Siku Ya Hedhi Salama

Tarehe 28 mwezi mei kila mwaka ni siku ya kuazimisha siku ya hedhi salama duniani (safe menstrual day)
Kwa kifupi tujikumbushe mambo machache kuhusu hedhi 

Hedhi ni kipindi ambacho wanawake waliokwisha balehe hupitia ambapo huambatana na kutokwa na damu, na kwa kawaida huwa mara moja kwa mwezi..Na hii hutokea kwa sababu mji wa mimba (yuterasi-uterus) unakuwa umeandaliwa tayari kwa kupokea na kulea mimba, maandalizi haya huusisha kuongezeka kwa unene wa misuli ya yuterasi na mishipa ya damu.
Pale ambapo mwanamke asiposhika mimba, ukuta wa mji wa mimba huachia au kudondoka (shading of uterus wall) na hii ndio hupelekea kutokwa na damu katika kipindi hiki ambacho kwa kawaida huchukua takribani siku 3 hadi 8, ingawa inaweza kutokea mwanamke kupata hedhi kwa muda zaidi ya siku nane kutokana na sababu mbalimbali.

Kwa wanawake wengi hedhi hutokea kwa namna ambayo wao huijua na wanaweza kujua ni siku gani katika mwezi huziona siku zao ( kwenda mwezini kama inavofahamika na watu wengi)

Kuna uchunguzi unasema, katika zile siku 3 hadi 8 za hedhi, siku mbili za mwanzo tangu kuanza kwa kutoka kwa damu ndio ambazo huwa na utokaji mkubwa wa damu. Na ikumbukwe kwamba kipindi hiki huambatana na maumivu makali na maumivu haya hutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine na hutokana na kuachilia kwa sehemu za misuli na mishipa ya damu iliyoongezeka katika ukuta wa mimba (uterus)

Kimsingi mwanamke anapofikia umri wa kubalehe (kuvunja ungo) hupatwa na mabadiliko makubwa kimwili na kiakili..kwa sababu huanza kupitia vipindi ambavyo tangia akiwa na miaka 0 hadi 10, 11 hajawai vipitia na hii huleta madhara ambayo yanahitaji msaada wa karibu sana ili kumuweka msichana (mwanamke) katika hali nzuri kimwili na kiakili.
Ndio maana upatikanaji wa taulo za kike (pedi) katika kipindi hiki ni muhimu sana. Hii ni kwasababu huwasaidia wanawake na kuwaweka katika hali ya usafi mahali popote watakapokuwa. Kwa mfano shuleni, njiani, ofisini, nyumbani, safarini nakadharika. Lakini, ni muhimu sana kukumbuka ya kuwa upatikanaji wa pedi haitoshi kuwasaidia wanawake hasa wale walio katika umri mdogo(hata wakubwa pia). 
Ijulikane kuwa katika kipindi cha hedhi kuna madhara yanayoathiri akili( saikolojia) ya mtu, ambayo msaada wa karibu zaidi huhitajika. Kipindi hiki pia huambatana na maumivu makali na shida mbalimbali. HIvyo basi ni muhimu kuwaeleza watoto wa kike kwa uwazi maswala ya hedhi, ili wakati ukifika waweze kuelewa kinachoendelea. Uwazi huo utawasaidia kupunguza aibu na kuongeza kujiamini kila siku. Msaada huu, unaweza kutolewa na walimu wao kwenye shule, wazazi wao na pia jamii kiujumla ina sehemu kubwa ya kuwasaidia wanawake (wasichana) katika swala hili.

Hedhi inahusiana na uzazi na katika swala hili kuna vitu vingi vinavyohusika mfano homoni, mabadiliko ya viungo vya uzazi ambavyo kiundani vimeelezewa katika sayansi ya baiolojia ya viumbe hai.
Baadhi ya shida zinazoambatana na hedhi
1.Kutokwa na damu nyingi isivyo kawaida
2. Maumivu makali ya tumbo
3. Kupata hedhi bila mpangilio (kuwa fupi zaidi au kuchukua siku nyingi zaidi) inayoweza kusababishwa na matatizo ya ulaji (eating disorders) na shida ya ufanyaji kazi wa tezi ya thairoidi (hyperthyroidism), ugonjwa wa PID-pelvic inflammatory disease, mawazo (stress)
4. Kupata hedhi isiyo ya kawaida mfano mwanamke kutokwa damu kipindi ambacho hayupo katika siku zake
5. Maumivu makali ya kichwa

Hizi ni baadhi tu ya shida zinazoambatana na hedhi ambapo hutofautina kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine na pia ni vyema kukumbuka kuwa visababishi vya shida hizi hutofautiana, hivyo basi ni vyema kufika kituo cha afya kwa uchunguzi zaidi kutambia sababu ya shida mtu anayopitia.

Hedhi na lishe
Katika kipindi hiki wanawake hupoteza kiwango kikubwa cha damu ambapo hii huwaweka katika hatari kubwa ya kupata upungufu wa damu mwilini.
Hivyo basi kutokana na upotevu huu wa damu wanawake wanahitaji aina fulani ya virutubushi ili kusaidia mwili kutengeneza damu iliyopotea.
*Madini ya chuma (ayani-iron) ni muhimu sana kwa wanawake katika kipindi hiki kwa sababu ni kirutubishi kinachohitajika katika kutengeneza damu na baadhi ya vyakula ambavyo ni vyanzo vizuri vya ayani ni nyama nyekundu, maziwa, spinachi, nyama za ogani kama ini, brokoli, jamii ya mikunde kama vile maharage, mdalasini, samaki..na pia ni muhimu kukumbuka kuwa ili mwili iweze kufyonza vizuri ayani itokanayo na mimea ni vizuri kuhusisha chakula chenye vitamini C kwa wingi katika mlo kama vile matunda ya aina mbalimbali"
Watu wengi huyadharau maharage na kuyaona si chakula bora ila ni chakula cha kimaskini bila kujua kuwa yana wingi wa madini haya muhimu katika kipindi hiki cha hedhi na pia ni chanzo bora kabisa cha protini mwilini..

Ikumbukwe pia ni muhimu kwa wanawake kupata lishe bora inayohusisha wingi wa virutubishi kama vile foliki asidi, kopa, vitamini B12, C, A kwani ni muhimu sana katika kipindi hiki cha hedhi bila kusahau virutubishi vingine kama vile kabohaidreti (nishati), protini na mafuta (nishati kwa wingi), madini mbalimbali kama vile kalisiamu ili kumjengea afya imara.
Katika maadhimisho ya mwaka huu, FASMO inaungana na watu wote ulimwenguni kusisitiza umuhimu wa hedhi salama kwa wanawake.Ni muhimu sana kuhakikisha wanawake wana uwezo wa kujiweka safi muda wote wa hedhi kupitia matumizi ya pedi bila kusahau msaada wa kisaikolojia hasaa kwa wasichana katika umri mdogo ili waweze kulikubali, kuwajengea kujiamini na kuchukulia kama ni suala la kawaida

Msichana Ondoa Aibu, Unastahili Hedhi Salama. Pedi ni kama Sukari, dawa ya meno, mafuta au bidhaa nyingine yeyote usione aibu kununua.

Siku ya hedhi salama na FASMO_TZ😁

Comments

Popular posts from this blog

Mitindo Yetu Ya Ulaji.

Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.

MADHARA YA UTENGANO WA KIJAMII YALIYOSABABISHWA NA COVID19