SIKU YA WATU WENYE UALBINO DUNIANI.

Siku ya watu wenye ualbino duniani
Ualbino ni hali ambayo husababishwa na kurithi jeni (genes) kutoka kwa wazazi wote wawili ambapo mtoto hukosa melanini (rangi ya asili-pigmentation). Rangi ya asili hukosekana katika macho, ngozi, nywele na kupelekea kuwa na uoni hafifu na kuwa katika hatari ya kupata saratani ya ngozi. Ikumbukwe kwamba wazazi wote wanaweza wasiwe na ualbino lakini kama walibeba jeni za ualbino, hii ndio hupelekea wao kupata mtoto mwenye ualbino kwa maana kwamba wao walibeba tu zile jeni ila hazikuoneshwa katika maumbile.
Barani Afrika Tafiti zinaonesha kuwa idadi ya watu wanaoathirika na ualbino ni kubwa kusini mwa jangwa la sahara ambapo kwa Tanzania inakadiliwa mtu 1 kati ya 1400 ana ualbino, kwa utafiti uliofanyika nchini zimbabwe ulionesha mtu mmoja kati ya 1000 ana ualbino.

Ni vyema kukumbuka pia ualbino hutokea kwa viumbe wengine kama vile mbwa, simba, tembo, taiga na wanyama wengine wengi.
Baadhi ya changamoto ambazo watu wenye ualbino hukumbana nazo ni kama
1. Kuwa katika hatari kubwa ya kupata saratani ya ngozi na hii hutokana na kukosa melanini ambayo husaidia kukinga ngozi na miale mikali ya jua.
Katika baadhi ya nchi watu wenye ualbino hufa katika umri kati ya miaka 30 hadi 40 kutokana na saratani ya ngozi

2. Kukumbwa na uoni hafifu na sababu ni ile ile ukosefu wa melanini machoni
3. Kukumbwa na ubaguzi katika jamii kutokana na kuwa na rangi ya mwili isiyo ya kawaida (nyeupe kupitiliza)- kama stori ya Takadini moja ya riwaya zilizoandikwa katika mazingira ya Kiafrika zinavyoangaza maisha ya watu wenye ualbino katika bara la Afrika.

4.  Ushirikina dhidi yao. Kupata majeraha kutokana na kuumizwa au kukatwa viungo vya mwili sababu ya imani potofu hasa barani Afrika (mfano Tanzania).

5. Kukosa huduma za afya ikiwemo kupata nyenzo zinazoweza kuwakinga na miale mikali ya jua kama vile miwani na mavazi haswa sehemu za kichwani na maangalizo ya afya mara kwa mara (health check up)
Aina ya unyanyapaa wanaoupata watu wenye albinizim hutofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine ambapo kwa upande wa Afrika huhusisha vitu kama kutengwa katika jamii kuanzia familia yake hadi mtu mwenyewe aliye na ualbino na mbali na vyote hivyo mauaji au kukatwa viungo vya mwili.

Sehemu zingine kama vile Amerika, ulaya na Asia huhusisha kuwaita majina mabaya watu hawa (bullying) na hata kuwatenga.

Katika jamii zote tabia hizi zote hutokea haswa kwenye shule na sehemu za michezo ingawa hata katika maeneo ya majumbani tabia hizi huonekana.

Vitu vyote hivi huonekana kwa sababu ya ujinga na imani potofu ambazo zimekuwa zikihama kutoka kizazi kimoja hadi kingine ndio maana hatuoni ukomo wa tabia hizi..Ila ni vyema kutambua ya kuwa jukumu letu, mimi na wewe kusaidia kuondoa uonevu unaotokana na ujinga wa watu wachache katika jamii zetu.
Ni muhimu kutambua kuwa ualbino ni mapungufu tu ya kijenetiki mwilini na hivyo itambulike kuwa mtu mwenye ualbino ana nafasi kama mtu wa rangi ya kawaida. Na pia ni vyema kutambua ya kuwa watu wenye ualbino wana uwezo mkubwa tu wa kufanikisha mambo kadha wa kadha katika jamii. Mfano Tanzania kuna watumishi wengi wa serikali na taasisi binafsi ambao ni albino. Pia tuna Haji Manala ambaye anawakilisha vyema moja ya klabu kubwa nchini.
Katika kuadhimisha siku ya ualbino duniani Fasmo Tanzania inapenda kuhamasisha jamii kuwajali watu wote wenye ualbino, kuwalinda na kuwapenda bila kusahau kujenga jamii inayolenga kuweka tabasamu katika sura zao. Huu ni muda wa kusherehekea tofauti zetu.

"Made to shine"
Nang'ara

Usisahau kuweka tabasamu.

Na
Innocent Sanga
Fasmo Tanzania.

Comments

Popular posts from this blog

Mitindo Yetu Ya Ulaji.

Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.

MADHARA YA UTENGANO WA KIJAMII YALIYOSABABISHWA NA COVID19