Mpango Binafsi wa Afya.

Tanzania ni moja ya nchi zilizopo kusini mwa jangwa la sahara zenye idadi kubwa ya watu. Licha ya serikali ya Tanzania kufanya jitihada nyingi katika kupambana na maadui watatu ambao ni Ujinga, umasikini na Maradhi bado kuna changamoto kubwa kwenye jamii za Kitanzania hususani kwenye afya na lishe. Watu wengi bado hawana elimu toshelezi juu ya ulaji bora na mitindo mizuri ya maisha itakayowaepusha na matatizo ya kiafya na kilishe.

Idadi kubwa ya Watanzania bado ina jikongoja katika kukamilisha milo mitatu kwa siku. Huku idadi kubwa zaidi ikiwa bado gizani katika kupangilia makundi ya vyakula katika mlo. Yote haya yanasababishwa na ukosefu wa elimu ya lishe kwa sehemu kubwa na pia umasikini unachangia kwa sehemu hali kuwa mbaya zaidi. Kwa kuwa wapo wenye uwezo wa kula watakavyo (idadi kubwa ya milo) lakini bado hawaipangilii vizuri.

Changamoto nyingine iliyopo kwenye afya na lishe kwa Watanzania wengi ni ukosefu wa tamaduni au tabia ya kuzingatia kanuni za mambo mbalimbali. Maisha yetu yamejengeka kwenye mazoea ya jinsi tulivyolelewa. Na katika malezi ya wengi wetu hatupendi kanuni. Hatupendi kufuata mlolongo wa kitu.. ila tunapenda sana mambo yaende haraka na kwa mafanikio huku tukisahau mafanikio huja kwa kanuni. Hili ndilo husababisha namna fulani za ulaji na utunzaji wa afya.

Mbio mbio za maisha pia ni moja ya sababu ya baadhi ya watu kula chakula bila mpangilio mzuri wa makundi ya chakula hivyo kupelekea kukosa baadhi ya virutubishi na wengine kupata uzito uliopita kiasi. Watu wanakosa muda wa kutosha kuamua walaje wanajikuta wanakula vilevile kama jana (Wali maharage kabichi). Hali hii huwapata zaidi watu wanaofanya kazi mbali na sehemu zao za kuishi hivyo hula kwenye migahawa kwa menyu sare siku nenda siku rudi.
Lakini kati ya yote hayo, tatizo la ukosefu wa elimu ya lishe limekuwa changamoto kubwa kwa Watanzania wengi. Elimu ya lishe sio tu kujua makundi ya vyakula.. Hapana, elimu ya lishe inampasa mtu kuyajua makundi ya vyakula na mpangilio wake katika mlo. Elimu ya lishe haiishii katika kujua mpangilio wa makundi ya vyakula katika milo lakini inaenda zaidi katika Kupangilia makundi hayo sawa na uhitaji wa afya au mwili wa mlaji. 

Jamii zetu nyingi tunakula bila kuzingatia uhitaji wa mwili. Umepikwa wali maharage basi tutakula wote hicho chakula. Baba aliyeshinda akifanya kazi ngumu, mtoto wa miaka miwili, mama aliyeshinda nyumbani na dada mjamzito wote tutakula. Wakati kiukweli sisi wote tunatofautiana uhitaji kuanzia virutubishi mpaka kiasi cha kwenye sahani. 
Hii ndiyo sababu wengine kunenepeana sana, wengine kudumaa na wengine kukosa lishe. Lakini tatizo hili linaanzia kwenye ngazi ya familia na kuendelea hukohuko kwa miaka na miaka. Hivyo mabadiliko inabidi yailenge familia.

Katika mabadiliko ni vyema sana kuwekeza katika kuelimisha kizazi kinachofuata yani kuwapa elimu ya lishe watoto tangia wakiwa na umri mdogo ili kadri wanavyokua wanazidi kuelimisha ndugu na majirani na baadae watakapo kuwa na miji yao basi wafuate taratibu na kanuni za ulaji bora na utunzaji wa afya kwenye familia zao. Na  huo ndiyo utakuwa ukombozi wa familia na jamii zetu.

