MTOTO WA AFRIKA
Mwaka1991, wakuu wa nchi wanachama wa OAU walianzisha Siku ya Mtoto wa Afrika (DAC) kama kumbukumbu ya uasi dhidi ya wanafunzi 16 Juni 1976 huko Soweto, Afrika Kusini. Wakati huo, wanafunzi watoto wadogo waliandamana, mosi kupinga aina ya elimu duni ya kibaguzi waliyopewa na serikali ya kibeberu, pili waliitaka serikali ya mzungu iwape ruksa kufundishwa kwa lugha zao wenyewe. Siku ya Mtoto wa Afrika hutumika kuwakumbusha watoto wetu hatua ya kijasiri waliyoichukua wenzao huko Afrika Kusini katika kulinda haki zao. Watoto wanakumbushwa kwamba wanaweza kuleta mabadiliko hata wakiwa wadogo
Katika kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika ni vyema kukumbuka mambo kadhaa ili kufanikisha kuijenga Afrika imara kupitia watoto;
1. Tuishi na watoto kama marafiki zetu
Katika maisha ya kila siku ni vyema kuishi na watoto kama marafiki zetu wa karibu sana bila kusahau majukumu yetu kama wazazi au walezi wao. Upande mzuri wa kufanya hivi ni kuongeza ukaribu na watoto ambao kwa tamaduni za kiAfrika huwa ni mdogo na hii hupelekea watoto kuishi kwa kujitenga na wazazi, walezi na hata watu wakubwa kwao wakiwemo dada na kaka zao. Kuna vitu vingi ambavyo watoto hupitia ambavyo huhitaji msaada wa mawazo au namna nyingine. Kwa mfano kipindi watoto wanapovunja ungo hupata mabadiliko kimwili na kiakili hivyo huhitaji msaada kutoka kwa watu wakubwa kwao ili waweze kukabiliana na changamoto zitokanazo na mabadiliko hayo.
Watoto wengi hujikuta katika matatizo makubwa na moja ya sababu ni kwamba hawapati muongozo wa aina yoyote kutoka kwa wazazi au watu waliowazidi umri. Kiukweli mimba nyingi za watoto zinasababishwa na watoto wa kike kutoelewa maswala ya hedhi zao pamoja na mahusiano na hii ni kwa sababu watoto huwa hawapati muda wala nafasi ya kuongea na wazazi wao kwa undani ili wawe na uelewa unaotakiwa
Endapo kutakuwa na mahusiano rafiki kati ya watoto na wazazi au kaka/dada zao unaohusisha maongezi chanya kati yao kuhusu maswala kama haya kuna uwezekano mkubwa wa kusaidia kupunguza mimba za utotoni zinazokatisha mwelekeo wa elimu kwa watoto wa kike wengi wa mijini na vijijini.
Hivyo ni jukumu letu sote kujenga urafiki chanya na watoto kwa jinsia zote na kwa usawa.
2. Tusaidie watoto wetu wapate ujuzi na maarifa yenye manufaa.
Ni muhimu kuhakikisha watoto wetu wanapata elimu kwa sababu hakuna kitu kibaya kama ujinga. Watoto wapewe elimu itakayo wawezesha kukabiliana na changamoto katika jamii wanazoishi..
Hii ina maana ni muhimu kwa wazazi wa kizazi hiki kuhakikisha wanabadili mitazamo yao kuhusu kuwasaidia watoto kupata ujuzi watakaoweza kuutumia kuwasaidia katika maisha ya kila siku. Kwa mfano kama baba au mama wanajihusisha na shughuli fulani kwa ajili ya kujipatia kipato, ni vyema kuwahusisha watoto katika shughuli hizo ili nao waweze kuwa na kitu cha ziada katika maisha yao zaidi ya shule ambayo huchukua muda mwingi wa maisha yao. Kama nyumbani kuna gari, baiskeli au pikipiki ni vizuri watoto wote wapewe nafasi ya kujifunza kuvitumia vyombo hivi kwa sababu mbali na kuwa na manufaa kwa watoto hawa, inaweza kuwa msaada wa kuvitumia vyombo hivi pale inapohitajika..
Ni bora kuwekeza kwa watoto katika fani zinazoweza kuwasaidia maishani haraka kama vile ufundi wa vitu mbalimbali (uselemala, mekaniki, umeme, ujenzi), kilimo, upishi kwa sababu hizi ni huduma ambazo watu huzitumia kila siku hivyo zitawasaidia watoto kupata kipato na hata shughuli ya kufanya kwa kujiajiri wao wenyewe.
3. Elimu ya teknolojia na matumizi mazuri ya mitandao.
Siku ya Mtoto wa Afrika ni zao la watoto kudai haki zao kadhaa haswa haki ya kupata elimu inayoendana na mazingira yao. Mazingira ya sasa yametawaliwa na teknolojia na shughuli nyingi zinazohitaji mitandao. Kusoma kupitia mitandao, biashara kwa kutumia mitandao na shughuli zingine nyingi hutumia teknolojia na mitandao.
Ni vyema sasa wazazi wawaongoze watoto katika ulimwengu wa teknolojia na mitandao. Kuwaunganisha watoto na waalimu wazuri, kuwafundisha watoto matumizi sahihi ya mitandao. Watoto wana haki ya kupewa mwongozo wa matumizi ya mitandao hiyo. Kuna faida nyingi za teknolojia na mitandao kwa watu wote, watoto wasiachwe nyuma. Madhara yanayoweza kuwapata watoto kwa kutumia mitandao yanaweza kudhibitika tusiishie kuyabeba na kuwakataza watoto wasitumie mitandao kabisa.
Mtoto wa mwenzio ni wako. Afrika ni yetu!
Na
Innocent Sanga
Fasmo Tanzania.
Comments