SIKU YA SICKLE CELL DUNIANI
Tarehe 19 juni ni siku inayotambulika na Umoja Wa Mataifa kama siku ya selimundu duniani ambayo lengo lake ni kuhamasisha watu kitaifa na kimatataifa kutambua uwepo wa aina hii ya ugonjwa unaotokana na mapungufu ya kijenetiki. Umoja Wa Mataifa unatambua ugonjwa huu kama moja ya magonjwa ya kijenetiki unaowakumba sana watu na ni tatizo kubwa linaloathiri watu wengi katika jamii zetu.
Kwa kawaida seli nyekundu za damu huwa na muonekano wa duara unaoziruhusu kufanya shughuli zake kiurahisi na kwa ufanisi mwilini.
Selimundu (sickle cell disorders) huhusisha magonjwa yote ambayo huathiri seli nyekundu za damu na kuzifanya kuwa na muonekano wa mundu 🌙 (muonekano wa kikwakwa kama cha kukatia nyasi) na ugonjwa huu ni wa kurithi kwa maana kwamba mtu huupata kutoka kwa wazazi wake na hauwezi kuambukizwa kutoka kwa watu wengine tofauti na wazazi wa mtu husika.
Tafiti zinaonesha Tanzania ni moja kati ya nchi duniani ambazo kuna watoto wengi huzaliwa na magonjwa ya selimundu. Inakadiriwa watoto 11000 wenye magonjwa haya huzaliwa kwa mwaka.
Katika magonjwa haya ya selimundu, protini iitwayo haemoglobini katika seli nyekundu za damu ndiyo huathiriwa na kwa watu walio na magonjwa haya huwa na aina hii ya protini iitwayo 'haemoglobini S' ambayo ndio husababisha seli nyekundu kuwa na umbo kama mundu au siko.
Aina za magonjwa ya selimundu
1. Siko seli anemia
2. Ugonjwa wa Siko haemoglobini C
3. Ugonjwa wa siko beta plasi (plus) Thalassemia
4. Ugonjwa wa siko haemoglobini D
Kila ugonjwa hapo juu una jenetiki tofauti jinsi unavyotokea na kumuathiri mtu. Lakini muda mwingine kuna muingiliano wa dalili zinazoonekana katika aina tofauti za magonjwa kwa watu tofauti.
Kazi ya seli nyekundu za damu mwilini ni kusafirisha hewa (oksijeni) kutoka kwenye mapafu kupeleka sehemu zingine za mwili na kuchukua kabonidayoksaidi kuipeleka kwenye mapafu ili itolewe nje ya mwili.
Seli nyekundu za damu zinapokuwa na umbile kama siko/mundu hupelekea kushindwa kufanya kazi yake kwa ufanisi unaotakiwa hivyo kushindwa kupita vizuri katika mishipa ya damu kwa maana kwamba hata ubebaji na usafirishaji wa hewa mwilini hupungua au huwa hafifu.
Madhara ya upungufu wa hewa katika sehemu mbalimbali za mwili ni maumivu makali ambayo hutokana na kuziba kwa mishipa ya damu kwa sababu seli hizi zenye umbo la siko haziwezi kupita vizuri katika mishipa hiyo hivyo husababisha kuziba kwake.
Dalili za magonjwa ya selimundu.
*Ni vema kukumbuka kwamba dalili za ugonjwa huu huanza kuonekana kwa mtu tangia anapokuwa mtoto na ni kama:
1. Kuwa na kiasi kidogo(namba ndogo) ya seli nyekundu za damu (anemia)
Hii hutokea kwa sababu seli nyekundu zenye umbo la siko hufa mapema.
*Ni vema kukumbuka pia kila seli nyekundu ya damu huishi kwa muda wa siku 120 sawa na miezi minne, baada ya hapo huaribiwa na malighafi zinazobaki hutumika kutengeneza seli nyekundu mpya*
2. Kupata kwa haraka na wepesi maambuzi ya magonjwa mara kwa mara.
3. Kupata maumivu makali kwa vipindi.
4. Kuchoka sana na mara kwa mara, kuwa na uchovu na kukosa nguvu.
5. Homa ya manjano
Hii huonekana kwa manjano katika sehemu nyeupe za macho na kwenye ngozi na hutokana na kufa mapema kwa seli nyekundu za damu.
