UNYONYESHAJI NA FAIDA ZAKE

UNYONYESHAJI 
Wiki ya unyonyeshaji duniani ni kampeni ya dunia nzima inayoadhimishwa na nchi mbalimbali kila mwaka katika wiki ya kwanza ya mwezi wa nane (tarehe 1 hadi 7 mwezi wa nane) inayolenga kuhamasisha unyonyeshaji sahihi wa maziwa ya mama ili kuimarisha afya za Watoto. Katika mwaka 1992 ndipo wiki ya kwanza ya unyonyeshaji duniani iliadhimishwa.
Kama ilivyokuwa miaka ya nyuma wiki ya kwanza ya mwezi wa nane (Agosti) kuadhimisha kwa wiki ya unyonyeshaji duniani, kauli mbiu ya mwaka huu ilikuwa“Tuwawezeshe Wanawake Kunyonyesha Watoto kwa Afya Bora na Ulinzi wa Mazingira”. lengo likiwa ni kuwasaidia wazazi na wahudumu wa nyumbani kutoa huduma inayostahili kwa watoto tangu mama akiwa mjamzito, anapojifungua na hata baada ya kujifungua.
Katika kuambatana na kauli mbinu ya mwaka huu, shirika la Afya duniani (WHO) na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) wamelenga katika kushauri na kuziita serikali kuhakikisha zinalinda na kuchangia upatikanaji ushauri nasaha na elimu ya unyonyeshaji iliyosahihi kutoka kwa wataalamu wa afya, ambayo ni sehemu muhimu katika kuhakikisha unyonyeshaji unafanikiwa vizuri na kwa ufanisi wa hali ya juu kupitia:

KUWEKEZA: ili kuhakikisha kuna wataalam wa utoaji ushauri nasaha kuhusu unyonyeshaji na wanapatikana kwa kila mwanamke. Na hilo linahitaji kuongeza ufadhili wa programu za unyonyeshaji na kuboresha mfumo wa ufuatiliaji na utekelezaji wa sera, mipango na huduma. 

MAFUNZO: Kuwapa mafunzo wahudumu wa afya wakiwemo wakunga na wauguzi ili waweze kutoa ushauri nasaha wa kitaalamu kuhusu unyonyeshaji kwa kina mama na familia. 

KUHAKIKISHA: Kwamba ushauri nasaha unapatikana kama sehemu ya utaratibu wa kila siku wa huduma za afya na lishe ambazo zinapatikana kwa urahisi. 
UBIA: Na ushirikiano na asasi za kiraia na jumuiya za wataalamu wa afya, kujenga mifumo imara ya ushirikiano kwa ajili ya kutoa ushauri nasaha unaostahili. 
Unyonyeshaji wa maziwa ya mama ni muhimu kwa mtoto kwani humpa mtoto mwanzo mzuri wa maisha. Siku 1,000 za mwanzo za maisha ya mtoto tangu akiwa tumboni mwa mama yake ni muhimu sana katika ukuaji wa ubongo hali.
Hii pia itaamua mustakabali wa mtoto, jinsi gani uwezo wake wa kufikiria utakuwa, kujifunza na tabia yake. Lishe muafaka, ikiwemo maziwa ya mama ni ufunguo wa kila kitu. Lakini pia huimarisha uhusiano kati ya mama na mtoto.
Unyonyeshaji wa maziwa ya mama sio jambo rahisi sana, kuna changamoto nyingi. Hivyo basi ushirikiano na msaada kutoka katika familia na jamii kiujumla ni muhimu katika kufanikisha suala la unyonyeshaji. Ushirikiano na msaada kutoka katika jamii yetu huhitajika kuhakikisha mama anaanza kumnyonyesha na muhimu zaidi kumhamasisha mama kuendelea kumnyonyesha mtoto kwa kipindi chote kama inavyoshauriwa na wataalamu.
Ufanikishaji wa unyonyeshaji si suala linalotegemea huduma zitolewazo na vituo vyetu vya kutoa huduma ya afya pekee, ila ni jukumu la jamii nzima. Familia au kaya huwajibika katika njia moja au nyingine ili kulinda kuendeleza na kuweza kufanikisha unyonyeshaji. Jamii ina wajibu wa kuwawezesha wazazi, hususani wanawake waweze kunyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo baada kujifungua. Na baada ya miezi sita waweze kuwapa watoto vyakula vya nyongeza, vyenye ubora kilishe huku wakiendelea kunyonyeshwa hadi watakapotimiza umri wa miaka miwili.
Akina mama wanahitaji muda wakutosha ili waweze kunyonyesha watoto kwa muda mrefu kila mtoto anapohitaji na kunyonyesha mara nyingi. Hii itawasaidia matiti yao kutengeneza maziwa mengi zaidi. Familia inaweza kusaidia kumpunguza kazi mama anaenyonyesha
Lakini pia jamii inayomzunguka mama anaenyonyesha inapaswa kutokuwa chanzo cha msongo wa mawazo kwa mama anaenyonyesha kwa namna yoyote ile, kwani msongo wa mawazo kwa mama mjamzito huathiri uzalishaji wa maziwa na hivyo mtoto anaweza asipate maziwa yakutosha pale anaponyonya. 

Kuna faida nyingi za kunyonyesha maziwa ya mama, kama inavyoelezewa hapo:
Kwa mtoto 
●Humpatia virutubisho kwa uwiano sahihi kwa ukuaji na maendeleo yake.
●Humpatia kinga dhidi ya maradhi mbalimbali kama kuhara na magonjwa ya njia ya hewa.
●Huyeyushwa kwa urahisi na kufyonzwa na mwili kwa ufanisi. 
●Huleta uhusiano mzuri na wa karibu kati ya mama na mtoto. 

Kwa mama 
●Husaidia tumbo la uzazi kurudi katika hali yake ya kawaida mapema; 
●Huchangia kuzuia upungufu wa damu kwa kuzuia utokaji wa damu kwa wingi baada ya kujifungua na husitisha kwa muda damu ya hedhi (LAM)
●Huzuia uwezekano wa kupata ujauzito katika miezi 6 ya mwanzo.
●Hupunguza uwezekano wa kupata saratani ya ovari na matiti; na 
●Humsaidia mama kurudia umbile lake la kawaida mapema. 

Faida nyingine za maziwa ya mama.
■Ni safi na salama, hupatikana muda wote katika joto sahihi na hayahitaji matayarisho; 
■Hayaharibiki yakiwa ndani ya matiti. Yakikamuliwa hukaa saa 6 mpaka 8 bila kuharibika katika joto la kawaida saa 24 katika la kawaida na saa 72 kwenye jokofu la kugandisha
■Gharama yake ni ndogo ukilinganisha na ile ya maziwa mbadala
■Huokoa muda wa mama na fedha za familia.
■Hayaleti matatizo ya mzio na hutunza mazingira kwani hayaachi mabaki kama makopo au chupa.


Imeandaliwa na,
Happyness Kisanga
Afisa Lishe (NuO)

Kwa msaada wa Makala mbalimbali kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF, Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), na wadau wengine wa Afya na Lishe

Comments

Anonymous said…
Ahsante kwa elimu hii
Fasmo Tanzania said…
Tunashukuru kwa mrejesho

Popular posts from this blog

Mitindo Yetu Ya Ulaji.

Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.

MADHARA YA UTENGANO WA KIJAMII YALIYOSABABISHWA NA COVID19