Mfumo wetu wa mmeng’enyo wa chakula, je umesahaulika?

Mfumo wetu wa mmeng’enyo wa chakula, je umesahaulika?

Ukikaa ukaangalia mambo mengi kwa makini utaona kwamba watu wengi huangaika na uzuri wa sehemu za miili yao wanazoziona. Ndio maana utakuta kuna huduma nyingi sana zinazohusu kutengeneza kucha, nywele (almaarufu kama saluni), kufanya maseji ya sehemu mbalimbali za mwili, skrabu. Ingawa huduma za afya zipo maeneo mengi lakini huduma ya uchunguzi ya mfumo wa chakula haipewi kipaumbele kama sehemu kubwa ya inayoweza kutumika kutatua matatizo mengi ya afya yanayoisibu jamii.

Ni mara chache sana watu wengi wakipatwa na shida za kiafya hufikilia kuhusu afya ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula. Hii sio kibongo bongo tu bali hata nchi za wenzetu suala hili halipewi kipaumbele na watu wa kawaida pamoja na wale walioelimika katika sekta ya afya (wataalamu wa lishe, madaktari, wafamasia n.k)

Hii ina maana kwamba kuna uwezekano mkubwa, matatizo mengi ya afya zetu yanaweza yakawa yanatokana na shida zilizopo katika mfumo huu kwa unafanya kazi kubwa katika miili yetu lakini hatuyamalizi kwa sababu hatujui na tulishapuuza umuhimu wa mfumo huu ambao hufanya kazi kama injini ya gari.

Kwa kuyaona haya tarehe 29 mei mwaka 2004, maadhimisho rasmi ya siku ya afya ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula yaliadhimishwa kusherehekea miaka 45 ya kuanzishwa kwa shirika la Gastroenterolojia Ulimwenguni. Hivyo kila mwaka katika tarehe hiyo, watu wote ulimwenguni huja pamoja kutafakari na kujifunza zaidi juu ya afya ya mfumo huu kama sehemu muhimu ya afya ya mwanadamu. Kauli mbiu ya maadhimisho haya kwa mwaka huu ni “Afya ya mmeng’enyo wako wa chakula: mfumo wa mmeng’enyo wa chakula wenye afya tangu mwanzo” au “your digestive health: a health gut from the start”. Kauli mbiu hii inalenga kutoa uelewa kwa kuakisi namna ambavyo mfumo huu unaanza kufanya kazi tangu mtu akiwa mtoto mdogo hadi pale anapozeeka. Mfumo huu huendelea kubadilika na kufanya kazi zote kumpatia mtu mahitaji yake kulingana na mabadiliko mengine ya mwili wake. 



Mfumo wa mmeng’enyo wa chakula unaanzia mdomo na kuishia sehemu ya nje kabisa ya haja kubwa ya miili yetu. Hapa katikati kuna vitu vingi sana vinaunganisha na kuufanya kufanya kazi kwa umaridadi mkubwa kila sehemu ikifanya kazi yake. Sehemu hizi ni kama vile ulimi, tumbo, utumbo (mkubwa na mwembamba), maini, nyongo, kongosho, kidole tumbo. Mfumo huu unahusisha utoaji wa vimeng’enya na vitu vinginevyo kama vile mate, vichochezi, nyongo n.k katika kukifanyia kazi chakula kinacholiwa ili kuzalisha nguvukani au viini lishe vinavyoweza kutumika sehemu mbalimbali za mwilini.

Ni vyema pia kuelewa ya kwamba sehemu kubwa ya kazi za mfumo huu hufanywa pasipo kuhusisha amri zetu sisi wenyewe ingawa kuna vitu kama vile kuamua kula, kutafuna, kumeza chakula hufanyika kwa maamuzi yetu sisi wenyewe.

Pamoja na kwamba watu wengi wanauchukulia mfumo huu kikawaida, lakini watu wengine ambao wapo waliamua kuupa mfumo huu umakini, walingundua mambo mengi sana kiafya yanayohusiana na mfumo huu ikiwemo, sababu zinazopelekea watu wengine kunuka sana midomo, hisia mbaya za kimaisha (kujisikia vibaya), magonjwa ya Ngozi (vipele, chunusi n.k). moja kati ya watu hawa ni GUILIA ENDERS ambaye ameandika kitabu kiitwacho THE GUT, kinachoelezea vitu vingi ambavyo havizungumzwi na wataalamu wengi wa afya kipindi hiki, akianza kwa kuelezea namna ambavyo alijifanyia tafiti yeye mwenyewe na kugundua masuala mbalimbali ambayo mfumo huu unayafanya katika miili yetu. Ni katika ugunduzi wa watu kama hawa mfumo huu umeweza kuitwa UBONGO WETU WA PILI au THE SECOND BRAIN kutokana na kazi zinazofanywa na mfumo huu mwilini.

