Mitindo Yetu Ya Ulaji.
MITINDO YA ULAJI
Viumbe hai vyote akiwemo na mwanadamu huitaji chakula ili kuishi. Mwanadamu ana mahitaji makuu matatu na chakula ni hitaji muhimu zaidi ya mengine ambayo ni mavazi na malazi.
Kwa umuhimu wa chakula, mwanadamu huitaji kula kila siku. Na inapotokea hajala au kavusha mlo kuna utofauti hujisikia. Utofauti huo waweza kuwa upungufu wa nguvu mwilini, kizunguzungu, na wengine hujisikia uwepesi wa mwili. Wewe ukishikwa na njaa unakuwaje au tabia gani hujitokeza?
Watu wanamitindo mbalimbali ya ulaji. Mitindo ya idadi ya milo, wakati wa kula, aina ya vyakula na kiasi cha chakula na hii hutokana na sababu kadhaa. Sababu kama za kiuchumi, mazoea, ratiba ya mtu, sababu za kidini, umri, hali ya mwili na kiafya ya mtu husika pamoja na mazingira na upatikanaji wa vyakula.
Kama picha inavyoonyesha hapo watu 4500 walioonyesha wao hula milo mingapi ndani ya masaa 24 yani milo kwa siku. Wapo wa mlo mmoja hadi milo minne na kuendelea. Kwani wewe unakula milo mingapi kwa siku na kwa nini? Waweza shirikisha jibu lako mwisho la hili bandiko sehemu ya maoni.
Hivi watu wa kale, zamani hizo walikuwa wanakulaje? Hii milo mitatu ambayo ndiyo mtindo maarufu na ndiyo kama kiwango cha ulaji mzuri ulianzia wapi? Je huu mtindo wa milo mitatu ni mzuri kwa afya kwa kiasi kipi?
Maswali ni mengi sana juu ya mitindo ya ulaji. Wingi huo wa maswali na utofauti wa majibu unatokana na tofauti zetu za kitamaduni, kimazingira, kiafya na kidini.
Dini na mitindo ya ulaji
Dini mbalimbali au tuseme dini zote zina namna zake za miongozo ya ulaji kwa waumini wake. Miongozo hio ni kama kukatazwa kwa aina fulani ya chakula, kuhamasishwa kwa aina fulani ya vyakula, miongozo ya kujizuia kula kama sehemu ya ibada( Mfungo). Pia kuna majumuiko ya kidini yanayoambana na elimu ya kiafya, lishe na chakula. Hivyo basi, ulaji wa mtu aliyeshika dini si sawa na ambaye hajashika. Na mshika dini hii anatofauti za mtindo wa ulaji na mshika dini nyingine.
Kuna rafiki yangu mmoja yeye ni anapenda kula milo miwili, mtaani tunaita pasi ndefu yaani akila asubuhi, kula tena ni jioni. Nikamuuliza kwa nini milo miwili akanijibu kwa kutumia mkasa wa Nabii Eliya kutoka kwenye biblia.
Kisa hicho ni kwamba kulitokea ukame na njaa kali kwenye hiyo nchi, Mungu kwa uweza wake akawa anamtuma kunguru ampelekee Nabii Eliya mkate na nyama kila asubuhi na jioni. (1Wafalme 17:1-6).
"Hivyo basi, kama Mungu aliona milo miwili kwa siku yamfaa mwanadamu basi milo mitatu ni anasa". Huo ndio ufafanuzi wa rafiki yangu ambaye naamini siku akijipata kiuchumi atakula milo minne yenye mboga saba. Hahaha! Kwani wewe unasababu zipi za milo unayokula?
Afya na mitindo ya ulaji.
Afya ni suala pana kiasi, kwa kuwa inaambatana na mambo kama umri wa mtu, hali ya afya yaani uzima au ugonjwa mwilini, uzito wa mtu, shughuli za mwili na mazingira ya nje ya mwili yanayochochea mabadiliko mwilini kama vile hali ya hewa. Lakini yote haya yanatupa picha moja juu ya afya ambayo ni mtindo wa ulaji kutokana na uhitaji na mahitaji ya mwili.
Ulaji wa mjamzito na mwanamke anayenyonyesha ni tofauti na mwanamke ambaye hapitii mabadiliko hayo ya kimwili. Wanatofautiana mahitaji ya kilishe.
Mtindo wa ulaji wa mtoto mchanga ni tofauti ya mtoto mwenye miaka mitatu na tofauti kabisa na mtu mzima. Na hii ndiyo sababu ya udumavu kwakuwa mtu mzima anataka kumlisha mtoto mchanga chakula kisichoendana na umri wake na unakuta anamlisha masaa ambayo na yeye mtu mzima kazoea kula. Wakati mtoto mchanga (miaka 0-2) anahitaji maziwa ya mama kwa miezi sita ya kwanza bila kumpa kitu kingine na baada ya muda huo ananyonyeshwa pamoja na kupatiwa chakula kilaini kutoka makundi yote ya vyakula kila baada ya muda mchache na sio asubuhi-mchana-jioni kama mtu mzima.
Wazee nao kwa sababu za kiafya na mahitaji ya mwili mtindo wao wa ulaji ni tofauti kidogo na vijana. Endelea kufuatilia ukurasa huu kwa elimu zaidi na ya kina juu ya namna nzuri ya ulaji na uandaaji wa chakula kwa wazee.
Magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu, kiharusi, magonjwa ya Figo na moyo huhitaji mitindo tofauti ya ulaji. Mgonjwa hula chakula kiutofauti kwenye aina ya upishi, kiasi cha chakula na muda wa kula.
Mazingira na mtindo wa ulaji.
Kisayansi inatarajiwa ulaji wa watu waishio Dar-es-salaam na mikoa yote ya Pwani uwe tofauti na mtindo wa ulaji wa watu waishio Mbeya na mikoa ya nyanda za juu kusini. Kutokana na mwili kuhitaji chakula zaidi kuthibiti baridi kuliko kuthibiti joto. Hivyo ni sawa na kusema, kama watu wa Dar-es-salaam na Mbeya wakawa na mfanano wa aina ya chakula, kiasi cha chakula na muda wa kula kwa kipindi cha mwaka mmoja ni lazima upande mmoja utakuwa na utapia mlo mkubwa. Ni upande upi huo? Waweza kuweka jibu lako kwenye maoni
Itaendelea...
Comments