FAHAMU KUHUSU UZITO WAKO

Watu wengi hufikiria uzito uliozidi mwilini ni wingi wa mafuta tu. Kwa upande mmoja fikra hizi huchangiwa na kile wanachokiona kwa mtu husika, yaani mtu kuonekana akiwa na amejaa nyama uzembe mfano upande wa mbele wa tumbo/ kitambi (haswa wanaume ingawa siku hizi hata wanawake wanakuwa na vitambi pia) au sehemu zingine za mwili mapajani, kiunoni na kifuani. 
Maana ya uzito wa mwili.
Uzito wa mwili huchangiwa na mafuta, misuli, mifupa, tishu zingine zikiwa na maji au ni sawa na kusema uzito wa mtu upo katika sehemu kuu mbili, yaani uzito wenye mafuta (fat mass) na ule usiohusisha mafuta (fat free mass). Unaposema mtu ana kilogramu 50, maana yake uzito huu umechangiwa na vitu vyote vilivyotajwa hapo juu bila kuhusisha nguo wala kitu kingine chochote. Na msemo kwamba takribani 75% ya mwili wa binadamu ni maji maana yake ni kwamba asilimia hizi zinachukua sehemu yote ya uzito wa mtu, yaani asilimia zinazobaki ndio uzito halisi wa kila kinachobaki mwilini baada ya kutolewa maji yote.


Uzito salama au usio salama ni upi?
Mitazamo ya watu wengi ni kwamba wembamba ndio muonekano unaotakiwa hivyo kuwa na uzito mdogo ndio uzito salama lakini cha kushangaza ni kwamba watu wengi hawawezi kusema kuwa na uzito fulani ndio  uzito salama. Kwa hiyo mitazamo kama hii huwa ni kama soga tu.

Ili kujua uzito wa mwili kama ni salama au sio salama, wanasayansi waligundua kipimo rahisi kinachohusianisha uzito na urefu wa mtu (Body mass index-BMI). Ili upate BMI ya mtu, unachukua uzito wako katika kilogramu gawanya kwa urefu wako katika mita skwea (m^2) na viwango vifuatavyo ndiyo hutoa majibu:
chini ya 18.5 - uzito pungufu
18.5 - 24.9 - uzito unaofaa (salama)
25-29.9 - uzito uliozidi sio salama
zaidi ya 30 - uzito uliokithiri (sio salama/hatari)

Lakini kipimo hiki hakitoshi kukupa majibu sahihi kwa uhakika kwa sababu uzito usio salama unahusishwa na wingi wa mafuta mwilini na kipimo hiki hakitenganishi ni kwa kiasi gani uzito wa mtu ni mafuta na yapo sehemu gani mwilini. NI vyema kujua ya kuwa sehemu ambayo mafuta yapo mwilini hutoa taarifa kama yanamuweka mhusika katika hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza kama vile magonjwa ya moyo, kisukari n.k

Hivyo kwa sababu urahisi wa kutumia kipimo hiki katika mazingira yetu, hii ndio huwa njia pekee inayotegemea ingawa kuna njia zingine ambazo zinaweza kuonesha mchango wa kila sehemu ya mwili katika uzito wa mtu husika, hivyo kujua kama ni mafuta au tishu nyingine ndio zinachangia kwa kiasi kikubwa katika uzito wa mhusika. Njia nyingine ambayo hutumika pamoja na hii ya uwiano wa uzito na urefu ili kujua uzito na kuonesha kiasi cha mafuta mwilini (eneo la katikati) ni kupima mzingo wa kiuno (Waist circumference) kwani wingi wa mafuta katika eneo hili huonesha uwezekano wa mtu kupata magonjwa yasiyoambukiza.

Wanaume huhifadhi  mafuta sehemu ya juu ya mwili haswa mbele ya tumbo kwa kiasi kikubwa kuliko sehemu nyingine ya mwili na mafuta haya huhusianishwa kwa kiasi kikubwa na magonjwa yasiyoambukiza wakati wanawake wanahifdhi mafuta sehemu ya chini ya mwili haswa kwenye hipsi na makalioni  kuliko sehemu zingine na mafuta haya hayana uhusiano kwa kiasi kikubwa na magonjwa yasiyoambukiza.

