COVID19 na Vitamini D
Habari za saa hizi mpendwa msomaji wa makala zetu!
Ni matumaini yetu unaendelea vizuri kiafya na upo wima katika mapambano dhidi ya Corona kwa kuchukuwa tahadhari zote muhimu kujilinda na kuwalinda waliokunzunguka msipate maambukizi. Leo tutaongelea juu ya Vitamini D dhidi ya Corona.
Hadi sasa kuna tafiti nyingi kuhusu ugonjwa huu wa Covid 19 zimefanyika na zinaendelea kufanyika na tafiti hizi hutofautiana hasa katika kuhusianisha ugonjwa huu na vitu kadha wa kadha. Ingawa CHAKULA (Lishe na Virutubishi) ni moja kati ya vitu ambavyo vimekuwa vikizungumziwa na kufanyiwa utafiti kwa kiasi kikubwa sehemu mbalimbali ulimwenguni tangu mlipuko wa ugonjwa huu uanze disemba 2019 huko China..
Hapa kwetu Tanzania kumekuwa na msisitizo mkubwa kutoka kwa wataalamu wa afya na lishe kuhusu ulaji wa Vyakula vyenye Vitamini C kwa wingi kama vile malimao, machungwa, tangawizi, mananasi, vitunguu swaumu, ndimu, mboga za majani kama vile giligilani, bila kusahau mapera (yaliyosahaulika na watu wengi kuwa yana vitamin C pia kwa wingi zaidi hata ya matunda yenye asili ya uchachu kama machungwa)
Hivi karibuni kuna utafiti uliohusisha ugonjwa wa Covid 19 na vitamini D (katika kuangalia kazi ya vitamini D katika kusaidia kupunguza dhoruba ya saitokini (cytokine storm) na vifo vihusianavyo na ugonjwa huu umechapishwa na katika utafiti huu imeonekana watu wengi wenye upungufu wa vitamini D mwilini wapo katika hatari kubwa zaidi ya kupata madhara yatokanayo na ugonjwa huu ikiwemo vifo.
Utafiti huu ulifanywa na watafiti kutoka chuo kikuu cha Northwestern na wengine kutoka kituo cha tiba cha Boston na ulitumia taarifa za watu wanaoandikishwa, wanaopona na vifo vinavyohusiana na covid 19 kutoka hospitali na kliniki mbalimbali katika nchi zilizo na visa vingi vya ugonjwa huu ambazo ni China, ufaransa, ujerumani, Italia, Iran, Korea ya kusini, Uhispania, Uswisi, Uingereza na Marekani (taarifa hizi ni zile zilizohifadhiwa hadi tarehe 20 Aprili 2020)
Katika utafiti huu wanasayansi hawa walitumia uhusiano uliopo kati ya vitamini D na aina ya protini inayotumika katika kinga ya mwili (Protini Tendaji C) ambayo huzalishwa na ini, na hutolewa pale ambapo mwili unakuwa na hitilafu ( uvimbe unaoambatana na wekundu na muwasho).
Kwa kifupi vitamini D ni moja kati ya vitamini kutoka kundi la vitamini zinazoyeyuka katika mafuta (pamoja na vitamini A, E na K)
Vitamini D hutokea katika namna mbili kulingana na chanzo chake, mimea (ambayo huitwa ergocalciferol-vitamini D2) au wanyama (cholecalciferol-vitamin D3).
Miale ya jua la asubuhi (UVB) husaidia mwili katika utengenezaji wa aina hii ya vitamini (katika fomu ya vitamini D3) kutumia malighafi (lehemu au cholesterol) zilizopo katika ngozi na hapa kazi ya miale ya jua ni kusaidia kutoa nishati inayotumika na seli za mwili kwenye ngozi kufanya kazi hiyo. Kuna tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa watu wengi ambao hujifunika mwili mzima kwa sababu mbalimbali au hukaa ndani kwa muda mrefu bila kupata mwanga wa jua huwa au wapo katika hatari ya kupata upungufu wa vitamini D (na hii ni kama watu hawa hawapati lishe bora)
Mfano wa vyanzo vingine vya vitamini hii ni kama nyama nyekundu, yai (kiini chake), samaki, aina flani za uyoga uliiota kwenye sehemu yenye miale mingi jua, maini.
Kazi kubwa ya vitamini hii ni kufanya kazi katika kusaidia matumizi ya madini ya kalisiamu mwilini kwa mfano , vitamini hii husaidia kuongeza ufyonzaji wa madini haya kutoka katika mfumo wa mmeng'enyo wa chakula na kupunguza upotevu wake kwenye figo (ili yasipotee kupitia mkojo). Pia Ikumbukwe kuwa madini ya kalsiamu yanatumika kutengeneza mifupa na sehemu zingine za mwili kama vile meno hivyo upungufu wa madini haya hupelekea mtu kuwa na mifupa laini.
Kuna tafiti zimethibitisha mchango wa vitamini D katika kusaidia mwili kupambana na baadhi ya magonjwa yatokanayo na virusi na bakteria wanaoshambulia mfumo wa upumuaji ambapo vitamini hii imeonekana kusaidia seli za ulinzi za mwili zilizoshambuliwa na bakteria aina ya Streptococcus pnemoniae. Pia kuna tafiti za kimaabara zinaonesha kuwa seli za epithilia katika mfumo wa upumuaji zina uwezo wa kubadilisha vitamini D kuwa katika hali inayoweza kutumika mwilini (Ikumbukwe kwamba mara nyingi vitamini D tunayoipata kwa njia ya chakula inakuwa katika hali ambayo haiwezi kutumika mwili hadi pale itakapo badilishwa kuwa katika namna inaweza kutumika, na haya yote hufanyika katika ini na figo)
Pamoja na tafiti hizi, hakuna uthibitisho wa moja kwa moja unaoelezea kuwa vitamini D inaweza kutumika kupunguza au kujikinga na Covid 19 ingawa kuna mwingiliano mkubwa unaoonesha kuwa watu wengi walio na hatari ya kupata Covid 19 na upungufu wa vitamini D ambapo tafiti zinaonesha ni watu wenye umri mkubwa, wenye magonjwa yasiyo ya kuambukizwa na watu wenye asili ya rangi nyeusi. Ndio mana hadi sasa halijatoka tamko linalohamasisha matumizi ya saplimenti za vitamini D katika mapambano dhidi ya virusi vya corona ila ni vyema kuendelea kupata lishe inayohusisha vitamini hii ili kupunguza aina ya utapiamlo itokanayo na upungufu wake.
Kwa sababu tafiti bado zinaendelea kufanyika hivyo tuendelee kusubiri wakati wowote tunaweza kusikia lolote...
Hivyo ni vyema kuendelea kupata lishe bora itokanayo na vyakula kutoka makundi makuu matano ili kujenga kinga imara ya mwili bila kusauhau kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Covid 19.
Lishe dhidi ya covid 19
Imeandaliwa kwa msaada mkubwa wa ripoti za tafiti mbalimbali zinazohusu magonjwa na lishe.
Na
Innocent Sanga
MwanaLishe
Fasmo Tanzania
0688301558
Comments