MAZINGIRA NA DUNIA YETU
Mazingira ni wewe na mimi, mawe, miti, anga wanyama na kila kitu tunachokiona na tusichokiona kama vile vijidudu ambavyo vinaweza kuonekana kwa msaada wa vifaa maalumu vya maabara.
Mazingira ndio chanzo cha hali ya hewa, chakula, hewa tunayoivuta (oksijeni), maji tunayokunywa na vitu vingine kede kede vyenye manufaa kwetu..
Vitu vyote katika mazingira hutegemeana. Kwa namna kwamba viumbe hai hutegemea viumbe hai wengine na visivyo hai ili maisha yaende. Kwa namna hii kunakuwa na matumizi ya vitu katika mazingira kwa namna fulani ambayo inaweza ikawa inafaa au ikawa isiyofaa. Kwa mfano binadamu hutumia mimea (miti) kama kuni au kutengeneza mkaa kwa ajili ya nishati ya kutumia majumbani na sehemu zingine, lakini tumeshafika mahali ambapo matumizi ya miti kwa ajili ya shughuli kama hizi na nyingine nyingi yamepelekea kuharibika na kupotea kwa uoto asili na kupelekea madhara katika hali ya hewa, mfano kuongezeka kwa jotoridi na kupungua kwa kiasi cha mvua duniani..
Madhara haya yanachangiwa pia na shughuli zingine za binadamu zinazoathiri mazingira kama vile uzalishaji viwandani unaotoa taka hatarishi pamoja na shughuli za kilimo zisizozingatia utunzaji wa mazingira.
Ikumbukwe kwamba madhara yote haya katika mazingira yana athari kwa kila mtu kwa namna moja au nyingine, kwa mfano
1. Kupungua kwa mavuno ya mazao ya chakula kutokana na upungufu wa mvua, hii inaweza kupelekea kutokea kwa baa la njaa katika eneo fulani
2. Kuzuka kwa magonjwa yanayohusiana na kuongezeka kwa kiasi cha jotoridi
3. Kupungua au kupotea kwa wanyama pori na uoto asilia na hii itapunguza shughuli za utalii nchini hivyo kupelekea kupungua kwa pato la taifa.
Pia ni muhimu kukumbuka yakuwa mazingira yana uhusiano mkubwa na afya pamoja na lishe ya kila mtu.
Mazingira mabovu yanapelekea upatikanaji mgumu wa vyakula vizuri kiafya ( vitokanavyo na mimea na wanyama) kwa sababu hayataruhusu watu kujitengenezea bustani nzuri kwa ajili ya kulima mboga za majani, matunda pamoja na kufanya ufugaji wa wanyama ambao pia hutegemea mimea kwa ajili ya chakula chao.
Hivyo basi kama tulivyoona kwa kifupi ni kwamba kuna mzunguko unaopita kwenye mazingira hadi kwa binadamu ambao nao ni sehemu ya mazingira katika kuruhusu mzunguko wa virutubishi kutoka katika kundi moja hadi lingine ni vyema tukatunza mazingira na kuyatumia kwa busara.
Tunza mazingira ili yakutunze
"Celebrate biodiversity" but do not forget to diverisfy your plate....smile😁
sherehekea bianuwai ila usisahau kumeremetesha sahani yako kwa kula chakula kinachozingatia makundi yote matano.
Tutabasamu kwa shairi la kimazingira
Jumla ya vyote,
Vilivyotuzunguka,
Tuvilinde sote,
Lasivyo tutaumbuka,
Tukiharibu chochote,
Sura zitatushuka,
Nzuri kuyatazama,
Hakika yanapendeza,
Wababa kwa Wamama,
Leo nawapongeza,
Hamstahili lawama,
Mazingira mewekeza.
Yatupa nishati,
Maligafi na maji,
Twayahitaji kwa dhati,
Kukidhi yetu mahitaji,
Tumepata kibahati,
Tuyatunze bila ubabaishaji.
Mungu aliumba misitu,
Na mali nyingi asili,
Ila kuna mibaya mijitu,
Yavitumia bila akili,
Yatumia moto na vitu,
Kuharibu uoto na mali.
Kwaheri na karibu tena kwenye makala zetu mbalimbali
Na
Innocent Sanga
Fasmo Tanzania
Comments