Kwa kusema hayo ni dhahiri kuna umuhimu elimu ya lishe kuanza kutolewa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari. Utolewaji huo waweza kuwa Lishe kama somo, au Lishe kama jambo la ziada katika mazingira ya shule. Kama itashindikana lishe kuwa Somo linalojitegemea basi ni vyema mada ya  Lishe iongezwe vitu kwenye somo la Sayansi. Vitu hivyo vitakavyoweka msingi mzuri wa elimu ya lishe kwa wanafunzi.
Lishe ya shule za msingi isiishie kutajwa kwa makundi ya vyakula na faida zake. Lakini ijikite pia kuhamasisha ulaji wa vyakula fulani kama mbogamboga, maziwa, samaki na matunda huku pia ikipinga ulaji wa vyakula venye sukari nyingi, chumvi nyingi, vyakula vyenye ubaridi na namna zingine za ulaji usiofaa.

Jambo moja zuri, nchi yetu imejaliwa vyakula mbalimbali, kuna mbogamboga nyingi, maziwa, mito, mabwawa na bahari vinavyotupatia samaki na dagaa wa aina nyingi. Pia Tanzania ni nchi ya pili Afrika kwa kuwa na ng'ombe wengi hivyo maziwa na nyama hupatikana kwa wingi. Tatizo ni elimu juu ya ulaji kwa wengi na hali ya uchumi. Kwenye hali ya uchumi hata kama mtu hawezi kununua kilo moja ya nyama lakini anaweza kununua dagaa au mayai ambayo yapo kundi moja la chakula. Hali ipo hivyo kwenye vyakula vyote, hakuna kundi la chakula lenye vyakula vya gharama pekee. Kila kundi lina vyakula vingine vya bei rahisi na upatikanaji rahisi.
Msingi wa Lishe Bora
Msingi wa Lishe bora ni utoaji wa elimu kwa wanajamii hususani tangia wakiwa na umri mdogo kama njia ya kuweka msingi wa maarifa ya ulaji bora ili kuiepusha jamii na matatizo ya kilishe na kiafya katika miaka ya mbeleni. Utoaji huu wa elimu mashuleni hususani shule za msingi utasaidia mambo kadhaa...
1. Watoto kupata maarifa na uelewa juu ya vyakula na namna nzuri za ulaji zinazoendana na uhitaji wa mwili na afya ya mtu.
2. Kutasaidia elimu kusambaa kwa watu wengi. Nyumba nyingi zina watoto wanaosoma hivyo kama wataelimishwa vizuri kule shuleni na hata kurudi na vipeperushi nyumbani watu wa nyumbani nao wataipata elimu na mabadiliko yatapatikana.
3. Miaka ijayo matatizo ya afya yatokanoyo na lishe kama kisukari, presha na mengineyo kupungua kwa kiasi kikubwa kwa kuwa watu wengi watakuwa na elimu ya ulaji bora na kuelimishana juu ya namna nzuri za lishe na mitindo ya maisha.
4. Mahudhurio shuleni kuongezeka. Wenda pia mahudhurio yakazidi kuongezeka. Wanafunzi wanapenda vitu vyepesi wanavyotumia kila siku kwenye maisha ya kawaida. Akisikia somo kuhusu lishe anavutiwa sana.

Elimu hii ikitolewa na kupewa nguvu na wanajamii na idara mbalimbali za serikali na binafsi itasaidia elimu hii kufikia wanafunzi wengi hivyo kuibadili jamii kubwa na kujenga taifa lenye afya.


Na
Nobel Edson Sichaleh
Fasmo Tanzania
0783961492

Comments

Popular posts from this blog

Mitindo Yetu Ya Ulaji.

Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.

MADHARA YA UTENGANO WA KIJAMII YALIYOSABABISHWA NA COVID19