            

Baadhi ya magonjwa yanayohusiana na mfumo wa mmengenyo wa chakula yanayosumbua watanzania, afrika na dunia kiujumla:

  1. Vidonda vya tumbo

  2. Saratani ya koo, utumbo, kongosho (mdogo au mpana)

  3. Constipation (choo kigumu)

  4. Bawasiri

  5.  Ugonjwa wa seliaki (celiac disease)

  6. Inflammatory bowel syndrome na irritable bowel syndrome

  7. Kiungulia (Heart Burn)

  8. Kisukari (aina ya pili)

Sababu kuu ya magonjwa mengi yanayohusu mfumo huu ni ulaji mbovu, ukihusisha aina, idadi ya milo na kiasi cha chakula husika baina ya watu wengi ulimwenguni. Haipingiki kwamba kuna sababu zingine zinazohusika katika kusababisha magonjwa haya, lakini ulaji mbovu ni sababu kuu ambayo hata mimi na wewe kwa miaka mingi tunaweza kuwa tumeitetea kama haki yetu ya msingi. Kuna nadharia ya kwamba watu wengi wana URAIBU NA CHAKULA ndio maana kuna watu wanakula mara 3 hadi 6 kwa siku wengine mara 1 na wote hawa wanaishi vizuri wakiwa na afya bora. Hii ina maana kwamba kuna uwezekano wa mtu kula mlo mmoja (almaarufu kama OMAD au One Meal A Day) kwa siku na akawa na afya thabiti.

Hivyo, fasmo Tanzania inaungana na watu wote ulimwenguni kukumbusha mambo yafuatayo kuhusu mfumo wako wa mmeng’enyo wa chakula ili uweze kuwa na afya bora:

  1. Tafuta kuelewa kwa usahihi kuhusu mfumo wako wa mmeng’enyo wa chakula: unaweza kufanya hili kwa kupitia wataalamu wa lishe, kusoma vitabu na kutumia mitandao

  2. Kuwa mwangalifu wa chakula unachoruhusu kingie kinywani mwako: hii ni kwa sababu ukiingiza ubovu, tegemea kuvuna ubovu huo huo, hata kama itachukua mwaka mzima baadaye. Pika chakula chako mwenyewe au kula nyumbani. Nunua chakula bora kilichoandaliwa kwa hali ya usafi na usalama, ikibidi zalisha chakula chako mwenyewe.

  3. Funga au kaa bila kula. Haimaanishi utaacha kabisa kutumia chakula. Inashauriwa utumie vinywaji kama chai (ya majani ya kijani au meusi) au kahawa ya ubuyu isiyo na sukari n.k. Jiulize swali, kwa nini ukiumwa unakosa hamu ya kula? Unazani mwili unajaribu kukwambia kwamba sihitaji chakula kwa kipindi hiki? Jibu unalo na unajua mazoea yetu, kipindi cha uginjwa ndicho mtu hulazimishwa hata kula lakini kumbuka huu mwili unaweza kujiendesha na una akili. Kuna taratibu rasmi na bora zinazoshauliwa kufuatwa wakati wa kufunga, wengine hufunga masaa 48 hadi 72. Zingatia ifanyike kwa usahihi ili iwe na manufaa kwa afya ya mfumo wako wa chakula (fuata ushauri wa mtaalamu wa lishe/afya)

  4. Epuka baadhi ya vyakula kabisa kama vile nafaka za kisasa zote (mahindi, ngano, mchele n.k), sukari/asali/matunda ya kisasa yenye sukari/, mafuta ya kupikia yatokanayo na mbegu za mimea pamoja na margarine, vinywaji vya viwandani (soda, pombe n.k)

Fasmo tunajali afya yako. Jizingatie na wewe si.

Na:

Innocent Sanga.

Baba Lishe.

Comments

Popular posts from this blog

Mitindo Yetu Ya Ulaji.

Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.

MADHARA YA UTENGANO WA KIJAMII YALIYOSABABISHWA NA COVID19