DHANA ZA MAHUSIANO KATI YA MZAZI NA MTOTO KATIKA MALEZI.

Tangu zamani kumekuwa na dhana na fikra mbalimbali katika jamii juu ya ukaribu wa mzazi na mtoto katika malezi na makuzi. Fikra na dhana hizi bado zipo kwenye jamii zetu kati ya familia na familia.
Wapo wanaoamini mzazi hapaswi kuwa na urafiki na mtoto. Mzazi akiwa na urafiki na mtoto kuna mfanya mtoto awe kiburi na dharau kwa watu wengine kwa kuwa anajua mzazi ni rafiki yake atamtetea. Na muda mwingine urafiki huo hujenga mazoea kisha mtoto huwa na dharau kwa mzazi husika "Mazoea huleta dharau". 
Dhana hii ni kubwa na maarufu sana kwenye familia nyingi za Kiafrika. Baba awe Baba na sio rafiki wa mtoto, baba inabidi aogopwe na kuheshimiwa sana na mtoto na sio mtoto akimuona baba aanze kumchezeachezea. Ni hii dhana ambayo wazazi wetu wengi wamekulia na imejenga nidhamu kubwa kati yao kwa kuwa kuna mstari mwekundu ulikolezwa (Red bold line) kati ya mtoto na mzazi. 
Pia kundi lingine linabeba dhana ya MZAZI LAZIMA UWE RAFIKI MKUBWA WA MWANAO. Kundi hili linaamini mtoto anahitaji upendo na ukaribu wa dhati ya mzazi. Mtoto anahitaji kusikilizwa. Dhana hii imejengeka katika misingi ya umuhimu wa mawasiliano baina ya mzazi na mtoto.  Watoto nao wanapitia mambo kadhaa maishani hivyo lazima kuwepo kwa urahisi wa wao kuwaeleza wazazi wao mambo wanayohitaji na wanayopitia. Kufanikisha urahisi huo ndipo kunapatikana hitaji la urafiki kati yao. Mzazi inabidi amjenge mwanae awe huru kumsemesha na wasiishie tu kwenye salamu "Shikamoo Baba.... Marhaba... Hujambo... Sijambo!" Pekee. 
Kwa kuzielezea hizo dhana mbili za malezi ni vyema tutazame URAFIKI ni nini au RAFIKI ni nani?

Kuna tafsiri nyingi za neno urafiki. Kati ya tafsiri zote zilizopo kwa pamoja zinaelezea 
●Ukaribu wenye mawasiliano mazuri. Ukaribu pekee hautoshi kuwa urafiki, kwa kuwa hata adui yako ni mtu wa karibu. Lakini ukaribu wenye mawasiliano mazuri yasio na unafiki. Mawasiliano hayo kama kujuliana hali, kuwaziana mema, kushaurina vitu, kushirikishana taarifa na vitu mbalimbali. Kwa tafsiri hii ndiyo utakuta kati ya ndugu zako kuna ndugu mnaukaribu lakini sio rafiki yako na kuna mtu ni ndugu na ni rafiki. Vivyo hivyo kwa jirani, kuna mwingine ni jirani tu (ukaribu wa nyumba) lakini mwingine ni jirani na ni rafiki. Kwa tafsiri hii pia kuna mzazi kama mzazi na kuna mzazi pia ni rafiki ambapo tunazipata dhana zetu mbili.

●Ushirikiano na Mwingiliano chanya. Hii ni tafsiri ya urafiki haswa kwa jamii au nchi. Urafiki wa kimakundi au kijamii. Urafiki wa Tanzania na Uchina. 

 ●Mazoea yaliyopo. Hii hutafsiri urafiki wa mtu na vitu au wanyama. Mzee Munisi ana urafiki na ng'ombe huyu. Johnson ana urafiki na sigara au pombe. 

Turudi kwenye mada yetu ya dhana hizo mbili za malezi na makuzi ya mtoto katika mahusiano na mzazi. Kwa tafsiri hizo za urafiki tutatumia tafsiri ya kwanza inayoelezea ukaribu na mawasiliano chanya.
Mara nyingi sana mzazi na mtoto huwa karibu. Ukaribu wa kuishi nyumba moja, ukaribu wa kimahusiano "Mtu na mwanaye" na ukaribu wa kiuwajibikaji yaani kutimiza majukumu kama mzazi kwa mtoto. Ukaribu huu hauepukiki na hautafsiri kwamba mzazi na mwanaye ni marafiki. 
Uwepo wa huo ukaribu bado mzazi anaweza akachora mstari au hata kujenga ukuta baina yake na mtoto. Ndiyo pale unakuta baba akirudi nyumbani watoto wanaondoka sebuleni au wanaanza kujishughulisha na vikazi ambavyo havipo. Mzazi anataka akiita mara moja tu mtoto awe amesikia na amekuja haraka na asipoitika kesi nyingine hiyo ndiyo utasikia ile misemo "Unahesabu sauti?" Changamoto huwa kubwa kwani rafiki mkubwa wa mtoto wa kumwelezea yanayomsibu sio mzazi anaweza akawa ndugu mwingine au mtu asiye mwanafamilia (mtu baki).

Faida za Dhana hii ya mzazi kutokuwa na urafiki na mtoto
●Heshima kwa mzazi inakuwa kubwa kwa kuwa hakuna nafasi ya mazoea yanayoweza leta dharau.
●Ni rahisi kwa mzazi kumjenga mtoto kinidhamu. Nidhamu ya muda, nidhamu ya matumizi na nidhamu kwa wakubwa. Kwa kuwa mtoto anajua akifanya ndivyo sivyo ni adhabu bila utetezi. Hivyo hujikuta anafanya kwa bidii na utii vitu vingi.
●Ni rahisi kwa mtoto kujiongoza kwa kuwa anakabidhiwa sheria za kufuata.

