RUSHWA YA NGONO KATIKA MAPANA YAKE.

RUSHWA YA NGONO KATIKA MAPANA YAKE.

Rushwa ya ngono ni moja ya rushwa maarufu na ya kawaida kuombwa na hata kutolewa katika jamii zetu. Aina hii ya rushwa ina mizizi sana kwenye taasisi mbalimbali hususani maeneo ya kazi, biashara na vyuoni.

Rushwa ni kitu chochote kinachoombwa au kinachotolewa visivyohalali ili mtu apate kitu fulani ambacho kinaweza kuwa haki yake au sio haki yake. Kuna aina na mitindo mbalimbali ya rushwa katika jamii za maisha ya mwanadamu.

Kati ya hizo aina mbalimbali, rushwa ya ngono ni moja wapo. Kama zilivyo rushwa zingine kutolewa katika uficho, rushwa ya ngono hufanyika katika usiri mkubwa sana baina ya hao watu wawili. Waathirika wakubwa wa hii rushwa ni wanawake.


Inakuwaje?
Kuna mazingira mbalimbali yanayopelekea rushwa ya ngono kuombwa na kutolewa. Kwa mfano rushwa ya ngono vyuoni ina sura kama tatu.. 
1. Kuna ile hali binti yupo vizuri kimasomo ila mhadhiri anamuwekea mizengwe na kutishia kumfelisha asipolala nae.

2. Kuna ile hali binti hayuko vizuri kimasomo ila mhadhiri anamuahidi kumfaulisha endapo atalala nae au atamfelisha zaidi (Discontinue) akikataa takwa la kulala nae.

3. Kuna ile hali binti hapendi kusoma au hajitumi darasani au somo kwake ni gumu sana hivyo hujilegeza kwa mhadhiri ili afaulishwe.

Hayo ni kwa uchache mazingira yanayosababisha rushwa ya ngono vyuoni. 
Lakini rushwa ya ngono pia ipo sana kwenye sekta ya ajira. Mtu anaombwa rushwa ya ngono ili apitishwe kwenye udahili wa kazi (job interview), ili apatiwe kazi au nafasi fulani na wengine wanaombwa rushwa ya ngono ili wapandishwe vyeo au hata kupata uhamisho kazini.

Siku hizi limekuwa jambo la kawaida sana kwenye vijiwe na mitandao ya kijamii kiongozi wa kike akiwa anashutumiwa basi rushwa ya ngono hutajwa kama chanzo cha yeye kupata hiyo nafasi. Shutuma hizi sio zote kweli ila zinaakisi kwamba rushwa ya ngono imekuwa kawaida kwenye ofisi nyingi ndiyo maana watu wanaona kawaida kumshutumu yeyote.


Kwanini haisemwi?
Ni kawaida kukuta rushwa zingine zikipigwa vita sana lakini rushwa ya ngono haiongelewi kwa viwango ambavyo sauti itasikika na suluhu kupatikana.
Wanawake ambao ni waathirika wakubwa wa hii rushwa nao hawaiongelei. Kwa nini hawaiongele wakati wao ndio wanaumizwa zaidi? Huenda wanawake wenye vyeo vikubwa wamefika pale juu bila bughudha za kuombwa hiyo rushwa hivyo kuona rushwa ya ngono sio tatizo au huenda walitoa hiyo rushwa na sasa wamekosa ujasiri wa kuikemea kwa kuwa ndio njia walioitumia wao kufika walipo. 

Kwa wanaume wao hawaiongelei rushwa ya ngono huenda kwa sababu wananufaika nayo, huenda kwa sababu hawaombwi hiyo rushwa au huenda ni ileile hulka ya wanaume kwamba hivyo ni vitu binafsi vya watu (personal issue) hivyo hawana kawaida ya kuongelea mambo binafsi ya watu.

Yote kwa yote nje ya sababu zingine zote zinazochangia rushwa ya ngono kutoongelewa kwenye jamii sababu nyingine kuu ni ustaarabu wa kijinga wa Kiafrika wa kuogopa na kujizuia kuongelea mambo ya kijinsia na manyanyaso ya kingono kwa kisingizio cha utamaduni hauruhusu na kuliona ni jambo la faragha.


