Sisi na Elimu Yetu
Nikiwa kwenye hekaheka za maisha nilijikuta nimetokea kwenye kijiwe kimoja cha magazeti. Kijiwe hiki sio kigeni kwangu kwa kuwa nimekuwa najituliza hapo mara kwa mara na kushiriki nao mijadala mbalimbali ya kijamii na iliyopamba vichwa vya habari vya magazeti.
Kutokana na kijiwe hiki kuwa na biashara ndani yake basi watu wa rika na jinsia tofauti huja kununua magazeti na kupiga soga huku wauza kahawa nao wakishinda hapo kusukuma gurudumu. Kijiwe hiki kina sheria mbili kuu, mosi huruhusiwi kutumia lugha ya matusi eneo hilo. Pili ni marufuku kuvuta sigara eneo hilo. Ni sheria hizi mbili zinazofanya wengi kutonunua magazeti na kuondoka kwa haraka, huvuta muda kujadili kitu kidogo kwa kuwa staha ni kubwa.
Nikiwa kijiweni watu wote wanachangia maada ambayo pia imetawala mitandaoni. Mada yenyewe ni "Elimu Itolewayo Tanzania na Mustakabali Wake". Kijiwe hiki kama vilivyo vijiwe vingi hapa mjini, watu wanajua sana vitu. Watu wanaupeo na upendo inapokuja suala la kuandaa hatma nzuri ya taifa lao. Kila mmoja anachangia lake, kuanzia sera, masomo, ubunifu; ufundishaji, lugha ya kufundishia, kuboresha maslahi ya waalimu na miundombinu mpaka idadi ya miaka ya kusoma.
Kuna umuhimu wa mawazo yao kuchukuliwa na sio kuishia hapahapa. Mbali na yote wachangiaji wengi wamejikita katika muundo wa elimu, kitu gani kiongezwe na kitu gani kitolewe.
Nikiendelea kuwasikiliza wenzangu, nikajikuta nawakumbuka watu mbalimbali ambao kwa sababu kadha wa kadha hawakuendelea na masomo. Wengine katika ngazi ya msingi, wengine sekondari na wengine chuo. Kwa harakaharaka katika safari yangu ya elimu nimeshuhudia watu zaidi ya 200 wakiishia njiani na kushindwa kuendelea na shule. Sababu ni nyingi na zinaumiza mioyo sana.
Kwa kumbukumbu yangu hii ndipo ninapopata mchango wangu katika mada. Nje ya jitihada mbalimbali za serikali na wadau wa elimu lakini idadi ya watoto ambao wanaacha shule na kutoendelea na masomo bado ni kubwa. Hii ni mbali na wale ambao hawajaanzishwa shule au kuandikishwa. Tukiyajumlisha makundi mawili hayo kuna idadi kubwa sana ya watoto waliokatika umri wa kwenda shule wapo mtaani.
Wazo langu
Je! kwa nini tusiwe na siku maalumu ya kuwakumbuka watu walioshindwa kuendelea na masomo?
Siku hii itasaidia kuangazia visa na sababu zinazosababisha watu kutoendelea na shule na hivyo kutumika kama funzo kwa wanafunzi wa sasa ili waweze kuzishinda na pia kuwa chachu ya kutatuliwa kwa changamoto zingine za kimazingira na kimfumo zinazopelekea watu kutoendelea na shule.
Ripoti ya UNICEF Tanzania ya mwaka 2016 inaonyesha watoto milion 1.33 sawa na asilimia (14.4) wa shule ya msingi (umri miaka 7-13) hawapo shuleni. Ripoti hii pia inaonyesha watoto milioni 2.3 (57%) wa sekondari (umri miaka 14-17) hawako shuleni. Hii inafanya jumla ya watoto milioni 3.6 wa umri wa shule kutokuwepo shule. Hii ni kwa mwaka wa utafiti ila hali imekuwepo miaka nenda, miaka rudi.
Kuna umuhimu kuangazia suala hili kwa mapana yake. Kubainisha visa, mikasa na sababu zinazopelekea hali hii kuwepo na hata kuongezeka kila uchwao.
Binafsi kwa niliyoyaona na niliyobaini kama mikasa na sababu za watoto kutokuwepo kwenye mfumo wa elimu rasmi ni
1. Vifo
Vifo vinavyosababishwa na magonjwa, vipigo na unyanyasaji, ajali za magari, moto na mitumbwi. Mwaka 2017 mkoani Arusha ilitokea ajali ya basi la shule likiwa na wanafunzi na kusababisha vifo vya wanafunzi zaidi ya 30. Kwa upande mwingine vipigo vikali kutoka kwa walimu kiasi cha kusababisha kifo kwa mwanafunzi huwaogopesha wazazi na wanafunzi wengine kwenda shule.
