Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.
MAZIWA MAZIWA MAZIWA!
Tulipokuwa shuleni tulijifunza makundi ya Wanyama kulingana na sifa zao. Moja ya kundi hili ni mamalia ambao sifa yao kuu ni Wanyama wanaonyonyesha akiwemo popo, binadamu, mbwa, ng’ombe, mbuzi, kondoo nk. Wanyama hawa hufanya hivi kwa kipindi fulani na kuacha kunyonyesha mtoto/watoto wao. Kwa mfano, ndama wa ng’ombe huachishwa akiwa na umri wa miezi 4 hadi 5, baadhi ya jamii za nyani huendelea kunyonyesha watoto wao hadi wanapofikia umri wa miaka 4 wakati tembo huendelea kumnyonyesha mtoto wake hata akiwa na umri wa Zaidi ya miaka 2. Hii ina maanisha kila mnyama anaezalisha maziwa ni kwa ajili ya mtoto/watoto wake tu. Pia tutakubali kuwa kila mnyama ana tabia zake katika kumuachisha mtoto wake kunyonya.
Kwa binadamu, inashauriwa mtoto anyonyeshwe hadi atakapotimiza umri wa miaka 2 na ikiwezekana aendelee kunyonyeshwa, ingawa watu wengi hawafanyi hivyo. Wengine huishia mwaka mmoja na nusu na kuacha kumnyonyesha mtoto wake.
Leo ni kilele cha maadhimisho ya Siku ya maziwa duniani. Siku hii huadhimishwa Juni 1 ya kila mwaka. Maadhimisho haya yalianzishwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa mwaka 2001 ili kuonyesha umuhimu wa maziwa kama chakula bora na kutambua mchango wa sekta ya maziwa duniani. Ni takribani miaka 23 tangu maadhimisho yaasisiwe. Kulingana na takwimu za shirika la chakula na kilimo la umoja wa mataifa takribani watu bilioni 2 wameajiliwa/kujiajili katika sekta ya maziwa wakati Zaidi ya watu bilioni 6 ulimwenguni kote hutumia bidhaa zitokanazo na maziwa.
Leo, ulimwengu mzima unasherehekea siku hii ili kuashiria umuhimu wa matumizi ya maziwa katika lishe yetu.
Maadhimisho ya Kitaifa kwa Mwaka 2024 yanaenda sambamba na kauli mbiu isemayo; 'Kunywa Maziwa Salama kwa Afya Bora na Uchumi Endelevu
Kama kilele cha wiki ya maziwa duniani, nchini Tanzania, maadhimisho haya hufanyika kuanzia tarehe 26 Mei na kuendelea hadi siku ya kilele, tarehe 1 Juni.
Sherehe hizi kitaifa zinafanyika mkoani Tabora, zikiwaleta pamoja wadau mbalimbali katika kuangazia mafanikio, teknolojia bora, ubunifu mpya na mafunzo mapya yanayojiri katika sekta hii.
Jukwaa la Maziwa Ulimwenguni na idara mbalimbali za maziwa za nchi nyingi zimekuwa zikiadhimisha kwa kufanya mikutano na wadau na washiriki kuzungumza juu ya faida za maziwa na kutafuta namna bora Zaidi ya kuwezesha mafanikio katika sekta hii. Kwa pamoja wadau huangazia changamoto za kupata maziwa na bidhaa zake sehemu mbalimbali ulimwenguni.
Unywaji wa maziwa nchini Tanzania bado upo chini. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) yampasa mtu mmoja kunywa lita 200 kwa mwaka. Tovuti za Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) Zinasema Mtanzania hunywa wastani wa lita 62 tu kwa mwaka (ongezeko la lita 15 kutokea mwaka 2020 ambapo ilionyesha mtu mmoja kunywa lita 47). Kwa kulinganisha na majirani zetu Kenya ambao kiwango chao ni lita 140, kiwango hiki ni kidogo sana kwani ni mara 2.3 ya kiwango ambacho Mkenya mmoja hunywa kwa mwaka.
Taarifa kutoka TDB kupitia mradi wa unywaji wa maziwa mashuleni (2018) inaonesha kuwa hali ya unywaji wa maziwa mashuleni bado ni ndogo sana, kwani jumla ya watoto 39,252 tu katika mikoa 6 ndio walionekana kutumia maziwa. Kwa kuzingatia umuhimu wa lishe bora kwa watoto mashuleni na ukuaji endelevu, maziwa yanaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa kutengeneza kizazi cha watoto wenye afya thabiti.
