MAISHA YETU YA KILA SIKU NA UCHANGIA WA DAMU.
Juni 14 ni siku ya kuadhimisha kuchangia damu duniani.
Siku hii hutumika kuwashukuru watu wote wanaojitolea kuchangia damu na kuhamasisha wengine ili waweze kuanza kuchangia damu. Damu hutumika kusaidia kuokoa maisha ya watu wengi sana duniani kama vile, watu waliopata ajali, wanawake wanaojifungua na watu wenye magonjwa mbalimbali kama vile upungufu wa damu mwilini (anemia).
Kuchangia damu ni kitendo cha mtu kutoa damu yake ambapo huhifadhiwa katika mfuko maalum (blood bag) na kuwekwa katika joto kati ya nyuzi joto (°c) +2 hadi +6. Joto hilo ni sahihi katika kuhakikisha vitu vilivyomo ndani ya damu kama vile seli nyekundu, chembe sahani na vinginevyo haviharibiwi na damu haishambuliwi na vijidudu hatari kama vile bakteria na virusi.
Tujikumbushe vitu vichache kuhusu damu na kuchangia damu
Damu ni moja kati ya tishu katika miili ya wanyama (binadamu) ambayo hutumika kusafirisha virutubishi, takamwili, oksijeni, homoni na vitu vingine mwilini..Uwepo wa seli nyekundu za damu ambazo ndani yake huwa na protini inayoitwa haemoglobini ambayo imetengenezwa kwa (haem) yenye rangi nyekundu na hiyo ndio hupelekea damu kuwa na rangi nyekundu.
Mara nyingi tunaposema kitu fulani kama vile kirutubisho kimeingia ndani ya mwili basi maana yake kibaiolojia ni kwamba kirutubisho hiki kimeingia ndani ya seli..Kwa maana hii shughuli nyingi za mwili na karibia zote hufanyika ndani ya seli za mwili.
Damu imegawanyika katika makundi makuu manne kulingana na uwepo wa antibodi na antijeni.
Kwa kifupi tu antibodi ni aina fulani ya protini ambayo kwa asili ni sehemu ya kinga ya mwili WAKATI antijeni ni aina protini ambayo hupatikana katika seli nyekundu za damu (kwa tafsiri nyingine antijeni ni kitu chochote ambacho hutafsiriwa na seli za mwili kama kitu kigeni na hatarishi mwilini hivyo hushambuliwa na antibodi ili kuulinda mwili)
Makundi ya Damu
1. Kundi A - grupu hili huwa na Antijeni A kwenye seli nyekundu na Anti B antibodi katika utegili (plasma)
2. Kundi B - hili huwa na Antijeni B kwenye seli nyekundu na Anti A antibodi katika utegili
3. Kundi O - hili hawana antijeni lakini huwa na Anti A na Anti B antibodi katika utegili
4. Kundi AB - hili huwa na A na B antijeni ila hawana antibodi kwenye utegili wa damu.
Kundi O la damu ni moja kundi ambalo hutokea kwa watu wengi kwa mfano karibia nusu ya watu wa Uingereza sawa na asilimia 48 wanapo katika kundi hili la damu.
Kwa upande mwingine kuna mgawanyo wa makundi ya damu kulingana na uwepo wa aina fulani ya protini iitwayo Rhesus D Antijeni na kama protini hii ipo katika damu basi kundi la damu huitwa RhD chanya na kama hamna basi huitwa RhD hasi. Hivyo kulingana na mgawanyo huu, kuna makundi 8 ya damu ambayo ni:
1. A RhD chanya A+
2. A RhD hasi A-
3. B RhD chanya B+
4. B RhD hasi B-
5. O RhD chanya O+
6. O RhD hasi O-
7. AB RhD chanya AB+
8. AB RhD hasi AB-
Ikumbukwe kuwa mara nyingi grupu RhD O hasi (O-) hutumika kumuongezea damu mtu yoyote kwa usalama hasa pale ambapo kundi la mpokeaji halijulikani na imetokea dharura ya uhitaji wa damu. Damu hii ni salama kwa wapokeaji kwa sababu haina aina yoyote ya antijeni kama vile A, B, AB wala RhD katika seli zake na hivyo huendana na makundi yote ya damu.
Kuna madhara makubwa ya kupokea damu kutoka katika kundi lisilofaa kwa mfano kama mtu ana kundi B la damu akapewa damu ya kundi A kitakachotokea ni kwamba Anti A antibodi za mtu wa kundi B la damu zitashambulia seli za mtu wa kundi A, kwa maana hii ni kwamba haitakiwi mtu wa kundi A la damu kupewa damu ya mtu wa kundi B.