2. Magonjwa sugu na majeraha
Magonjwa kama kifafa, magonjwa ya akili, magonjwa ya neva na mifupa yamesababisha sana watoto kutoendelea na shule na wengine kutoandikishwa kabisa. Hii ni kutokana na kushughulikia matibabu kwa muda mrefu, hofu ya kumpeleka mtoto shuleni angali mgonjwa pamoja na mazingira ya shule zetu kutokuwa rafiki.
3. Ulemavu
Ulemavu wa viungo unaonekana hata usionekana umefanya wazazi wengi kuwaficha na kutowapeleke watoto shuleni na pia mara nyingi hata watoto kukataa shule kwa kuwa shuleni hawapati upendo na mazingira rafiki kama miundombinu rafiki na usafi kwa wao kujifunza kwa utulivu. Uwepo wa shule za walemavu umesaidia sana lakini kuna changamoto ya uchache wa hizo shule kwenye baadhi ya wilaya hapa nchini.
4. Kukosa ada na mahitaji
Licha ya uwepo wa elimu bure lakini bado kuna wengine hushindwa kugharamia mahitaji ya shule na chakula. Kwa mfano mzazi hana hela ya kumpa mtoto ale shule, hivyo mtoto hujikuta anaona ni heri abaki nyumbani ale kuliko kwenda shule kushinda njaa. Pia kuna wengi sana hushindwa kuingia au kuendelea na vyuo vikuu au vya kati kwa kukosa ada na gharama nyingine.
5. Kufeli mitihani
Hususani mitihani ya taifa ambayo huwazuia wao kuendelea na masomo ya ngazi za juu. Wengi hufeli kidato cha nne, sita na hata vyuoni na kushindwa kujiendeleza kielimu hivyo kuishia mtaani.
6. Mimba za utotoni
Watu wengi sana ambao hupata mimba wakiwa bado wanafunzi hushindwa kuendelea na shule hata wakishajifungua. Hii ni kutokana na mazingira ya malezi kwa vichanga na pia hamasa ndogo kutoka kwa wasimamizi wa elimu na wazazi. Kwa mujibu wa Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya (TDHS) wa mwaka 2015-2016, mwanamke mmoja kati ya wanawake wanne wenye umri wa miaka 15 hadi 19 tayari wana watoto (mama).
Chapisho hilo pia lilitanabaisha kuwa kila mwaka, wastani wa wanafunzi 8,000 wa kike huacha shule kutokana na ujauzito.
7. Ndoa za utotoni.
Bado kuna mikoa wazazi wana kawaida ya kuwaozesha watoto wao wakiwa bado wadogo. Wengi wameozeshwa baada ya kumaliza darasa la saba na wengi sana wameozeshwa baada ya kidato cha nne hivyo kushindwa kuendelea na madarasa ya juu hata kama wamefaulu. Takwimu za shirika la Watoto Duniani (UNICEF 2012) lilitaja Tanzania kuwa ya tatu kwa Afrika kwa kuwa na ndoa nyingi za utotoni. Mkoa wa Shinyanga ukiongoza kwa 59%, ukifuatiwa na Tabora 58%, Mara 55%, Dodoma 51%, Lindi 48%. Mikoa mingine inayofatia ni pamoja na Mbeya 45%, Morogoro 42%, Singida 42%, Rukwa 40%, Ruvuma 39%, Mwanza 37%, Kagera 36%, Mtwara 35%, Manyara 34%, Pwani 33%, Tanga 29%, Arusha 27%, Kilimanjaro 27%, Kigoma 26%, Dar es Salaam 19% na Iringa 8%.
8. Tamaa ya maisha na fedha
Wapo watoto wengi ambao wameacha shule ili wafanye kazi au biashara na wapate hela. Hii pia inachochewa na umasikini uliokithiri kwenye jamii zetu, kupungua kwa thamani ya elimu kwa kuwa hata waliomaliza vyuo hawana maisha mazuri yenye ushuhuda. Mbali na hayo pia michezo wa kamari na upataji wa pesa kirahisi imechochea tamaa ya maisha kwa watoto kisha kujikuta wameacha shule.
9. Mkumbo na ujinga
Wapo watoto waliocha shule kisa wenzao wameacha, wengine huacha shule kisa adhabu za shuleni na kutotaka kujihimu kuamka (kukataa kuwajibika). Nakumbuka kuna mwanafunzi mwenzangu alipewa adhabu kutohudhuria shule (suspension) kwa wiki tatu, baada ya muda kuisha yeye hakurudi kabisa shule na taarifa zilisema alikataa kuendelea na shule kabisa.