Ingawa Tanzania ni moja kati ya nchi zenye Wanyama wengi wakufugwa wakiwemo ng’ombe, mbuzi, kondoo kama Wanyama wanaotoa maziwa, hali ya matumizi ya maziwa na vyakula vingine vitokanavyo na Wanyama bado ni HAFIFU SANA.
Watanzania wengi hatunywi maziwa ipasavyo kwasababu ya uelewa mdogo na hatuzijui faida za maziwa mwilini. Watu wengi hudhani maziwa ni kwa ajili watoto wadogo, watu waliotoka kufanya kazi sehemu zenye vumbi sana au mtu aliyekunywa au kula sumu, lahasha mawazo haya sio kweli kwani maziwa yana faida lukuki.
UMUHIMU WA MAZIWA KWA AFYA YA MNYWAJI
Fasmo tunapenda kutumia siku ya maziwa duniani kukuelimisha mwananchi na umma kuhusu matumizi ya maziwa kama chakula bora kwa watu wa rika zote na faida za maziwa katika kujenga afya zetu. Umuhimu wa maziwa katika lishe na afya bora ya binadamu unatokana na:
● Kuwa na protini nyingi, bora na rahisi zaidi kwa ajili ya kujenga mwili
● Kuwa na vitamini A, B, na D kwa wingi kwa ajili ya kulinda mwili na kuimarisha mifupa, kuwa na ngozi nyororo na kuzuia upofu
●Kuwa na madini kwa wingi hasa ya kashiamu na fosfolasi kwa ajili ya kujenga mifupa na meno imara
● Kuwa na mafuta mazuri (samli/siagi) ambayo yanaweza kutumika kupikia vyakula vingine.
●Kuwa na maji yanayowezesha mwili kuyeyusha viinilishe ili viweze kutumika vizuri mwilini na
● Kuwa ni chakula kamili kinachojitegemea kwa kuwa na viinilishe vyote muhimu vinavyohitajika mwilini kwa pamoja.
TUKUMBUKE NINI KUHUSU MAZIWA YA KUNYWA
1. Je, wajua binadamu ndio kiumbe pekee ambaye huendelea kunywa maziwa baada ya kuachishwa rasmi kutoka kwa mama yake, lakini huendelea kunywa maziwa ya Wanyama wengine na sio ya mama yake. Mara nyingi maziwa ya ng’ombe hutumika ingawa yale yatokanayo na Wanyama wengine kama vile ngamia, mbuzi na hata kondoo hutumika hasa kwa maeneo ambayo ufugaji wa Wanyama hawa umeshamiri kama vile nchi za Afrika ya Kati, Mashariki, Magharibi (Somalia, Sudani, Ethiopia, Libya N.K).
2. Tujifunze matumizi ya maziwa kutoka kwa jamii za wafugaji (wamasai na makabila mengine ya jamii zao Tanzania na Afrika kwa ujumla) wamekuwa na mbinu mbalimbali ambazo wanazitumia hadi leo katika kuchakata maziwa na kuyatumia. Ingawa zinaweza zinakachukuliwa kama ni mbinu za kizamani na duni lakini uwezekano ni mkubwa kwamba ndio mbinu hizo zinazowafanya wao kuwa jamii za watu wenye afya thabiti duniani kutokana na ulaji wa vyakula vinavyoandaliwa kwa njia za kiutamaduni wao.
3. Namna ya uandaaji wa maziwa inachangia kwa kiasi kikubwa ubora wa zao litakalopatikana. Tupo katika kipindi ambacho kuna mageuzi makubwa ya teknolojia hivyo kufanya uchakataji wa vyakula kuwa mkubwa. Kuna namna za uandaaji wa maziwa zinazohusisha kuchemsha katika joto kubwa ili kuharibu vijidudu na kuongeza muda wa kuyatunza (mbinu kama Pasteurization, UHT n.k). mbinu hizi zinasaidia kutunza maziwa lakini haziyaachi kama yalivyokuwa baada ya kukamuliwa.
Ni vyema kuelewa kwamba maziwa huwa na baadhi ya vitu ambavyo huaribiwa katika joto kubwa ikiwemo vimeng’enya kama vile phosphatase - huitajika kwa ajili ya ufyonzwaji wa madini ya kalsiamu, lipase – huhitajika kwa ajili ya kumeng’enya mafuta. Pia hali ya maziwa (rangi na ladha) hubadilika baada ya kuchakatwa kwa mbinu hizi za kisasa.
