HAKI ZA AFYA YA UZAZI NA JINSIA
HAKI ZA BINADAMU
Haki za binadamu ni haki zinazohusiana na mambo ya msingi na asili ya uhuru na heshima ya ubinadamu ambapo watu wote wamepewa haki ya kupata heshima kama binadamu. Mara mtu azaliwapo mume au mke hupata haki hizi. Haki hizi zinatambuliwa kimataifa na zina usawa kwa watu wote. Nchi mbalimbali zimetia sahini na kuidhinisha haki hizi za kimataifa na kufanya ni sehemu ya sheria zao pamoja na kuweka sera zinazolinda haki hizi.
HAKI ZA UZAZI
Haki za uzazi ni haki zinazomwezesha mwanamke na mwanaume, mwajiriwa kutimiza majukumu yake ya uzazi na kufanya kazi bila kubaguliwa, kubugudhiwa au kupoteza ajira. Likizo ya uzazi ikiwa ni moja ya haki za uzazi, humpa mama na baba muda kutoa matunzo muhimu kwa mtoto katika siku/miezi ya mwanzo ya maisha yake, ikiwa ni pamoja na kumnyonyesha. Vilevile likizo ya uzazi humpa mama mwajiriwa muda wa kupumzika na hivyo kusaidia mwili wake kurudi katika afya na hali ya kawaida baada ya kujifungua.
Haki za uzazi zina misingi yake katika haki za binadamu na pia zinahusiana na haki za mtu mmoja mmoja.
Kupata habari juu ya ujinsia na mada zinazohusu afya ya uzazi.
Vijana balehe wote wana haki ya kupata habari juu ya mambo yote yanayohusu afya ya uzazi. Watoto wanavyokuwa, wanapitia mabadiliko ya kimwili, hisia na ya kisaikolojia katika maisha yao. Watu wazima, hasa wale wanaowasimamia watoto wanapaswa kuwapa habari juu ya mabadiliko na jinsi yanavyoshawishi ukuaji wa kimwili na hisia. Hii ni muhimu ifanyike muda wote na katika kila rika.
Iwapo vijana hawapati habari za kutosha juu ya mabadiliko ya miili yao wanaweza kuingizwa katika matatizo ya kimaisha, ya kijinsia na mimba zisizotarajiwa au magonjwa yatokanayo na kujamiiana pamoja na Virusi vya UKIMWI.
Kwa hiyo wasichana na wavulana wanahitaji kupata elimu ya ujinsia wanapokuwa vijana wadogo. Hii ni pamoja na habari ya jinsi ya kujilinda wenyewe. Siyo kweli kwamba elimu ya ujinsia inahimiza vijana wajamiiane. Kinyume chake, wale vijana waliopata habari sahihi wanakuwa na mwelekeo mzuri na wana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi.
Mwanamke au mwanaume kuamua kwa uhuru na kuwajibika, kama unataka kujamiaana lini na nani.
Kuna aina nyingi za unyanyasaji wa kijinsia na unaweza kutokea kwa wote wanaume na wanawake. Kwa kawaida unajulikana kama matumizi ya makusudi ya kutumia nguvu na uwezo na kutishia au kwa hali halisi kinyume cha mtu au kikundi au jamii ambapo matokeo yake yanaweza kuleta jeraha au kifo, kuumia kisaikilojia. Mwanamke au mwanaume mwenye umri sahihi kisheria ana uhuru wakuchagua kama anataka kujamiana bila kulazimishwa na mwingine
Kuamua kwa hiari na kuwajibika juu ya idadi na muda wa kupishana katika kupata watoto.
Kila mzazi anahaki ya kuchagua kwa hiari muda wakupata mtoto/watoto pasipo kulazimishwa na mtu mwingine. Wanawake katika jamii nyingi za Kitanzania wamekuwa hawana haki ya kuchagua idadi ya Watoto na hata kuchagua muda wakupishanisha mtoto mmoja na mwingine, hivyo kupelekea watoto wengi kuzaliwa wakiwa wamepishana umri mdogo sana na kuathiri ukuaji wa watoto kwa sababu ya matunzo mabovu yanachongiwa pia na watu wengi kuwa na uchumi unaochechemea.
Kupata huduma za afya ya uzazi kwa urahisi.
Kila mtu anahaki ya kupata huduma ya afya ya uzazi, na hakuna kiwango cha umri kwa kutumia huduma za afya ya uzazi na njia za uzazi wa mpango. Unatakiwa kuanza kutumia huduma za afya ya uzazi pale unapoona unazihitaji. Na hasa iwapo mtu ameamua kupata mtoto, anapaswa aende kwanza kwenye huduma za afya ya uzazi, na kupata ushauri juu ya ujinsia na masuala ya afya ya uzazi pamoja na njia mbalimbali za uzazi wa mpango.
Vijana kisheria wamepewa haki ya kutumia njia za uzazi wa mpango, Siyo haki kwa jamii kukataa kuwahusishwa vijana katika masuala ya uzazi kwani vijana ndio wazazi wa kesho na wasipokuwa na elimu sahihi ya uzazi wanaweza kuharibikiwa. Kama kijana, una haki sawa ya kupata elimu/ushauri juu ya masuala ya uzazi kama watu wengine.
