FURAHIA UNENE AU UPUNGUZE KWA STAHA
- Get link
- X
- Other Apps
Watu wengi huanza taratibu za kupunguza uzito wa mwili sababu tu wameambiwa 'aise umenenepa' na mtu fulani au kwa sababu amevutiwa na mwenzie ambaye mwili wake ni mdogo au kuona nguo nyingi zimeshaanza kuwa ndogo au kwa sababu kasikia unene au uzito uliozidi sio salama kiafya.
Ila ukweli ni kwamba, hata kama utaweza kuyafikia malengo ya kupunguza unene/uzito wa mwili wako ni kheri kuyafikia malengo yako kwa njia sahihi ambayo itakuwezesha kudumisha uzito wa mwili wako bila kuumiza wala kukuletea madhara mwilini.
NIJUE NINI KABLA YA KUANZA KUPUNGUZA UZITO WA MWILI?
Ni vyema kufahamu ya kuwa kuwa na uzito uliozidi sio dhambi ingawa watu wengi hutumia muonekano wa watu wanene (ambao mara nyingi huwa na uzito uliozidi) kuwatania kwa kuwaita majina mabaya na unyanyapaa mwingine na kwa kiasi kikubwa hii ikimpata mtu ambaye hajikubali jinsi alivyo, basi hupelekea kufanya vitu vyenye madhara zaidi.
1. Tambua ya kuwa uzito wa mwili huchangiwa na sehemu kubwa mbili, sehemu yenye mafuta (fat mass) na sehemu ya mwili isiyo na mafuta (fat free mass- na hii ndio huwa na misuli, mifupa n.k) pamoja na maji na kwa kiasi kikubwa sehemu ya uzito wa mwili inayochangiwa na mafuta ndio huwa inamuweka mhusika katika HATARI ya kupata magonjwa yasiyoambukiza na hivyo mafuta haya ndio yanatakiwa kupungua mwilini. Zaidi ya yote ni vyema kutambua ya kuwa sehemu ambayo mafuta yamehifadhiwa mwilini kwa wingi ndio inaonesha hatari kwa mtu kupata magonjwa haya, na tafiti zinasema mafuta yanayohifadhiwa sehemu ya tumbo (central adiposity) ndio yanahusiana na magonjwa haya zaidi kuliko yale yanayohifadhiwa sehemu zingine za mwili.
2. Uzito uliozidi husababishwa na muingiliano wa sababu zaidi ya moja zikiwemo; sababu za kijenetiki na mazingira. Sababu za kijenetiki huhusisha vitu vingi vikiwemo vichocheo kama vile Leptini na ghrelini ambapo leptini hufanya kazi ya kuzuia hamu ya kula na kuongeza matumizi ya nishati mwilini wakati ghrelini hufanya kazi ya kuchochea hisia za kula yaani kukufanya utake kula na pia kusaidia mwili kuhifadhi nishati. Kwa kifupi ni kwamba, Leptini husaidia usijisikie njaa na hivyo usifanye jitihada za kula wakati ghrelini hukufanya ujisikie njaa na hivyo kupelekea kutafuta chakula kilipo.
Mazingira huhusisha vitu vyote tunavyokula pamoja na shughuli za mwili (physical activities). Mazingira ya sasa yanatuweka katika ushawishi mkubwa wa kula vitu ambavyo sio rafiki kiafya na vinachangia kuongeza uzito kwa kiasi kikubwa, mfano, vyakula vyenye sukari na mafuta kwa wingi. Ulaji kupitiliza ukichangiwa na uvivu wa kutoshughulisha mwili, hupelekea kuongezeka uzito kwa watu wengi sana haswa maeneo ya mijini.
Tambua kwamba, hata watu wanaokuzunguka wana mchango mkubwa katika kupelekea ule mlo bora au usio bora. Mfano; ukiwa na rafiki zako wakiagiza nyama choma na chipsi, ni rahisi na wewe kuagiza chakula kile kile kwa sababu ya msukumo wa watu waliokuzunguka kwa kuogopa kuwa tofauti.