10. Malezi na shinikizo kutoka kwa wazazi au walezi.
Wazazi wengine hawawajibiki ipasavyo, hawafuatilii maendeleo na kuhamasisha shule kwa watoto wao. Suala la shule hubaki kwa mtoto kuamua kusoma au kuacha. Pia wazazi huwashinikiza watoto kutokwenda shule na kuwapeleka kwenye kazi zao au vibaruani. Wengine husafirishwa na kutumika kama wasaidizi wa kazi mijini hivyo safari ya elimu kutoendelea.
11. Mila na imani potofu
Zipo imani za kidini na kimila ambazo elimu sio kipaumbele. Hivyo mtoto hutopelekwa shule kwa kuwa kwao elimu ya dunia au ya darasani haina thamani. Na hata watoto nao hujikuta hawazingatii na wanaacha shule kwa kuwa elimu haithaminiki kwao. Siku ya darasani ila mtoto anapelekwa kwenye mikutano ya kidini.
12. Uonevu na unyanyasaji katika mazingira ya shule.
Vipigo vikali kutoka kwa walimu, unyanyasaji kati ya wanafunzi kimaumbile, kiakili na hata kijinsia. Kuepuka mateso hayo wengine hujikuta wanaacha shule. Tumeshuhudia mikasa ya unyanyasaji wa kijinsia ukifanywa na walimu kama mwalimu kumtaka mwanafunzi kimapenzi na mwanafunzi akikataa hufelishwa au kuadhibiwa bila sababu zinzoeleweka. Pia wanafunzi wa madarasa ya kujuu kuwanyanyasa wa madarasa ya chini.
13. Umbali wa kufika shuleni
Umbali mrefu huleta uchovu, uvivu na uwoga. Kuna watoto ilikufika shule huhitajika kutembea kilomita nyingi na kukatisha misitu, vichaka na mito. Shule shikizi "satellite schools" husaidia katika ngazi ya awali ila madarasa ya juu changamoto hiyo husababisha wengine kuacha kutokwenda shule kwa kukatazwa na wazazi kwa sababu za kiusalama na mazingira mabovu.
14. Kukimbilia vipaji
Kuna watoto wamebarikiwa vipaji mbalimbali. Na hujikuta wanafanya vizuri katika vipaji vyao kiasi kuamini ni kheri waache masomo ya darasani na kujikita zaidi kwenye michezo na maigizo. Wapo wengi waliachana na shule na kwenda kucheza mpira na kuigiza. Baadhi walifanikiwa na wengine kutokana na mifumo yetu kutokuwa rafiki kwa vipaji walikosa vyote (elimu na mafanikio kutokana na kipaji)
15. Wamefungwa magerezani
Kutokana na mikasa mbalimbali ya maisha kuna idadi ya watoto wapo kwenye mahabusu na magereza ya watoto na watu wazima. Jambo hili huwazuia kuendelea na masomo. Mwaka 2015 kuna tukio la kuchomwa moto kituo cha polisi jijini Dar es salaam. Kati ya watuhumiwa 8 waliokutwa na hatia katika tukio hilo mmoja wao alikuwa bado mwanafunzi. Hukumu ilivyotolewa 2019 alihukumiwa kifungo cha maisha jela pamoja na wenzake.
16. Adhabu angamizi.
Kwa kuwa shule ni sehemu ya kujifunza hivyo adhabu ni sehemu ya kumfundisha mtoto. Kwa bahati mbaya sana kuna adhabu ambazo hutolewa sio kulenga kufundisha bali kumuangamiza mtoto. Kwa mfano kumrudisha nyumbani kwa muda (suspension) isiyo na ukomo, kumfukuza shule mwanafunzi na kutomruhusu hata asifanye mtihani wa taifa.
Hakika visa vya watu kuacha shule na kutoendelea na masomo ni vingi na vinasikitisha. Kama tunavyojionea kuna sababu za udhaifu katika taasisi, kuna sababu za kijamii, sababu za kiafya na sababu binafsi za mtoto. Katika sababu binafsi za mtoto kuna zingine zinakuwa nje kabisa ya uwezo wa mtoto kuhimili. Nakumbuka nikiwa kidato cha tano kuna rafiki yangu mmoja ilimlazimu kuacha shule ili akawalee wadogo zake waliokuwa shule ya msingi kwa kuwa wazazi walikuwa wameshafariki na ndugu hawakuwaweka karibu. Safari yake ya elimu iliishia pale.
