Je Mazingira ya Shule nchini yanachukua tahadhari kuwalinda watoto na magonjwa?

Dunia ikiwa bado ikipambana na janga la Korona na nchi nyingi zikiwapatia wananchi wake chanjo na kulegeza sheria za tahadhari za kupambana na gonjwa hilo ambalo linaambukizwa kwa njia ya hewa. Baadhi ya nchi ziliwahi sana kuruhusu shughuli za masomo kwa wanafunzi wa shule za msingi hadi chuo huku zikitoa masharti ya kuzingatiwa wakati wa masomo. 
Moja ya nchi hizo ni Tanzania, bila kutazama sana jinsi nchi yetu ilivyopambana na janga la Korona makala hii fupi imejikita katika kuangalia kwa makini mazingira ya shule hususani za msingi na sekondari jinsi yanavyoweza kulinda afya za wanafunzi au kuchochea maambuzi ya magonjwa mbalimbali yenye mfanano wa namna ya kuambukizwa na kukumba watu wengi. 

Mazingira ya usafi wa madarasa, vyoo vya wanafunzi, uwepo wa maji tiririka ya kunawa na usafi kwa jumla kwa shule nyingi za msingi za serikali bado ni kitendawili. Hii kwa shule zote bila kujali eneo iliyopo, shule zilizopo mjini zina changamoto zake lukuki ikiwemo mazingira ya uuzaji wa chakula katika eneo la shule kama maandazi, ubuyu, barafu, kashata, sambusa nk
Huku kwa shule zilizopo vijijini au pembezoni mwa jiji changamoto kubwa kwao ni uhaba wa maji.

Changamoto na hali ilivyo.
●Miundombinu ya madarasa na samani. Uchakavu wa madarasa na madawati unaweza chukuliwa si kitu kikubwa kwa kuwa umezoeleka kuwepo lakini. Mtoto kujifunzia kwenye darasa bovu inamuathiri kiakili na kiafya. Kitendo cha kukaa chini au kwenye dawati ambalo kwanza wamesongamana na pia muda wowote linaweza vunjika au msumari kumchoma linaiweka hali ya afya ya mtoto katika mashaka. 
Kuna madarasa hayana nyavu madirishani hili lilisababisha shule moja kuvamiwa na nyuki na kusababisha taharuki kubwa kwakuwa nyuki waliingia madarasani,  shule zingine zina madarasa hayana sakafu na kuta zimeharibika kiasi cha kuweka hofu ndani ya mwanafunzi.

●Miundombinu ya maji
Uhaba wa maji na ubovu wa mifumo ya maji pia ni changamoto katika shule nyingi. Na changamoto hii hufika kiasi kuathiri waalimu pia. Kukuta shule haina chanzo cha maji ni jambo la kawaida sana, shule haina bomba wala tenki la maji ya mvua si kitu cha kushanganza katika jamii yetu. Hali hii hupelekea shule kutumia maji yaliyotwama, maji ya mito iliyokaribu vitu ambavyo vyote kwa pamoja vinahatarisha usalama wa afya za wanafunzi kwa kuwa maji hayo si salama na huyatumia kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kunawa na chooni.
 Juu ya hayo shule zingine hufika hatua kuwaagiza wanafunzi waje na maji kwenye vidumu jambo ambalo nakiri linachochea usafi lakini nina shindwa kujizuia kujiuliza juu ya usalama wa maji hayo kwa kuwa yanatoka vyanzo tofauti na hakuna anayezingatia usalama wa maji, mwanafunzi anabeba ili kuepuka adhabu.

●Miundombinu ya vyoo
Hapa ndipo changamoto ni kubwa zaidi. Shule nyingi zinakumbwa na changamoto hii. Baadhi ya shule hazina vyoo, zingine zina vyoo vibovu ambavyo vinaweza anguka muda wowote au vimejaa hivyo uchafu na harufu kusambaa, shule zingine zina vyoo visivyoendana na idadi ya wanafunzi (tundu chache) hivyo kuleta msongamano na kuchangia uchafuzi mkubwa wa vyoo. Pia changamoto ya ubunifu wa vyoo kutozingatia matumizi kwa walemavu. Magonjwa ya mlipuko kama kuhara na magonjwa ya ngozi husambaa sana kwa wanafunzi kupitia miundombinu mibovu ya vyoo.
Tumeshuhudia wanafunzi wakijisaidia vichakani, wanafunzi wakichangia choo na waalimu na pia wanafunzj wakipeana zamu ya kutumia choo. Baadhi ya changamoto za vyoo zinaweza tatuliwa na shule yenyewe kwa kuwa madhubuti katika kusimamia miundombinu na usafi ya vyoo na changamoto zingine ni jamii na serikali kutopuuzia vyoo katika ujenzi au usimamizi wa shule. 
Kwa leo tuishie hapa tutaendela siku nyingine kuelezea changamoto zingine wanafunzi wanazopitia na namna ambayo jamii tunaweza kusaidia kuokoa jahazi hili kwa kuwa ni wazi mazingira ya shule nyingi za msingi na sekondari si rafiki. Na si huko tu hata vyuo vyetu vikuu, mwaka 2018 hayati Magufuli alitembelea moja ya chuo kikuu na mwanafunzi mmoja alisema wanachangamoto ya miundombinu mibovu ya vyoo na mabafu. Hii inaweza kukupa picha maeneo mengine ya kielimu ambayo hayana fungu kubwa wala usimamizi mkubwa wana kumbwa na hali gani.

Fasmo Tanzania
Nobel Edson Sichale.

Comments

Popular posts from this blog

Mitindo Yetu Ya Ulaji.

Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.

MADHARA YA UTENGANO WA KIJAMII YALIYOSABABISHWA NA COVID19