Ikumbukwe kwamba kwa sababu damu ya mtu wa kundi O haina antijeni A wala B inaweza kutumika kwa mtu wa kundi lolote kwa maana hiyo watu wa kundi hili huitwa yuniveso dona (universal blood donor) WAKATI kundi AB+ hupokea damu kutoka makundi yote kwa sababu damu yao haina antibodi hivyo watu hawa huitwa yuniveso risipienti (universal recepient).
Kabla mtu hajachangia damu ni lazima damu yake itapimwa kuangalia vitu kadhaa ikiwemo kundi lake la damu na maambukizi ya magonjwa mengine kama vile Ukimwi.
Inashauriwa mtu mwenye miaka kuanzia 18 na chini ya 60 ndiye mwenye uwezo wa kuchangia damu lakini pia kiasi cha haemoglobini katika damu kisiwe chini ya 12.5 gramu / desilita za damu. Pia mtu huyu awe na uzito usio pungua kilogramu 45.
Pia inashauriwa mtu kunywa maji ya kutosha kabla ya kuchangia damu bila kusahau kupata mlo kamili kabla na baada ya kuchangia damu ili kujiweka katika hali nzuri ya afya na lishe.
* Inashauriwa mtu kukaa angalau miezi mitatu baada ya kuchangia damu ili kusaidia mwili kurudisha kiasi cha haemoglobini kinachotakiwa*
BAADHI YA FAIDA ZA KUCHANGIA DAMU
1. Husaidia kutengenezwa kwa seli nyekundu za damu mpya.
Ndani ya masaa 48 baada ya kutoa damu, mwili huanza kuzalisha seli nyekundu za damu mpya.
2. Kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya moyo
Kuna baadhi ya tafiti zinasema pale kiasi cha madini ya chuma yanapoongezeka kwenye damu uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo huongezeka pia hivyo ni vyema kupunguza kiasi hicho kwa kuchangia damu.
3. Uwezekano wakupata vipimo vya afya na damu bure.
Hii ni kwa sababu kabla mtu hajachangia damu, ni lazima afya na damu yake vichunguzwe kujua shida yoyote hivyo kumuwezesha mtu kujua shida yoyote aliyo nayo.
Damu na Lishe
Baadhi ya vyakula ambayo husaidia utengenezaji bora wa damu ni vile vyenye madini (hasa madini ya chuma) na vitamini (kama vile vitamini B9) kwa wingi. Mfano wa vyakula hivi ni;
1. Mchai chai
2. Nyama nyekundu na nyama za ogani kama vile maini
3. Dagaa
4. Mayai
5. Mboga za majani
6. Jamii ya mikunde kama vile maharage
Ni vyema kuzingatia mlo kamili ili kuweza kujenga afya njema ili kurahisisha utengenezwaji mzuri wa damu mwilini.
Damu salama ni muhimu kwa sababu husaidia kuokoa maisha ya watu wengi kwa sababu uhitaji ni wa kila siku na wachangiaji ni wachache..Hivyo mimi na wewe ni jukumu letu kuhakikisha tunachangia damu ili kuokoa maisha ya watu hata tusiowajua kwa sababu unaweza kuta damu ya mtu usiyemjua inakuja kukusaidia wewe..
Baadhi ya Imani potofu kuhusu kuchangia damu.
1. Watu wasiokula nyama hawapaswi kuchangia damu
Kumekuwa na imani potofu kuhusu utoaji damu na kumefanywa utafiti kulibaini hili ikiwemo fikra kuhusu watu wasiokula nyama kuwa hawawezi kutoa damu.
Wasiwasi unatokana na kiwango cha madini ya chuma (kiini kikuu cha damu mwilini) na wasiwasi kwamba wasiokula nyama hawapati madini haya.
Lakini ni kwamba kama unakula lishe bora yenye virutubisho vizuri, basi bila shaka utapata madini ya chuma ya kutosha.
2. Watu wenye tatoo/michoro mwilini hawawezi kuchangia damu.
Unaweza kuchangia au kutoa damu hata kama una michoro ya tatoo au umetobolewa mwilini, tofauti na baadhi ya watu wanavyoamini.
Hatahivyo kuna sheria, lazima usubiri kwa miezi minne kutoka siku uliochorwa tatoo au kutobolewa mwilini kabla ya kuweza kutoa damu.
Na iwapo umetoa damu kwa kati ya miezi minne na mwaka mmoja baada ya kuchora tatoo au kujitoboa mwili, huenda ukafanyiwa ukaguzi wa ziada katika kituo cha kutoa damu.
Changia damu Okoa maisha na rudisha tabasamu usoni 😁
Ahsante kwa kuwa nasi. Karibu tena kwenye blog yetu.
Imeandaliwa na,
Innocent Sanga na Charles Msigwa.
Fasmo Tanzania.
Comments