamu ni muhimu sana kuheshimu jitihada na mitaji yao. Ripoti zinaonyesha watu takribani bilioni moja ni watumiaji wa tumbaku, hivyo ni kusema biashara ya tumbaku ni kubwa na yenye faida. Ili kuepusha hasara kwa wawekezaji nchi ina kila sababu ya kuweka malengo ya muda mrefu ya kupunguza uzalishaji wa tumbaku na hatimaye kuzuia kabisa. 
Hiyo ni pamoja na....
●Kushirikisha na kutaarifu makampuni juu ya dhamira hiyo. Kwa mfano serikali iseme makampuni yajipange kufikia mwaka 2030 yawe yamesitisha au kupunguza uzalishaji wa sigara kwa zaidi ya 95%. Hii itasaidia makampuni kujipanga ili yasipate hasara kubwa.
● Kutoa elimu ya kilimo (mazao mbalimbali ya biashara) na ujasirimali kwa wakulima. Ili waone fursa zingine nje ya kilimo cha tumbaku. Hivyo kupunguza uzalishaji wa zao hilo na hatimaye kulizuia kabisa.
● Kuja na ubunifu na njia zingine zitakazofaa za muda mrefu na muda wa kati.
Family Smile Organization tunaungana na watu wote duniani, kupaza sauti yetu siku ya leo kupinga matumizi ya bidhaa za tumbaku. Pia kuwakumbusha wavutaji wasivute sigara kwenye mikusanyiko ya watu, kwa sababu wanaumiza watu wengine kiafya na hata kero ya harufu ya moshi wa sigara.
Tunakutakia kheri ya mwezi mpya, mwezi Juni. Ufanikiwe kwenye mipango yako.


Na, 
Nobel Edson Sichaleh,
Fasmo Tanzania,
Consumer Scientist,
0783961492

Comments

Popular posts from this blog

Mitindo Yetu Ya Ulaji.

Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.

MADHARA YA UTENGANO WA KIJAMII YALIYOSABABISHWA NA COVID19