FAIDA ZA MAZIWA YA MAMA KWA MTOTO
FAIDA ZA MAZIWA YA MAMA KWA MTOTO
Maziwa ya matiti ni maziwa yanayotolewa na mama ili kumnyonyesha mwanawe. Maziwa hayo hutoa chanzo msingi cha lishe kwa watoto kabla ya wao kupata uwezo wa kula vyakula vingine, yaani watoto wachanga hadi umri kadri wanavyoweza kuendelea kunyonyeshwa.
Kunyonyesha ni tendo la kumpa mtoto maziwa kutoka katika titi la mama moja kwa moja au kumnywesha mtoto maziwa ya mama yakikamuliwa kwa kutumia kikombe. Maziwa ya mama ndiyo chakula bora kwa mtoto mchanga kuliko maziwa wengine au chakula kingine.
Shirika la Afya duniani (WHO) linapendekeza mtoto kunyonyesha maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza ya maisha, vyakula vizito huanzishwa mnamo umri huu unapoongezeka, hatua kwa hatua wakati ishara ya utayari huonekana, kunyonyesha huendelea kupendekezwa kama nyongeza mpaka angalau miaka miwili, au kwa muda mrefu jinsi mama na mtoto watakavyotaka. Maziwa ya mama ni chakula na kinywaji cha kwanza, na cha pekee kwa mtoto tangu anapozaliwa mpaka kufikia umri wa miezi sita.
Uzalishaji
Wanawake huweza kutoa maziwa baada ya kujifungua chini ya ushawishi wa homoni za prolaktini na okistosini. Maziwa ya kwanza kutolewa hujulikana kama kolostramu, ambayo huwa na kiwango cha juu cha imunoglobulini IgA ambayo huzingira njia ya utumbo. Hii husaidia kulinda mtoto mchanga mpaka mfumo wa kinga yake unafanya kazi vizuri, na inajenga athari ya kupumzika, huondoa mekoniamu na kusaidia kuzuia kujengwa upya kwa bilirubini (sababu muhimu ambayo huchangia ugonjwa wa macho kugeuka manjano).
Kiasi cha maziwa kinachotolewa hutegemea ni mara ngapi mama hunyonyesha na/au kusukuma maziwa, mama anayenyonyesha mtoto wake zaidi au kukamua, ndivyo anavyotoa maziwa zaidi. Ni jambo la manufaa kunyonyesha kwa mahitaji- nyonyesha wakati mtoto anataka badala ya kufuata ratiba.
Muundo
Ufuatao ni muundo wa maziwa ya mama ikiwa ni mjumuisho wa virutubisho tofauti kama inanyoonyesha na viwango vyake husika. Muundo huu umejumuisha mafuta, protini, kabohaidreti na madini.
Baadhi ya ukweli muhimu kuhusu unyonyeshaji
Watoto walionyonyeshwa kwa kawaida huwa na afya bora zaidi, hukua na kuwa na maendeleo mazuri ikilinganishwa na wale wanaolishwa maziwa yasiyo ya mama. Kama watoto wengi zaidi wangenyonyeshwa maziwa ya mama pekee yake bila ya kitu kigine chochote laini au kigumu, hata maji inakadiliwa kwamba maisha ya kiasi cha watoto 800,000 wa umri chini ya miaka mitani yangeweza kuokolewa kila mwaka.
Kama watoto wataendelea kunyonyeshwa hadi miaka miwili na zaidi, afya na maendeleo yao hua bora zaidi.
Watoto wachanga ambao hawanyonyeshwi maziwa ya mama wapo katika hatari zaidi ya kupata magonjwa au kupoteza maisha kwa magonjwa. Watoto wanaonyonyeshwa hupata kinga ya magonjwa kutoka kwa maziwa ya mama.
Kunyonyesha ni njia ya asili na inayohimizwa ya kulisha watoto wachanga, hata kama kuna vyakula vingine vya watoto, maji safi, pamoja na mazingira mazuri na salama.
Faida za maziwa ya mama kwa mtoto
Faida kwa mtoto katika na baada ya kipindi cha utoto.
●Kupunguzwa kwa dari hatari ya kifo cha ghafla kwa watoto (SIDS).