*Ni vema kukumbuka kuwa dalili za magonjwa haya hutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine*
Madhara yatokanayo na selimundu
Kutokana na kwamba seli nyekundu huwa na umbo kama siko na kupelekea kuziba kwa mishipa midogo ya damu, maana yake ni kwamba damu yenye oksijeni haitazifikia sehemu zenye uhitaji mwilini na hii hupelekea sehemu hizi kukosa hewa kwa ajili ya shughuli zake hivyo husababisha kufa kwa seli katika ogani mbalimbali za mwili kama vile mapafu, figo, ubongo na wengu (spleen), na hivyo kupelekea kufa taratibu kwa ogani hizi na mwishowe kushindwa kufanya kazi.
Mtu mwenye selimundu huwa na hatari ya kupata;
1. Kiharusi (hutokana na kuziba kwa mishipa ya damu kwenye ubongo)
2. Upofu
3. Mifupa kuharibika
4. Kuharibika kwa viungo vya mwili kama vile figo, ubongo, mapafu
5. Msukumo mkubwa wa damu katika mishipa inayoenda kwenye mapafu (pulmonary hypertension) na hii hutokea kwa karibia 1/3 - theruthi moja ya watu wazima wenye magonjwa ya selimundu. Hii hupelekea moyo kushindwa kufanya kazi.
6. Kuchelewa kwa kukua na maendeleo ya watoto wadogo.
7. Kifo kutokana na madhara yanayoambatana na magonjwa haya
Selimundu na lishe
Kuna baadhi ya tafiti zinaonesha yakuwa watu wazima na watoto wadogo wenye selimundu huwa na upungufu wa nishati lishe mwilini. Hivyo kuna tafiti zinapendekeza watu wenye magonjwa haya kuendelea kupata lishe bora inayohusiha vyakula vinavyotoa nishati kwa wingi (wanga, mafuta na protini)
Ni vema kuzingatia ulaji wa aina za mafuta zinazofaa ambazo ni zile zitokanazo na mimea kama vile;
1. Alizeti
2. Karanga
3. Mahindi
Lakini pia ni muhimu watu hawa hasa watoto wakapata vyakula vyenye protini kwa wingi ili kuwasiadia katika ukuaji na maendeleo ya kimwili kama vile;
1. Jamii ya mikunde (maharage na njegere)
2. Samaki
3. Nyama na nyama za ogani kama vile maini na figo
4. Maziwa
5. Soya
Lakini pia protini huhitajika kwa ajili ya kuimarisha sehu mbalimbali za mwili hasa misuli
Virutubishi vingine ambavyo huhitajika kwa watu hawa ni pamoja na vitamini za aina mbalimbali mfano;
1. Vitamini D kwa ajili ya matumizi ya kalisiamu mwilini hasa kwenye mifupa
2. Vitamini A ili kuboresha afya ya macho - karoti, mapapai, viazi lishe (rangi ya njano), mrehani mbichi
3. Vitamini B9, B12, C, E
Madini na vyanzo vyake;
1. Madini ya chuma (ayani)- mdalasini, maharage, nyama nyekundu, mchaichai
2. Kalsiumu - maziwa, dagaa, nyama, mboga za majani
3. Zinki - korosho, maharage, nyama nyekundu, nyama ya kuku
4. Magniziamu - maharage, mboga za majani zenye rangi ya kijani iliyokolea, nafaka ambazo hazijakobolewa
Bila kusahau kunywa maji ya kutosha kila siku.
*Ni vema kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya katika kupunguza madhara ya magonjwa haya ambayo hayana dawa ya kuyatibu kabisa yakaisha*
Selimundu ipo ila madhara yake yanaweza kupunguzwa. Kwa pamoja mimi na wewe tusaidie kusambaza ufahamu juu ya magonjwa haya ili watu wajue jinsi ya kuyakabili...
Fasmo_tz inaungana wa watu wote duniani kuongeza uelewa kuhusu selimundu. Tuwasaidie watu wote wenye selimundu ili wafurahie maisha na waishi wakiwa na tabasamu tele..
Na
Innocent Sanga
Mwanalishe
Fasmo Tanzania
Comments