Nini kinapelekea?
Rushwa ya ngono inasababishwa sana na mifumo iliyowekwa ya uendeshwaji wa mambo. Mifumo inapokuwa dhaifu husababisha watu kutumia udhaifu huo kutekeleza tabia zao mbaya na aina mbalimbali ya uovu. Kwa mfano rushwa ya ngono ipo sana kwenye taasisi ambazo MAAMUZI HUFANYA NA MTU MMOJA NA SIO JOPO LA WATU. Hii utaiona kwenye makampuni ambapo mtu mwenye nguvu, kwa mfano nguvu ya kuajiri mfanyakazi hushutumiwa kutumia uwezo huo kuomba rushwa.

Pia huko vyuoni ambapo mhadhiri ndiyo anashikilia hatma ya mwanafunzi. Yeye ndiyo anamfundisha, yeye ndiye anatunga mtihani na kusahihisha na yeye ndiye anatoa maksi zinazoruhusu mtu kuendelea miaka ya mbele au kufeli kurudi nyumbani. Kwa uwezo huu wa kushikilia hatma ya mtu kielimu basi ni rahisi tabia yake mbaya ikachipuka na ndio hapo rushwa ya ngono, rushwa ya hela na zingine hutokea. 
Mwanafunzi asipofanya vizuri darasani rushwa ya ngono inaweza ikachipuka na hii ndiyo sababu vyuoni kumekithiri kwa rushwa ya ngono. Lakini mfumo ungekuwa kuna Baraza la mitihani la vyuo kama ilivyo NECTA au namna yeyote ambayo hatma ya mwanafunzi haishikiliwi na mhadhiri mmoja rushwa ya ngono isingekuwa kubwa.

Maadili
Kumomonyoka kwa maadili hakuwezi kuepuka kuwepo kama sababu ya rushwa ya ngono kushamiri. Sio rushwa ya ngono tu bali unyanyasaji wa aina mbalimbali wa kijinsia kama ubakaji, ulawiti na kadharika.

Matukio kutoripotiwa.
Idadi ya kesi zilizopo Takukuru au mahakamani zinazohusu rushwa ya ngono ni chache mno ukilinganisha na idadi ya kesi zinazongelewa mitaani. Endapo kesi zingekuwa nyingi mahakamani na hatua kali kuchukuliwa naimani matukio ya rushwa ya ngono yangepungua sana tu kutokana pande zote wasingeaminiana kila mmoja angeona mwenzake anaweza kumchoma kwa Takukuru muda wowote.

Watu kutojiweka katika nafasi nzuri.
Watu wanataka vitu kwa wepesi. Kwa mfano mwanafunzi hasomi sana chuoni akifeli anajikuta anatoa rushwa ya ngono. Endapo angesoma sana na kukataa kutoa rushwa, hata kama akifelishwa na mhadhiri ni rahisi kupinga matokeo na yeye kusaidika kutokana kiuhalali kafaulu.


Vipi Takukuru?
Taasisi ya Kuzuia na Kupanmbana na Rushwa inajitahidi kwa sehemu yake. Tukisema Takukuru hawafanyi kazi ya kutosha juu ya aina hii ya rushwa tutakuwa tunawaonea. Rushwa ya ngono hufanywa kwa usiri zaidi kiasi ni ngumu kwa taasisi kuingilia kati endapo mtendwa hatotoa taarifa. Lakini tutawashutumu Takukuru endapo wahanga watapeleka ripoti ofisini kwao lakini zisishughulikiwe au mhadhiri akawapa rushwa maofisa wa Takukuru ili asishughulikiwe kama ule msemo wa "Anti corruption institutes are corrupted" Taasisi za kupinga rushwa zinanuka rushwa..


Kwa nini visa vya rushwa ya ngono haviripotiwi sana?
Kesi na matukio ya rushwa ya ngono hayaripotiwi sana hususani na wale wanaoombwa kwa sababu kadha wa kadha. 
1. Uoga : Kumekuwa na uoga wa kuripoti matukio ya rushwa ya ngono kwa sababu ya hisia kwamba ni jambo la aibu au ni jambo binafsi. Pia uoga kutokana na hofu ya maisha baada ya kuripoti. Kumekuwa na visa kadhaa wale wanaoripoti kuombwa rushwa ya ngono na wahadhiri kutomaliza vyuo. Hujikuta wananyoshewa vidole na wahadhiri wengine kwamba wanakichafua chuo hivyo husakamwa kiasi cha kushindwa kumaliza masomo yao.

2. Kuchukulia poa au kawaida
Hii sababu inawakumba wengi wahanga wa kuombwa hii rushwa. Hawachukulii kama jinai na kuripoti bali huona ni kama katongozwa tu kwahiyo anahiari ya kukubali na kukataa. Na jibu lake lolote halipaswi kujulikana kwa watu, labda kwa rafiki zake wa karibu sana. Hii husababisha visa vingi kutoripotiwa.

