KUKATAA MAARIFA NI UJINGA ULIOKOMAA

Naomba nianze kwa kucheka kidogo (haha ) kuna kauli nyingi sana zinazoumiza ukizisikia mtu akisema ila zinachekesha ukizitafakari. Bila shaka umewahi sikia kauli "Sikiliza wewe sisi ndio wataalamu....". Hiyo kauli ni moja ya kauli maarufu tu kwenye mitandao ya kijamii hapa nchini kwetu Tanzania. Nje ya hio kauli kuna kauli zingine kama..
●Utaniambia nini wewe?
●We mtoto wa juzi unajua nini?
●We wakuja utatueleza nini sisi wazawa?
●Mkubwa hakosei
●Nimeanza kuliona jua kabla yako huna chakuniambia sikijui
●Kwani yenye elimu mkubwa wamenipita nini mimi? 
 Siwezi zitaja kauli zote kwakuwa ni nyingi na kila siku zinakuja kwa mfumo tofauti ila zote zinakuwa zimejengeka katika kukataa maarifa mapya au maarifa mbadala kutoka kwenye taasis za kutoa elimu au kutoka kwa watu waliotuzunguka. 

 Tangu kuumbwa kwa dunia mpaka leo hii nje ya mapungufu au kasoro zingine za kila mwanadamu, binadamu hajatimia kimaarifa. Kuna maarifa kila mwanadamu anakuwa na uhaba nayo au hayajui. Ndio maana wahenga walisema ELIMU HAINA MWISHO yaani huwezi ukayamaliza maarifa yote ukawa nayo, kila siku utahitaji maarifa ili kuzidi kumudu maisha na kutawala mazingira yako.
 Kwa bahati mbaya sana kuna watu hujikuta wakikataa kupata maarifa mapya au maarifa mbadala tena kwa kauli za kejeli au kwa matendo tu. 
Unamkuta mtu hataki kushauri au kukosolewa na wazee au watu wanaomtakia mema kwa sababu mbalimbali zisizo na kichwa wala miguu. Eti mtu hapokei ushauri kwa mtu mdogo kiumri au aliye na kipato kidogo na wengine huenda mbali zaidi hawapokei ushauri kwa watu waliowapita elimu au hujui ndio mwanzo wa kauli za SIKILIZA WEWE SISI NDIO WATAALAMU. 
Kuna kiongozi mmoja hapa nchini kwetu alisema, "Haiwezekani mtu wa darasa la saba (from nowhere) aje kunikosoa mimi mtu na digrii zangu nne)". Huku kote ni kutotaka maarifa mbadala.

Kuna watu kwa ujinga na mazoea hujikuta hawataki kupokea ONYO, TAHADHARI na MIONGOZO ya vitu mbalimbali kwenye maisha. Tahadhari za kiafya ili kujiepusha na majongwa yanayoambukizika na hata yale yasiyoambukizika, mtu anakunywa tu pombe kupitiliza huku kashaambiwa pombe inaharibu utendaji kazi wa ini na figo na hata kupelekea kansa ila wapi? Mtu anabwia tena na tena. 
Tahadhari za ujio wa mvua kubwa watu wamefariki kutokana na kusomwa na maji na kukumbwa na mafuriko.

"Kaka nimeamua kuacha chuo naona chuo kinanichelewesha kufikia ndoto zangu...."
Hii ni moja ya sababu maarufu sana ya vijana wengi walioacha shule au vyuo. Wengine huenda mbali zaidi na kusema "Kwani hao wasomi wana maisha gani ya kutisha kiasi cha mimi kuamini hakuna maisha mazuri bila elimu??
Anaacha shule au chuo kwa sababu zisizo na mashiko kama hizo. Elimu au maarifa yatabaki na umuhimu bila kujali mwingine aliyapata na hakuyatumia. Uthamani wa elimu utabaki kuwa mkubwa siku zote. Kila kitu kinahitaji maarifa ili kifanyike vyema iwe kipaji, iwe biashara, kazi zisizo rasmi na zilizorasmi. Ni ujinga wa hali ya juu kukataa kujifunza kitu kipya chenye tija kwako.

Ukipata cheo au fedha usijiruhusu vikupofushe kiasi ukajiona wewe ndio wewe hakuna wa kukuambia kitu. Sikiliza mawazo ya watu ukikaza shingo itakatika.
Ukiwa na umri mkubwa au elimu kubwa usiache kutafuta maarifa. Wasikilize wadogo, jijenge katika kupokea vitu kutoka sehemu mbalimbali. Usiridhike kwa mengi unayoyajua.
Sikia mitazamo ya wengine, Usipuuzie.

Njia saba za kupata maarifa
●Kujisomea vitabu, magazeti, makala, Majarida na vitabu vya dini.
●Kuhudhuria semina, warsha mbalimbali
●Simulizi, maonyo, ushauri kutoka kwa wazee na watu waliotuzunguka
●Kutazama Video (YouTube, Dokumentari, na vipindi vya kuelimisha)
●Kutembelea maeneo/Sehemu mbalimbali za hapa duniani iwe mitaa,miji na hata sehemu za kihistoria utajua watu wanaishije, tamaduni zao nk
● Kudadisi na kutafiti mambo, ndani yake utapata maarifa.

AMKA TAFUTA MAARIFA
TUJIKINGE NA KORONA.

Comments

Popular posts from this blog

Mitindo Yetu Ya Ulaji.

Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.

MADHARA YA UTENGANO WA KIJAMII YALIYOSABABISHWA NA COVID19