Sisi na Elimu Yetu
Nikiwa kwenye hekaheka za maisha nilijikuta nimetokea kwenye kijiwe kimoja cha magazeti. Kijiwe hiki sio kigeni kwangu kwa kuwa nimekuwa najituliza hapo mara kwa mara na kushiriki nao mijadala mbalimbali ya kijamii na iliyopamba vichwa vya habari vya magazeti. Kutokana na kijiwe hiki kuwa na biashara ndani yake basi watu wa rika na jinsia tofauti huja kununua magazeti na kupiga soga huku wauza kahawa nao wakishinda hapo kusukuma gurudumu. Kijiwe hiki kina sheria mbili kuu, mosi huruhusiwi kutumia lugha ya matusi eneo hilo. Pili ni marufuku kuvuta sigara eneo hilo. Ni sheria hizi mbili zinazofanya wengi kutonunua magazeti na kuondoka kwa haraka, huvuta muda kujadili kitu kidogo kwa kuwa staha ni kubwa. Nikiwa kijiweni watu wote wanachangia maada ambayo pia imetawala mitandaoni. Mada yenyewe ni "Elimu Itolewayo Tanzania na Mustakabali Wake". Kijiwe hiki kama vilivyo vijiwe vingi hapa mjini, watu wanajua sana vitu. Watu wanaupeo na upendo inapokuja suala la kuandaa hatma nzuri y...