Ni mikasa hiyo inayoniwazisha kuwepo na siku au wiki ya wanajamii, wanafunzi, walimu na wadau wote wa elimu kuadhimisha au kuwakumbuka wale wote walioshindwa kuanza shule au kuendelea na masomo kwa sababu mbalimbali. Kwa kuwa licha ya lengo kuu la taifa la kupambana na ujinga, idadi kubwa sana ya walioacha shule wanaishi maisha duni, kutokana na kukosa elimu ya kutumia kama silaha ya kupambana na umasikini.
Dhumuni la siku hiyo
1. Kukumbushana visa na sababu zinazochangia watoto kutoendelea na masomo.
2. Kujadili namna ya kupunguza au kumaliza kabisa visababishi vya watoto kutoanzishwa shule au kuacha shule.
3. Kuwaasa watoto na wazazi faida za elimu na namna ya kuzishinda changamoto zinazoweza kuwafanya waache shule.
4. Kuwajengea watoto tabia ya kusema yanayowasibu nyumbani, shuleni na mtaani ili waweze kusaidika kwa haraka.
5. Kuwakumbuka walioshindwa kuendelea na masomo kwa sababu zilizo nje kabisa ya uwezo. Mfano vifo, ulemavu wa akili nk
6. Kukemea uonevu "school bullying" na unyanyasaji wa aina zote.
Matokeo tarajiwa
1. Maboresho ya mazingira ya upatikanaji wa elimu, miundombinu, sheria, sera.
2. Kuongezeka kwa uelewa kwa wanajamii. Hii itasaidia kuongezeka kwa watoto wanaoanzishwa shule na wazazi kusimamia maendeleo ya watoto.
3. Kuongezeka kwa ukaribu wa kiutendaji na usimamizi kati ya uongozi wa shule, serikali za mitaa na wazazi.
4. Matendo ya unyanyasaji wa kimwili, kiakili na kijinsia kukemewa na watu kwa umoja.
5. Kujengeka taifa la watu wanaoithamini elimu.
6. Watoto kuwa huru na jasiri katika kujieleza na kutetea haki zao.
Itafanyikaje?
Kiuhalisia siku moja haitoshi, kama ni siku basi ni kilele. Inaweza ikatambulika wiki. Kwa mfano wiki ya kwanza ya kila mwezi wa pili itatumika na ijumaa ndiyo itakuwa kilele chake.
●Waalimu watazungumza na wanafunzi
●Kuratibiwa kwa vikao vya wazazi na shule
●Watendaji serikali za mitaa watazungumza na wanajamii juu ya masusla ya umuhimu wa elimu na kupinga ndoa za utotoni, kazi nzito kwa watoto na unyanyasaji
●Elimu kupitia vyombo vya habari
●Kupaza sauti juu ya miundombinu mibovu ya kujifunzia.
●Viongozi wa serikali kama afisa elimu, wakuu wa mikoa, wilaya na wizara pamoja na wadau kutembelea shule na vyuo kutoa hamasa ya watoto kushika elimu na kutatua changamoto zilizopo.
Gharama zake
Kuna namna inaweza kufanyika ikafanya kukawa na gharama na kuna namna ya kuepuka gharama kabisa. Kama itafanyika chini ya usimamizi wa serikali za wilaya na mitaa na idara za elimu basi wafanyakazi (walimu na maafisa) watatekeleza kama majukumu yao ya kila siku. Ila kama itafanyika kwa mfumo wa kuhusisha matembezi, maonyesho itahitaji gharama.
Kwani hamna siku zingine?
Ni kweli kuna siku ya elimu duniani, siku ya waalimu duniani, siku ya mtoto wa afrika nk. Siku zote hizo kwa kiasi hutumika kuelezea elimu. Lakini kwa bahati mbaya hatuna siku maalum kwa mazingira yetu ya kitanzania ya kupigania elimu yetu kwa maendeleo yetu. Kila mtanzania kuna namna anaguswa na elimu, aidha kwa kuhitaji elimu au kuhitaji na wengine wapate elimu. Kwa pamoja kwa kujitambua au kutojitambua yatupasa kupigania haki ya elimu bora kwa vizazi na vizazi.
Kama aishivyo yoyote mwenye ndoto, basi ni shauku yangu siku moja kuona kama taifa tunakuwa na vitu na mifumo yetu imara ya kuifanya haki ya elimu bora inawafikia wengi wote wanaostahili bila kuwa na kizuizi chochote.
Na
Nobel Edson Sichaleh,
Fasmo Tanzania.
Comments
Now all that’s left is implementing
Great work Sir