3. Hakuna kipya kitakachotokea
Muhanga anahisi hata hakiripoti hakuwa suluhu inayoeleweka itakayofanyika zaidi atakuwa kajitangaza (exposing and self risking). Unakuta mtu anamifano kichwani mwake kuwa kuna visa viliripotiwa na hakuna hatua zilizochukuliwa. Hivyo huona bora abaki kimya apambane pekeyake.


Mapendekezo
1. Kupunguza mfumo wa mtu mmoja kushikiria hatma ya mtu. Kuna ugumu huu mfumo kuondolewa kabisa kwa sababu kuna vitu unakuta kuna mtaalamu mmoja pekee chuo au hata Tanzania nzima na yeye ndiyo mwomba rushwa. Kwenye mifumo mingine ikiwezekana maamuzi yafanye na wengi ili kupunguza mianya ya rushwa ya aina yeyote.

2. Takukuru kufungua ofisi kwenye vyuo. Hii itasaidia angalau kujenga hofu katika maeneo ya vyuo na pia kusaidia matukio kuripotiwa kwa haraka ili upelezi na hatua zingine zichukuliwe ndani ya muda mfupi.

3. Mwanamke kujiweka katika sehemu salama. Kujiamnini na kutumia nafasi yake. Kama mwanafunzi asome sana ili mazingira ya rushwa yakitokea aweze kusaidika haraka na kwa wepesi ili apate haki yake ya kielimu. Pia kujua haki zake na malengo ya muda mrefu ya maisha. Asiruhusu tamaa imuendeshe.

4. Mtoa taarifa kunufaika zaidi kuliko kuathirika.. 
Hii ndiyo njia bora kabisa ya kupambana na rushwa ya ngono. Mtoa taarifa asione kwamba anapoteza kitu pale anaporipoti. Mtoa taarifa afaidike aone kuna msaada wa kudumu nikiripoti na sio akisharipoti maisha yake yawe hatarini au hatma yake isieleweke. Hii itasaidia waomba rushwa ya ngono kuripotiwa kwa wepesi hivyo kupungua kwa matukio na hata kuisha. 

5. Elimu ya jinsia na uelewa juu ya haya mambo. 
Mtu ajue rushwa ya ngono ikoje.. aweze kutofautisha rushwa ya ngono na kutongozwa, ajue namna gani za kukusanya na kutunza ushahidi na namna za kumripoti mwomba rushwa wa ngono.

6. Kuzibana hotel... lodge... guest houses. Kuhamasisha nyumba hizo za wageni ambazo hutumika sana kutendeka kwa rushwa hiyo zinakuwa na mifumo mizuri ya kutunza taarifa za wateja wao. Kama majina kamili, muda wa kuingia na maelezo mengine ili kusaidia upelelezi wa Takukuru pale itakapohitajika. Na endapo nyumba hizo zitazembea katika hilo zipigwe faini au kufunguliwa mashitaka.

7. Ushirikiano
Mtu akiona dalili za kutakwa rushwa aseme. Asisubiri mambo kumfika shingoni ndio afungue mdomo na kusema. Unakuta mdada wa chuo baada ya kufeli (kufelishwa) ndiyo anasema "Profesa alinitaka nikamkatalia, kaamua kunifelisha kunikomoa".Paza sauti haraka iwezekanavyo ili kusaidika.

Kwa kuhitimsha Family Smile Organization kama wadau wa maendeleo ya jamii na ustawi wa mtu mmoja mmoja tunawasihi watu wote tuungane kupaza sauti kukemea, kulaani na kushirikishana mbinu mbalimbali za kupambana na rushwa ya ngono. Ubaya wa rushwa ngono ni inaathiri utu wa mtu na kidini ni dhambi mbili (dhambi ya rushwa na dhambi ya uzinzi). Kwa kuwa hii rushwa ipo miongoni mwetu basi tunaweza kuishinda tukiongeza ushirikiano kati yetu.

Na
Nobel Esson Sichaleh
Fasmo Tanzania 
Consumer Scientist.
0783961492
Mwanajamii.

Comments

Anonymous said…
Hili suala pana sana

Popular posts from this blog

Mitindo Yetu Ya Ulaji.

Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.

MADHARA YA UTENGANO WA KIJAMII YALIYOSABABISHWA NA COVID19