MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZIWA DUNIANI

Siku ya Maziwa Duniani huadhimishwa kila mwaka mnamo Juni 1. Siku hiyo ilianzishwa kwanza na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa ili kuonyesha umuhimu wa maziwa duniani. Imekuwa miaka 20 tangu maadhimisho yaasisiwe. Leo, ulimwengu mzima unasherehekea siku hii ili kuashiria umuhimu wa matumizi ya maziwa katika lishe yetu .
Kwa kutimiza miaka ishirini maadhimisho ya mwaka huu yamebeba ujumbe wa "MAADHIMISHO YA MIAKA 20 YA SIKU YA MAZIWA DUNIANI." 
Leo ni kilele cha wiki ya maziwa, tangu tarehe 26 Mei,, Jukwaa la Maziwa la Ulimwenguni na idara mbalimbali za maziwa za nchi nyingi duniani zimekuwa zikiadhimisha kwa kufanya mikutano na wadau na washiriki kuzungumza juu ya faida za maziwa na kuwatia moyo wengine kujumuika nao, pamoja na kuangazia shida za kupata maziwa na bidhaa za maziwa katika sehemu kadhaa za ulimwengu.

Unywaji wa maziwa nchini kwetu Tanzania bado upo chini. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) yampasa mtu mmoja kunywa lita 200 kwa mwaka. Tovuti za Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) Zinasema Mtanzania hunywa wastani wa lita 47 tu kwa mwaka ni kiwango kidogo kikilinganishwa na majirani zetu Kenya ambao kiwango chao ni lita 140. Watanzania wengi hatunywi maziwa ipasavyo kwasababu ya uelewa mdogo na hatuzijui faida za maziwa mwilini. Watu wanahisi maziwa ni kwa watoto wadogo, watu waliotoka kufanya kazi sehemu zenye vumbi sana au mtu aliyekunywa au kula sumu ndiyo anahitaji maziwa ili aitapike.
Siku ya maziwa duniani tunaitumia kuelimisha wananchi na umma matumizi ya maziwa kama chakula bora kwa watu wa rika zote na faida za maziwa katika kujenga afya ya binadamu. Umuhimu wa maziwa katika lishe na afya bora ya binadamu unatokana na:
● Kuwa na protini nyingi, bora na rahisi zaidi kwa ajili ya kujenga mwili
● Kuwa na vitamini A, B, na D kwa wingi kwa ajili ya kulinda mwili na kuimarisha mifupa, kuwa na ngozi nyororo na kuzuia upofu
●Kuwa na madini kwa wingi hasa ya calcium na phosphorus kwa ajili ya kujenga mifupa na meno imara
● Kuwa na wanga (lactose) kwa ajili ya kuupatia mwili nguvu na joto
● Kuwa na mafuta kwa ajili ya kuupatia mwili nguvu na joto
●Kuwa na maji yanayowezesha mwili kuyeyusha viinilishe ili viweze kutumika vizuri mwilini na
● Kuwa ni chakula kamili kinachojitegemea kwa kuwa na viinilishe vyote muhimu vinavyohitajika mwilini kwa pamoja.


Namna nzuri za kuongeza hamasa ya watu kunywa maziwa
●Kutoa elimu kwenye shule, wanafunzi wakijua umuhimu watarudi nyumbani na kuwataarifu wazazi wao na pia wakiwa wakubwa wataitumia elimu ile kunywa maziwa na kuhamasisha wengine wanywe maziwa.
●Makampuni kupunguza hali ya ubiashara. Utakuta tangazo la kampuni ya maziwa likielezea maziwa wanayotengeneza wao ni bora kuliko mengine, hivyo mitazamo ya watu huwa maziwa fulani ndiyo mazuri kuliko mengine. Hii inapelekea akienda dukani na kuyakosa yale maziwa aliyoaminishwa ni bora hanunui mengine hivyo kutokunywa maziwa.
●Elimu kwa umma iongezeke kuliko matangazo ya biashara ya maziwa. Watu wajue faida za maziwa zaidi ili waweze kununua hata kwa jirani. Hii itakuwa njia bora zaidi kuongeza hamasa ya watu kunywa maziwa. Bodi ya Maziwa ina kila sababu ya kuandaa kampeni ya utoaji elimu bila kusindikizana na makampuni ya maziwa ili watu wasione sura ya biashara nyuma ya elimu wanayopewa.

Maziwa ni lishe sio tu kinywaji. Kikombe kimoja cha maziwa kinaweza kikafanya mambo mengi ya kiafya na kilishe kwenye mwili wako. Hamasika kunywa maziwa, usisubiri kunywa siku unayojisikia. 

Na
Nobel Edson
Nutritionist & Consumer Scientist
Fasmo Tanzania
nobeledson95@gmail.com
0783961492

Comments

Popular posts from this blog

Mitindo Yetu Ya Ulaji.

Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.

MADHARA YA UTENGANO WA KIJAMII YALIYOSABABISHWA NA COVID19