FAIDA ZA KUFANYA UCHUNGUZI WA KIAFYA MARA KWA MARA
Faida za kufanya uchunguzi wa kiafya mara kwa mara.
Kuna kampeni nyingi zinazohamasisha watu kufanya uchunguzi wa afya zao juu ya gonjwa fulani au hata juu ya hali ya afya ya mwili wote kwa ujumla. Kampeni kubwa ni za kuhamasisha kupima Virusi Vya Ukimwi (VVU) pia kupima chanzo cha homa "Sio kila homa ni Malaria". Pamoja na hayo kuna kampeni nyingi za kuhamasisha wanawake kupima hali zao afya hususani kwenye mifumo ya uzazi (saratani ya matiti na shingo ya uzazi)
Licha ya jitihada nyingi za kuhamasisha watu kupima na kujua hali zao za kiafya zinazofanywa na serikali pamoja na asasi za kiraia lakini bado muamko wa watu umekuwa mdogo.
Sababu zinazofanya muamko uwe mdogo ni pamoja na hali ya uchumi, wengi kipato chao ni kidogo kiasi hata kupata milo mitatu ni mtihani.
Sababu zingine ni pamoja na uelewa mdogo juu ya umuhimu wa kuchunguza afya zao, baadhi ya Bima za Afya haziruhusu uchunguzi wa kiafya kwa asiye mgonjwa. Utaratibu ni kwamba huwezi kupima magonjwa mbalimbali kama hauumwi chochote hivyo. Hii hupelekea watu kusubiri kuumwa ndiyo kufanya vipimo kitu ambacho si tena kujua hali ya afya bali ni kujua hali ya ugonjwa.
Sababu nyingine kubwa ni mitizamo ya woga. Watu wengi hususani Watanzania wanaamini kupima wakati hauumwi ni kujitafutia magonjwa, ni kujiweka katika msongo wa mawazo. Hivyo wengi husubiri waumwe ndiyo wapime ila hivi kawaida umekuwa sio utamaduni wetu kupima.
Kiukweli kuna umuhimu mkubwa na faida nyingi za kufanya uchunguzi wa afya zetu mara kwa mara.
1. Faida ya kwanza kubwa ni kujua hali yako ya afya.
Kupima afya kunasaidia kubaini hali ya mwenendo wa afya. Kama mtu alikuwa mgonjwa kupitia vipimo itasaidia kujua maendeleo yake ya kimatibabu. Pia kama mtu anajisikia dalili kadhaa zisizo za kawaida mwilini uchunguzi utasaidia kujua haswa tatizo ni nini. Na kama mtu mzima ya afya uchunguzi utaeleza hali ya utendaji kazi wa viungo vyake na mifumo ya mwili na atapewa ushauri wa jinsi ya kutunza afya yake ili asipatwe na matatizo ya kiafya.
2. Inasaidia kubaini ugonjwa katika hatua za awali hivyo kusaidia kupambana nao kabla haujawa kubwa na hatari. Kwa mfano mtu anapima afya na kuonyesha dalili za saratani fulani hatua kadhaa za kitabibu zitachukuliwa kumsaidia kuthibiti hiyo saratani. Watu wengi waliobainika wana saratani mapema, waliweza kupambana nazo kuliko wale waliobainika wana saratani katika hatua ambayo saratani ilishasambaa sana.
3. Inasaidia kuboresha afya.
Kwa kupitia ushauri wa kitabibu mtu anaopewa baada ya uchunguzi utamsaidia kuboresha afya yake.
4. Inapunguza gharama za huduma za kiafya. Kitendo cha mtu kupima ugonjwa na kuanza kuchukua tahadhari mapema kujizuia kupata ugonjwa hakuna gharama sana kama gharama za kupambana na ugonjwa wenyewe. Kinga ni bora kuliko tiba. Kinga haina gharama sana kama gharama za kutibu ugonjwa.
5. Inajenga mahusiano mazuri kati ya mpimwaji na mtaalamu. Mtu anayechunguza afya yake mara kwa mara hujijengea ukaribu na daktari kiasi kwamba huwa ni rahisi kwake kusaidika ukimlinganisha na yule ambaye hana mazoea ya kuchunguza afya yake.
6. Inaongeza kujiamini kwa mtu.
Msafiri anayejua anakwenda wapi na ubora wa usafiri anaoutumia huwa anajiamini kuliko yule ambaye halijui gari analosafiria na hajui huko aendako atafika saa ngapi naatafikia wapi. Vivyo hivyo kwa afya zetu, mtu anayejua afya yake anakuwa wakujiamini kwakuwa anajua nini kinaendelea mwilini mwake kuliko yule ambaye hajui haki yake anakuwa wakujishtukia na hofu... hivi itakuwaje kama naumwa? Nikiwa naumwa nitakuwa nimepataje huo ugonjwa??
Fasmo Tanzania tunaungana na asasi zote katika kada ya afya zinazopigia upatu watu kujijengea tabia ya kufanya uchunguzi wa afya zao(check up). Kwa manufaa tuliyoyaainisha hapo juu ni matumaini yetu mwamko utaongezeka kwa wanajamii.
Na
Nobel Edson Sichaleh.
Fasmo Tanzania.
Comments