MAADHIMISHO YA SIKU YA MOYO DUNIANI

Siku ya moyo duniani huadhimishwa tarehe 29 mwezi septemba kila mwaka. Shirikisho la moyo duniani ndio chimbuko la siku hii muhimu yenye lengo la kusaidia jamii kujua madhara ya magonjwa ya mfumo wa mzunguko wa damu ambapo zaidi ya nusu ya vifo vyote vitokanavyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza duniani husababishwa na magonjwa haya. 

Hapo awali siku ya moyo duniani ilikuwa ikiadhimishwa jumapili ya mwisho ya mwezi wa tisa na kwa mara ya kwanza iliadhimishwa tarehe 24 septemba 2000.
Magonjwa ya mzunguko wa damu husababisha takribani vifo vya watu milioni 17.9 dunia nzima na vifo hivi haswa huhusisha magonjwa ya moyo na kiharusi (stroke). Hii huchangia takribani asilimia 31 ya vifo vyote duniani.

Moyo ni ogani ifanyayo kazi kama pampu inayosukuma damu kupitia mirija katika mwili wa binadamu na hivyo husaidia katika kusafirisha na kuzungusha virutubishi na hewa za oksijeni, kabonidayoksaidi pamoja na vitu vingine vingi. Moyo huanza kufanya kazi kuanzia siku ya 22 tangia kutunga kwa mimba na huendelea kufanya kazi hadi pale uhai wa mtu unapofikia mwisho.. Ufanyaji kazi wa moyo huendelea hata pale ambapo utakuwa upo nje ya mwili wa binadamu kwani mapigo yake huzalishwa na umeme utokanao na moyo wenyewe bila kutegemea umeme kutoka kwenye ubongo wa mtu.

Ukubwa wa moyo wa mtu hulingana na ule wa ngumi ya mkono wake. Watu wengi husema moyo unapatikana sehemu ya kushoto ya kifua, ingawa ukweli ni kwamba sehemu kubwa ya ncha yake imeelekezwa zaidi upande wa kushoto, ndio maana watu husema moyo hupatikana upande huu.
Mfano wa magonjwa ya moyo
1. Magonjwa yanayoathiri mishipa ya damu ya moyo

2. Magonjwa yanayoathiri misuli ya moyo

3. Magonjwa ya valvu za moyo

4. Magonjwa ya moyo ya kuzaliwa

Visababishi vya magonjwa ya moyo
Kiujumla mtindo wa maisha usiofaa ndiyo sababu kubwa ya magonjwa haya, ikiwemo;
1. Matumizi ya tumbaku yaliyokithiri
2. Kutofanya mazoezi ya mwili
3. Matumizi ya pombe yaliyopitiliza
4. Ulaji wa chakula usiofaa (vyakula vyenye sukari, chumvi, mafuta kwa wingi)

Matokeo ya visababishi tajwa hapo juu ambavyo hupelekea magonjwa ya moyo ni kama;
1. Kuongezeka kwa shinikizo la damu (pressure)
2. Kuongezeka kwa kiwango cha sukari kwenye damu
3. Kuwa na uzito uliozidi au uliokithiri

Dalili za magonjwa ya moyo
Mara nyingi dalili za magonjwa haya huonekana pale ambapo tayari mtu ameshapata athari kubwa, yaani sehemu husika imeshapata madhara makubwa. Baadhi ya dalili hizo ni;
1. Mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida ( mfano; moyo kudunda haraka sana)
2. Maumivu ya kifua hasa yanayotembea mpaka kwenye mabega, shingo au taya
3. Kukosa pumzi au kushindwa kupumua vizuri hasa unapolala chali
4. Miguu, uso na tumbo kuvimba na kujaa maji

Kupambana na magonjwa ya moyo
1. Zingatia mlo bora 
*Punguza ulaji wa nyama nyekundu na vyakula vyenye sukari, chumvi na mafuta kwa wingi
*Ongeza ulaji wa mbogamboga, matunda, jamii ya mikunde na tumia nafaka zisizokobolewa

2. Mazoezi ya mwili
Ni vyema kufanya mazoezi ya mwili kila siku kama vile kutembea, kukimbia, kuruka kamba, kuendesha baiskeli na mengineyo kwa angalau dakika 30. Au kufanya hivyo angalau mara 3 kwa wiki nzima
3. Kuepuka matumizi ya pombe na sigara

4. Kuepuka msongo wa mawazo au mkazo (stress) na kutafuta njia mbadala za kukabiliana nayo kama vile kuwaona wataalamu wa afya ya akili

5. KUHAKIKISHA UNAPIMA AFYA YA MOYO MARA KWA MARA KATIKA VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA ZA AFYA.

Moyo ndio msingi wa afya, linda kila pigo la moyo wako..

💝💝💝💝💝


Kwa msaada wa mtandao

Nna 
Innocent Sanga
Fasmo Tanzania

Comments

Popular posts from this blog

Mitindo Yetu Ya Ulaji.

Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.

MADHARA YA UTENGANO WA KIJAMII YALIYOSABABISHWA NA COVID19