SIKU YA CHAKULA DUNIANI

Tarehe 16 mwezi oktoba kila mwaka ni maadhimisho ya Siku ya chakula duniani. Siku hii ilihasisiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula, (FAO) mnamo mwaka 1979. Tarehe ya leo pia ni maadhimisho ya miaka 75 ya FAO tangu kuanzishwa kwake.
Lengo kuu la maadhimisho haya ni kuongeza uelewa kwa watu kuhusu umuhimu wa chakula na uhakika wa chakula na lishe kwa watu wote duniani hasa wale walio katika hatari ya kukosa chakula kabisa.

Chakula ni moja kati ya mahitaji muhimu ya kila binadamu, hivyo ni sehemu ya maisha yetu kila siku kwa kuwa bila chakula uhai wetu hutetereka.

Hivyo, tunaposherehekea siku ya chakula duniani, jiulize;

1. Nina uhakika wa chakula? Kama ndiyo (naweza kununua, kuandaa na kula chakula cha kutosha) je vipi kuhusu ambao hawawezi kula hata mlo mmoja kwa siku?

2. Chakula ninachokula ni salama? Ni kisafi, kimeandaliwa katika hali gani, hakina vijidudu vyovyote au sumu ya aina yoyote itokanayo na vijidudu hivyo (kama vile sumukuvu itokanayo na kuvu au fungi), hakiwezi kunisababishia madhara ya aina yoyote?

3. Je, chakula ninachokula ni bora? Chakula bora ni kipi? Je, naweza kusema nina ulaji bora?

4. Vipi kuhusu upande wa lishe wa chakula ninachokula? Je, kinakidhi mahitaji ya virutubishi mwilini? Vipi kuhusu mlo kamili?

5. Kuna madhara yoyote ya ulaji chakula kisicho bora? Je, magonjwa kama kisukari, saratani, magonjwa ya moyo yanahusiana na tabia za ulaji usio bora?

6. Ni vyakula gani ambavyo vipo katika mazingira yangu na ni bora, upatikanaji wake ni mwepesi na hata uandaaji, lakini sina mazoea ya kuvitumia?

7. Je, nazingatia ustaarabu wa kula muda wa kula kama vile kupakua kiasi ninachoweza kula na kumaliza, kula kwa kutulia sio huku natembea?

8. Je, tabia ya kununua au kuandaa chakula kingi mwisho wa siku kinaharibika na kutupwa inafaa kuendelea?

9. Ni mazoea gani niliyo nayo kuhusu chakula na ulaji ambayo najua siyo sahihi lakini siwezi au sitaki kuacha?

Kuna vitu vingi kuhusu chakula ambavyo vinahusiana na afya pamoja na maisha yetu kiujumla. Chakula hutumika kama namna ya kuwakilisha utamaduni wa watu fulani kwa mfano nchini Tanzania, ugali ni chakula pendwa kwa kabila la Kisukuma, kama ilivyo wali kwa Wapogoro, wakati tambi huliwa sana na Waitaliano.

Upande mwingine chakula kina kazi kubwa kiafya kwani hutupatia nishati ili kutuwezesha kufanya shughuli mbalimbali kila siku.

Ni vema kuzingatia yafuatayo;

1. Unaweza kujihakikishia usalama wa chakula kwa kula chakula kilichoandaliwa sehemu salama kama vile nyumbani, lakini katika hali ya usafi. Hii huenda sambamba na utunzaji wa chakula kikiwa bado hakijapikwa. Sehemu zingine salama ni ambazo migahawa au hoteli ambazo zinaaminika kuwa wanaanda vyakula katika usafi na usalama wa hali ya juu ( hii hata kwa macho unaweza kuona kwa upande mmoja)

2. Chakula unachokila ndiyo kinakutengeneza jinsi ulivyo ( YOU ARE WHAT YOU EAT). Ukila kisicho bora basi matokeo yake yatakuwa wewe ambaye sio bora.

3. Chakula bora ni kile kinachoupa mwili virutubishi vinavyotakiwa kwa uwiano unaotakiwa. Hivyo punguza ulaji wa vyakula visivyo bora kama bile vyenye mafuta mengi, chumvi pamoja na sukari kwa wingi.
# Ulaji bora ni ule unaozingatia vyakula kutoka katika makundi yote matano kwa uwiano unaotakiwa. Makundi hayo ni;
- Nafaka, mizizi na ndizi mbichi
-Jamii ya mikunde na vyakula asili ya nyama
-Mboga mboga (za majani hata zile za asili)
-Matunda (hata yale ya msituni ila yanayoliwa)
-Sukari, asali na mafuta

4. Kuandaa, kununua au kupakua chakula kingi kuliko mahitaji ambayo hupelekea kuharibika au kutupa chakula ni kitendo kisichofaa. Ni heri kupeleka chakula kilichozidi kwa walio na uhitaji.

5. Achana na mazoea ya ulaji usiofaa kwani unaweza usiwe na madhara ya haraka na ya moja kwa moja lakini yakaja kujitokeza baadae ambapo katika mazingira yetu inakuwa ni kazi kujua chanzo cha matatizo hayo. Magonjwa kama kisukari, saratani na magonjwa ya moyo kuhusiana sana na ulaji wa chakula usiobora.

6. Unaweza kuwa na uhakika wa chakula (food security) lakini ni muhimu kutazama na upande wa lishe wa chakula unachokula. Yaani kama kinakidhi mahitaji ya mwili ya virutubishi kulingana na umri, shughuli za mwili pamoja na jinsia.

Juu ya yote, Hakikisha unakula, kwani kula ni burudani.

Kula, ishi halafu furahi kwa kuweka tabasamu😁

"Grow, nourish, sustain. Together. Our actions are our future."

Na
Innocent Oswald Sanga
Nutritionist 
Fasmo Tanzania

Comments

Popular posts from this blog

Mitindo Yetu Ya Ulaji.

Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.

MADHARA YA UTENGANO WA KIJAMII YALIYOSABABISHWA NA COVID19