3. Sababu za msingi ambazo unaweza ukazitumia kufanya maamuzi ya kupungua au kutokupungua ni kama, kiasi cha uzito uliozidi ulichofikia (extent of overweight), umri wako, afya yako kiujumla na jenetiki ya mwili wako. Sababu hizi zitakuonesha ni kwa kiasi na umuhimu gani unahitaji kupunguza uzito wa mwili wako kwani sio kila mwenye uzito uliozidi atapata magonjwa yasiyoambukiza na sio kila mwenye uzito salama hatopata magonjwa yasiyoambukiza.
4. Njia nyingi za kupunguza uzito mkubwa kwa muda mchache haswa zinazohusisha matumizi ya vidonge au dawa zingine sio salama kwa afya ya mtu. Hii hujumuisha taratibu za ulaji zinazozuia/kuepuka ulaji wa vyakula fulani (hasa wanga) kabisa katika mlo wa mtu husika. Sababu ni kwamba, baadhi ya njia hizi hazijathibitishwa na pia huhusisha madhara mengine mwilini kama vile kupoteza virutubishi kama vitamini na madini kwa kutapika au kuharisha
Zaidi ya yote ni vigumu kwa watu hawa kutunza uzito wanaoufikia kwa sababu wanabadilisha utaratibu wa mwili na maisha kiujumla kwa muda mfupi na kujikuta wanarudi walikotoka mapema sana na kukata tamaa
5. Unashauriwa kupunguza uzito wa mwili taratibu kwa kutumia njia salama na kwa kuweka malengo yanayotekelezeka. Tafiti zinathibitisha ya kuwa watu wanaofata njia hii huweza kupunguza uzito wa mwili na kuutunza pale wanapofikia lengo kuliko wale ambao huamua kufata njia za mkato zenye kuleta majibu ya haraka.
Kulingana na uzito wa mtu alionao kabla ya kuanza kupungua wataalamu tunashauri mtu apungue kwa walau kilogramu 0.2 hadi walau kilogram 0.9 kwa wiki au 10% ya uzito wako kwa muda wa miezi 6, yaani ukiwa na kilogramu 60, maana yake yakupasa upungue wastani wa kilo 6 ndani ya miezi 6 ambayo ni sawa na kilogramu moja kwa mwezi mmoja. Hivi ndivyo viwango salama vya kupunguza uzito kwani vinamuwezesha mhusika kubadilika taratibu na kuweza kutunza afya na uzito atakaoufikia.
Watu wengi hufurahia kupungua kilogramu nyingi kwa muda mchache, lakini kikubwa cha kujiuliza ni, Je, nimepungua kwa njia na kiwango salama?
Kumbuka; kulingana na hali ya afya ya mhusika, wataalamu wanaweza wakashauri kutumia njia mbadala kama vile kutumia madawa au kufanya upasuaji ili kupunguza uzito wa mtu husika. Hivyo ni vyema kujua yakuwa hata njia hizi mbadala huwa na madhara pia.
6. Mabadiliko madogo na ya taratibu yanayohusisha ulaji wa chakula bora na shughuli za mwili (mazoezi) ndio njia bora, salama na sahihi itakayokusaidia kupunguza uzito wa mwili uliozidi.
Ni vyema kutambua ya kuwa aina, kiasi cha chakula pamoja na aina ya mazoezi na muda unaotumika kufanya mazoezi hayo ni vitu muhimu sana kuzingatia ili njia hii ikuletee matokeo chanya na yakudumu.
Tunashukuru kwa uwepo wako katika ukurasa wetu, kwa kujali afya na mienendo ya wengine unaweza ukasambaza elimu hii kwa wengine. Ahsante.
Imeandaliwa na:
Innocent O Sanga
Mtaalam wa Afya na Lishe
Family Smile Organization.
- Get link
- X
- Other Apps
Comments