Changamoto ya dhana hii malezi.
●Inambana sana mtoto kufurahia malezi hususani uhuru wa kujieleza kwa mzazi. Hivyo mtoto hujikuta anamengi sana ndani mwake na hana wa kumwambia kwa kuwa mzazi hajamjengea uhuru huo.
●Upendo kwa mzazi unakuwa wa mashaka. Mtoto akilelewa sana katika hali hii hujikuta anawathamini watu baki. Watu wale waliompa sikio au kimsaidia na mzazi anabaki kuheshimika kama mzazi ila sio kama msaada kwake.
●Nidhamu ya uoga. Mtoto anaweza akajengeka katika misingi ya kinafiki kwa kuwa malezi yalimfanya yeye kutanya vitu hata kama moyoni havikubali na akithubutu kukataa ni adhabu.
●Mtoto anaweza akaja kuwa mwenye tabia za ubabe na kuonea watu wengine. Aina hii ya malezi inaweza kumfanya mtoto kuhisi maisha inabidi yaende hivi. Hivyo akiwa na wenzake anawapigapiga bila sababu au yeye anataka akiongea mara moja wamsikilize, wasipomsikiliza anakiwasha. Jamii nyingi zenye malezi namna hii hata viongozi wa kijamii huwa na hulka za kidkteta kwa kuwa hawapendi maneno akiongea kaongea.
Dhana ya Urafiki kati ya Mzazi na Mtoto
Kwa ile tafsiri ya kwanza ya urafiki, uwepo wa ukaribu na mawasiliano chanya kati ya mzazi na mtoto. Ukaribu wa kifamilia, na mawasiliano mazuri baina yao ni muhimu sana katika malezi. Mtoto akiwa rafiki kwa mzazi anakuwa huru kuelezea hali ya masomo yake, hali ya afya, kwamba baba najikisia kichwa kinauma na akaeleweka wakati usipokuwepo urafiki mtoto anahisi baba atahisi nasingizia ili nisiende shule au nisifanye kazi fulani.
 Pia mzazi na mtoto wanajiwekea mazingira mazuri ya kushauriana. Kwa mfano mtoto anashida katika somo la hesabu na kamwambia mzazi watashuriana namna nzuri na kukubalina inaweza mzazi akajitolea kumfundisha, akamnunulia vitabu au akampelekea tuition  au hata kama kwenye mashauriano yao ikaonekana mwalimu wa shuleni hayuko vizuri mzazi akamwamisha mtoto shule. Ila yote haya ni zao la mawasiliano mazuri na mtoto. 
Pia urafiki kati yao ni msingi wa kushikishana vitu mbalimbali vya kiroho kwa mfano mtoto kaota ndoto fulani ni rahisi kumwambia mzazi rafiki ila mzazi asipokuwa rafiki hiyo ndoto atabaki nayo au atamwambia kiongozi wa dini au mtu baki. 
Kushirikishana hali ya uchumi,mzazi kumwelezea mtoto mapito ya kiuchumi ili kumuweka sawa kisaikolojia kipindi hicjo. Kuna watoto wengi wa mtaani wapo mtaani kama machokoraa kwa kuwa walitumwa dukani wakapoteza hela njiani na wanajua wazazi wao hawana urafiki kabisa wakirudi nyumbani kipigo kizito sana hivyo wakatorokea mtaani na kuishi kama hawana wazazi. 
 Ni hii hali ya urafiki inaweza ikaboresha vitu vingi kwenye familia kama lishe, afya, uchumi na mahusiano kwa kuwa inashirikishs wazazi na watoto.
Faida za hii dhana ya urafiki kati ya mzazi na mtoto
●Kujengeka kwa upendo na kuthaminia baina ya mzazi na mtoto.
●Mtoto anajengeka katika misingi ya mawasiliano na maelewano. Hivyo ndivyo ataona inapendeza kuishi na watu wengine.
●Mtoto anajengeka kifkra. Mtoto anakuwa mtu wa kufikiria kwa mapana mambo ili anapokuwa anawasiliana na mzazi wake awe na ushawishi asiwe mjinga.
●Mtoto anakuwa muwazi sana kwenye mambo yake kwa kuwa anajua atasaidika katika gumu analopitia kimawazo au kimali.

Changamoto za hii dhana
●Ni rahisi mtoto kuwa na mazoea hivyo kujikuta anawadharau wazazi na watu wengine. Baba ataelewa.... Mama hawezi nifanya lolote....
●Inaweza mfanya mzazi kumwamini sana mtoto kiasi cha kumtetea au kumdekeza sana.

Malezi ya mtoto 
Kwa dhana zote hizo mbili, dhana ya mtoto kuwa rafiki ina faida nyingi na inajenga misingi ya mawasiliano baina ya watu. Japo watu wanailaumu sana dhana ya urafiki kati ya mzazi na mtoto kwamba ni moja ya sababu ya watoto kuharibika kimaadili kwa sababu wazazi wanatetea tabia za watoto. Lakini kiukweli kama urafiki wa mzazi na mtoto utasababisha mtoto kuwa na tabia mbaya basi tatizo sio urafiki tatizo ni tabia zao. Nionyeshe rafiki yako nitakuambia tabia zako. 
Ni vyema wazazi wajenge urafiki na watoto wao ila wasisahau usimamizi na majukumu yao kama wazazi.



Na
Nobel Edson Sichaleh
Fasmo Tanzania
Parenting 
0783961492

Comments

Popular posts from this blog

Mitindo Yetu Ya Ulaji.

Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.

MADHARA YA UTENGANO WA KIJAMII YALIYOSABABISHWA NA COVID19