●Inapunguza uwezekano wa kupata baadhi ya saratani kama vile saratani ya damu kwa watoto (leukemia).
●Hupunguza uwezekano wa kuambikizwa ugonjwa wa katikati mwa sikio, homa na viini vinavyoleta homa.
●Humpatia virutubisho (viini lishe) vyote anavyohitaji kwa uwiano ulio sahihi kwa ukuaji na maendeleo yake. Watoto walionyonya maziwa ya mama huwa na mwenendo mzuri pamoja na akili ukilinganisha na wale wasionyonya maziwa ya mama.
●Maziwa ya mama humeng’enywa (huyeyushwa) kwa urahisi tumboni mwa mtoto na hivyo kutumiwa kwa urahisitumboni mwa mtoto na hivyo kutumiwa na mwili kwa ufanisi.
●Hayaleti mzio (allergies) kwa mtoto kama vile pumu.
●Hupunguza hatari ya mwanzo wa ugonjwa wa kisukari wa mtoto
●Hupunguza matatizo ya meno
●Hupunguza hatari ya fetma baadaye katika maisha
●Hupunguza uwezekano wa kupata matatizo ya kisaikolojia
●Humpatia kinga dhidi ya maradhi mbalimbali kama kuharisha, magonjwa ya njia ya hewa na masikio.
●Humwezesha mtoto kukua kimwili na kwa ukamilifu.
●Huleta uhusiano mzuri na wa karibu kati ya mama na mtoto.
Faida kwa mama
●Hupunguza uwezekano wa kupata saratani ya mfuko wa uzazi, na matiti.
●Husaidia kupunguza uzito au kumrudisha katika umbile lake la kawaida endapo alipata ongezeko kubwa la uzito kipindi cha ujauzito.
●Husaidia kulinda afya ya mama kwa kusaidia kurudi katika hali ya kawaida mapema baada ya kujifungua.
●Pia hupunguza damu kutoka hivyo kuzuia upungufu wa wekundu wa damu (Anaemia).
●Hupunguza uwezekano wa mama kupata ujauzito mwingine hasa ndani ya miezi sita ya mwanzo na kipindi chote cha unyonyeshaji, ikiwa atanyonyesha mara nyingi kwa siku kwa kuwa hatopata hedhi.
●Maziwa ya mama ni safi na salama na hayahitaji matayarisho kama maziwa mbadala.
●Maziwa ya mama hupatikana muda wote katika joto sahihi.
●Hayabadiliki ndani ya titi na hata yakikamuliwa hukaa saa 8 katika joto la kawaida na saa 72 katika jokofu bila ya kuharibika.
●Hujenga na kuimarisha uhusiano wa karibu kati ya mama na mwanae.
●Mama anaponyonyesha mara baada ya kujifungua husaidia tumbo la uzazi kurudi katika hali yake ya kawaida mapema.
●Gharama yake ni ndogo (lishe bora kwa mama) tofauti na maziwa mbadala.
●Maziwa ya mama huokoa fedha na muda wa familia.
●Hutunza mazingira kwani hayaachi makopo au chupa kama maziwa mbadala.
Ni muhimu
~Mtoto aanze kunyonya ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa.
~Mtoto anyonyeshwe maziwa ya mama ya mwanzo yenye rangi ya njano (colostrumu).
~Mtoto anyonyeshwe kila wakati usiku na mchana.
~Mtoto aendelee kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila hata maji katika miezi sita ya mwanzo.
~Endapo mama ana maabukizi ya VVU, aanze (kama hajaanza bado) au aendelee kutumia dawa za kupunguza makali ya ukimwi na amnyonyeshe mtoto wake maziwa ya mama pekee kwa miezi 6, harafu amwanzishie vyakula vya kulikiza na kuendelea kumnyonyesha hadi atakapotimiza umri wa miaka miwili au zaidi.
Kumbuka
>Maziwa ya mama yana maji na virutubisho vyote anavyohitaji mtoto katika miezi 6 ya mwanzo kwa afya na ukuaji bora.
>Mama anaweza kukamua maziwa yake na mtoto kulishwa wakati mama anapikuwa mbali na mtoto wake.
Na
Neema Robert
MwanaLishe
Fasmo Tanzania
Comments