USIYOYAJUA KUHUSU UZITO WAKO
Wanasayansi wanaamini kwamba mwili wa binadamu una namna yake ya kutunza/kumeiniteini uzito kama ufanyavyo kwa hali zingine kama vile joto la mwili, sukari katika damu na hali zingine ndio maana baada ya mtu kufikia uzito fulani na kujaribu kuongeza au kupungua, mwili hujiseti ili urudi katika uzito wake wa mazoea, Mfano: ni kazi sana kwa mtu aliyepungua kutunza/kumeiniteini uzito alioufikia au kwa mtu aliyeongeza uzito kubaki na uzito alioongeza.

Mwili wa binadamu una seli mahususi kwa ajili ya kuhifadhi mafuta mwilini. Seli hizi huongezeka idadi kipindi cha ukuaji hasa kipindi cha kubalehe. Mtu anapokula vyakula vyenye nishati zaidi kuliko ile anayoitumia, seli hizi huongezeka saizi yake na ulaji huu ukiendelea wakati matumizi ya nishati yakiwa ni madogo vilevile, seli hizi huongezeka idadi maradufu ili kuweza kuhifadhi nishati hii inayozidi kama mafuta. Hii inatusaidia kutambua kwamba hata pale mtu anapoamua kufanya jitihada za kupungua, seli hizi hupungua saizi tu na sio idadi, maana yake ni rahisi sana kwa mtu huyu kurudia uzito mkubwa unaochangiwa na mafuta kwa sababu tayari ana mazingira rafiki yanayowezesha mwili wake kuhifadhi mafuta hayo.

KAA UKIJUA:
Unapswa kumthamini mtu kwa dhana zingine za kibinadamu kama vile uadilifu, upendo, hekima na sio kwa muonekano wake kama ni mnene au mwembamba. Kwani hii itawasaidia watu wengi wenye muonekano wa unene kuepuka misongo ya mawazo itokanayo na kuitwa majina yasiyopendeza

Kuwa mnene/uzito uliozidi sio dhambi na zaidi ya yote sio kila mwenye uzito uliozidi ana hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza na sio kila mwenye uzito unaofaa hayupo katika hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza.

Muunganiko wa mazoezi na ulaji unaofaa ndio njia pekee na salama itakayokuokoa katika safari ya kupunguza uzito utokanao na mafuta mwilini. Achana na kufanya dayati ili kupunguza uzito badala yake badili mfumo wako katika ulaji na shughuli za mwili ili uweze kupunguza mafuta katika njia salama na kuweza kuutunza uzito huo.

 Mafuta mwilini sio mabaya kabisa, kwani mwili hutumia kama njia ya kujihifadhia nishati kwa ajili ya matumizi yake kama wewe uwekapo fedha benki ili ukipatwa na shida ya kifedha uwe na pa kukimbilia sema utofauti ni kwamba mafuta yakizidi mwilini ndipo shida huanza ila fedha zikizidi.


Ni ukweli usiopingika kwamba watu wengi wanataka kupungua kwa malengo ya kutaka kuwa na muonekano fulani ambao kwa  kiasi kikubwa ni kutaka kuwa na mwili mwembamba au kilo chache na sio kwa sababu za kiafya. Sasa basi, ni vyema kutambua kwamba unapotamani kuufikia mwili wa saizi ya ndoto zako, kwa uharaka kama ambavyo watu wengi hufanya, unaenda kubadili mazoea ya mwili na ya mtindo wako wa maisha kwa kiasi kikubwa na kama una lengo la kutunza uzito utakao ufikia basi hakikisha unajiandaa kwa kuwa na mpango madhubuti unaotekelezeka laasivyo utarudi ulikotoka

Na 
Innocent Sanga
Mtaalamu wa Lishe.
Fasmo Tanzania.

Comments

Popular posts from this blog

Mitindo Yetu Ya Ulaji.

Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.

MADHARA YA UTENGANO WA KIJAMII YALIYOSABABISHWA NA COVID19