Kujilinda kutokana na mila zenye madhara kama vile ukeketaji wa wanawake.
Tendo la ukeketaji ni aina ya ukatili wa kijinsia. Ukeketaji au tohara ya wanawake ni hatari sana kwa msichana anayetahiriwa. Wasichana hufa kutokana na madhara yake makubwa zaidi kwa vile:
■Hutokwa na damu nyingi.
■Uambukizo unatokea iwapo vifaa vilivyotumiwa havikuwa safi. Uambukizo unaweza kuenea mpaka katika viungo vya ndani vya uzazina kusababisha ugumba na hata vifo.
■Hatari ya kuambukizwa Virusi vya UKIMWI wakati wa ukeketaji.
■Kuziba kwa mkojo na damu ya mwezi (hedhi) ndani ya mwili wa mwanamke na kusababisha uambukizo.
■Matatizo na maumivu makali wakati wa kujamiiana na wakati wa kujifungua kutokana na kupungua ukubwa wa uke. Ukeketaji wa wanawake mara nyingi una madhara ya kisaikologia ambapo wasichana hupoteza tumaini na imani kwa walezi au wazazi na wanaweza wakapata mateso ya kujisikia waoga, kufadhaika, kutojiweza na kutokuwa kamilifu kimwili.
Kiafya hakuna sababu ya kumtahiri msichana, kinyume chake inaweza kusababisha idadi ya matatizo ya afya. Ukeketaji hautakiwi na dini yoyote na hata sheria inakataza.
LIKIZO YA UZAZI
Likizo ya uzazi ni haki kwa kila mama anayefanya kazi kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa na ni muhimu katika afya ya mama na mtoto lakini zaidi ukuaji wa mtoto. Hata hivyo kwa mujibu wa shirika la kazi duniani (ILO) lililopitisha mkataba wa likizo ya uzazi mwaka 1919, suala hili limekuwa changamoto kwa mamilioni ya wazazi katika nchi nyingi duniani kutokana na sheria za kazi zilizowekwa na waajiri wao.
Mwanamke mwajiriwa anapaswa kumfahamisha mwajiri wake nia ya kuchukua likizo ya uzazi angalau miezi mitatu kabla ya tarehe ya makisio ya kujifungua huku akiambatanisha kielelezo cha daktari juu ya ujauzito. Likizo ya uzazi inaweza kuchukuliwa wiki nne kabla ya kujifungua au mapema zaidi iwapo kuna uthibitisho wa daktari kwamba ni muhimu kufanya hivyo kwa ajili ya afya ya mama au mtoto. Mama ana haki ya kupewa likizo ya uzazi sio chini ya siku 84 yenye malipo.
Vilevile kwa aliyejifungua mtoto zaidi ya mmoja (mapacha au zaidi) anapaswa kupewa likizo ya uzazi ya siku 100 yenye malipo.
Iwapo mtoto amefariki. Mwanamke ana haki ya kupewa tena likizo ya uzazi ya siku 84 yenye malipo endapo mtoto wake atafariki katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kuzaliwa.
Mama mwajiriwa haruhusiwi kurudi kazini katika kipindi cha wiki sita za mwanzo tangu kujifungua isipokuwa pale tu atakapokuwa ameruhusiwa kufanya hivyo na daktari. Pia anaporudi kazini mama anayenyonyesha ana haki ya kupewa muda wa saa mbili kwa siku wakati wa kazi kwenda kumlisha/ kumnyonyesha mtoto wake.
Likizo ya uzazi kwa baba mwajiriwa.
Sheria ya ajira inampa likizo ya siku zisizopungua tatu zenye malipo baba wa mtoto aliyezaliwa. Kwamba siku hizo zichukuliwe katika muda wa wiki moja ya kwanza tangu kuzaliwa kwa mtoto. Kwa kawaida likizo hiyo ya siku 3 hutolewa mara moja tu katika mzunguko wa likizo ya mwaka bila ya kujali idadi ya watoto watakaozaliwa katika kipindi hicho. Yaani likizo hii hutoka mara moja tu kila mwaka hata kama baba ana watoto aliowapata zaidi ya mara moja katika mwaka husika.
Likizo inampa baba fursa ya kumhudumia mama na mtoto, kumsaidia mama kujenga msingi mzuri wa kumlisha mtoto na pia kutafuta mahitaji ya familia.
Baba wa mtoto aliyezaliwa anaweza pia kupewa likizo isiyopungua siku 4 yenye malipo, wakati wa kuuguliwa na mtoto, kifo cha mtoto au kifo cha mwenzi wake.
Likizo hiyo ya siku 4 hutolewa mara moja katika kipindi cha mzunguko wa likizo ya mwaka bila kujali idadi ya matukio yaliyojitokeza katika kipindi hicho.
Hata hivyo, mwajiri anaweza kuidhinisha mwajiriwa kuchukua siku zaidi zisizo na malipo kulingana na tatizo alilopata.
Makala hii imeandaliwa na FASMO Tanzania,
Kwa msaada wa Makala kutoka Umoja wa Mataifa (UN), shirika la SemaTanzania na wadau mbalimbali wa masuala ya haki za binaadamu
Na
Charles Msigwa.
Fasmo Tanzania.
0759948211
Comments