Hivyo maziwa yaliyochakatwa viwandani kwa mbinu kama hizi yanapoteza vitu muhimu vya asili ambavyo vina faida kubwa kwenye mwili wa binadamu.
4. Usiyakimbie mafuta ya Wanyama hasa yatokanayo na maziwa. Ukiangalia kwa makini utakuta jamii za watu wengi ambazo zimekuwa zikitumia maziwa tangu zamani, zilikuwa na watu wenye afya bora na thabiti. Hata kimuonekano ni wembamba (Ingawa wembamba hauashirihi afya bora siku zote) na wana nguvu madhubuti (tuna mifano hai na ya karibu, wamasai (hasa wale wanaoishi umasai hadi sasa ni watu ambao mionekano yao inathibitisha hili hadi sasa – Unazani unaweza kumkabili Moran wa Kimasai). Hii inaenda mbali hadi kwa jamii za wafugaji hasa Afrika ya kati na mashariki/kaskazini kama vile Wasomalia, Ethiopia, Sudan n.k.
• Tunaweza kupata mafuta bora ya kutumia kutokana na maziwa almaarufu kama SAMLI. Vitu vingine ni kama SIAGI na hata mafuta yatokanayo na nyama za Wanyama. Kitu cha kushangaza ni kwamba watu wengi wanayakimbia wakidai kwamba yataganda mwilini na kupendelea kutumia mafuta ya mbegu za mimea (alizeti n.k) lakini ni hao hao ambao wanasumbuliwa na magonjwa ya moyo na mfumo mzima wa damu. Uzalishaji na matumizi ya mafuta haya unahitaji kupewa mkazo katika uzalishaji na matumizi yake.
5. Hakuna maziwa salama yanayozalishwa nje ya mwili wa mnyama wenyewe. Kasumba ya kutumia vitu vilivyo katika maboksi/makopo vikiambatana na picha pamoja na maneno mazuri hufanya watu wengi waamini kwamba bidhaa hizo ni bora kulingana na hadhi zao. Hii inawafanya hata watu wa hali ya chini kiuchumi kuamini kwamba wanahitaji kujikwamua ili waweze kununua vyakula kama hivyo, JAMBO AMBALO SIO SAWA NA LINASIKITISHA SANA.
Ukitaka kujua kwamba kuna madhara makubwa ya kuweka maslahi ya kibiashara mbele kuliko ya kiafya, kuna maazimio na taratibu maalumu zinazoelekeza juu ya biashara/masoko ya bidhaa mbadala wa maziwa ya mama (International Code of Marketing of Breastmilk Substitutes) yaliyotokana na kuona kwamba usalama wa maziwa hayo mbadala ni mdogo kwa afya ya watoto wetu.
NAMNA NZURI ZA KUONGEZA HAMASA YA WATU KUNYWA MAZIWA.
1. Elimu mashuleni: wanafunzi wakijua umuhimu watarudi nyumbani na kuwataarifu wazazi wao na pia wakiwa wakubwa wataitumia elimu ile kunywa maziwa na kuhamasisha wengine wanywe maziwa.
2. Kuondoa ubiashara kwenye suala la afya. Utakuta tangazo la kampuni ya maziwa likielezea maziwa wanayotengeneza wao ni bora kuliko mengine, hivyo mitazamo ya watu huwa maziwa fulani ndiyo mazuri kuliko mengine. Hii inapelekea mtu akienda dukani na kuyakosa yale maziwa aliyoaminishwa ni bora hanunui mengine.
3. Elimu kwa umma iongezeke kuliko matangazo ya biashara ya maziwa. Watu wajue faida za maziwa zaidi ili waweze kuyafuata mahali popote yanapopatikana maziwa yenye ubora. Bodi ya Maziwa ina kila sababu ya kuandaa kampeni ya utoaji elimu bila kusindikizana na makampuni ya maziwa ili watu wasione sura ya biashara nyuma ya elimu wanayopewa.
Ni vyema uelewe kwamba maziwa ni chakula bora kwa ajili ya afya zetu kama kitaandaliwa, kutunzwa na kitatumika ipasavyo. FasmoTz inakusihi msomaji wetu kutafuta na kuelewa taarifa sahihi zinazohusu maziwa kutoka katika vyanzo vinavyoaminika kama vile wataalamu wa mifugo, chakula, afya na lishe ili ufanyea yanayostahili.
Na
Innocent Sanga
Mtaalamu wa Lishe na Sayansi ya Mlaji
Fasmo Tanzania
#Lishe #Maziwa
Comments