Yakimbie Magonjwa Sugu Yasiyoambukizwa.
Tupo ndani ya mwezi wa kuadhimisha kujikinga na kupambana na magonjwa sugu yasiyoambukiza. Maadhimisho haya haswa huanza tarehe 6 hadi 13 mwezi Novemba kila mwaka ambapo hiyo wiki huwa ni kilele chake.
Lengo la maadhimisho haya ni kuifahamisha na kukumbusha jamii uwepo wa magonjwa haya hatari na kujua jinsi ya kujikinga na kuyatibu. Magonjwa yasiyoambukiza ni magonjwa yote ambayo hayawezi kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Mara nyingi huwa ni ya kudumu na ni matokeo ya muunganiko wa sababu za kijenetiki, mazingira, tabia pamoja na fiziolojia (ufanyaji kazi wa sehemu mbalimbali za mwili wa mtu).
Mfano wa magonjwa haya ni kama magonjwa ya mfumo wa mzunguko wa damu (kiharusi na mshtuko wa moyo), kisukari, saratani na magonjwa katika mfumo wa upumuaji kama vile athma (asthma). Magonjwa mengine ni kama magonjwa ya akili, majeraha, selimundu na ulemavu.
Kati ya magonjwa haya, magonjwa katika mfumo wa mzunguko wa damu yanaongoza kusababisha vifo vya watu wengi zaidi duniani, ikifuatiwa na saratani, magonjwa katika mfumo wa upumuaji na mwisho ni kisukari. Hii ni kutokana na taarifa ya shirika la afya duniani la umoja wa mataifa.
Hali ya magonjwa yasiyoambukiza nchini kiujumla kulingana na taarifa ya shirika la afya duniani, inaonesha takribani 27% ya vifo vyote nchini vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza.
Magonjwa yanayoongoza kusababisha vifo nchini ni: ·
● Magonjwa katika mfumo wa mzunguko wa damu.
● Magonjwa mengine yasiyoambukiza (mfano: selimundu, majeraha, magonjwa ya akili n.k)
● Saratani – saratani ya mlango wa kizazi, matiti na kaposi sarcoma kama aina za saratani zinaoongoza kuonekana nchini.
●Magonjwa katika mfumo wa upumuaji.
●Kisukari
Kiwango cha watu wanaoathiriwa na magonjwa haya kinaweza kikawa ni zaidi ya hiki kinachoripotiwa kwa sababu mara nyingi, watu wengi hawapimi ili kujua afya zao kwa maana kwamba mtu anaweza akawa na ugonjwa usioambukiza lakini akashindwa kupata vipimo stahiki ili aweze kutibiwa na kurahisisha utunzaji wa taarifa hizo, hivyo huyu anaweza akapoteza uhai pasipokuiwezesha mamlaka kuhifadhi taarifa za sababu zilizopelekea kifo.
Hali ya magonjwa mengine yasiyoambukiza.
● Selimundu (sickle cell anemia); Tanzania ni nchi ya nne duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa na ugonjwa huu, nchi zingine ni India, Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Takribani watoto 11,000 huzaliwa kila mwaka wakiwa na ugonjwa huu nchini. Kwa kiasi kikubwa watoto hawa hukua bila kutambua kama wana ugonjwa huu na inakadiliwa 50-90% ya watoto hawa hufariki bado wakiwa wadogo kama hawatapatiwa matibabu.
●Majeraha – hasa yanayosababishwa na ajali za barabarani, kuanguka na mashambulizi.
●Magonjwa ya akili – Zaidi ya 1% ya watu wote nchini wana magonjwa sugu ya akili.
Vihatarishi vinavyopelekea watu kupata magonjwa yasiyoambukiza nchini ·
■ Matumizi ya tumbaku na bidhaa zake hasa SIGARA (hupelekea saratani kama vile ya mapafu) zaidi ya 16% ya watu wote nchini ni watumiaji wa tumbaku katika mitindo tofauti tofauti.
■ Matumizi ya pombe kupindukia (pombe inaonekana kuongeza uwezekano wa kupata aina nyingi za saratani hasa zile za mdomo, koo, matiti na tumbo. Pia magonjwa ya ini) ·
■ Kutoshughulisha mwili/kutokufanya mazoezi (husababisha uzito wa mwili kuongezeka maradufu haswa kama ulaji ni mbovu)
■ Ulaji usiofaa - matumizi ya vyakula vyenye sukari na mafuta kwa wingi (hupelekea uzito wa mwili kuongezeka maradufu haswa kama mtu hashughulishi mwili/kufanya mazoezi)
Vihatarishi vingine
● Uzito uliozidi na unene uliokithiri · Shinikizo la juu la damu
● Kuongezeka kwa kiasi cha mafuta kwenye damu (lehemu, triglaiselaidi).
●Sababu za kijenetiki. Mfano, katika ugonjwa wa selimundu
Ni vyema kutambua ya kuwa kuna magonjwa yasiyoambukiza ambayo ni rahisi kuyaepuka kwa kuwa na mtindo mzuri wa maisha. Magonjwa hayo ni kama vile saratani za aina mbalimbali, kisukari na magonjwa katika mfumo wa damu.
Jinsi ya kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza (Kisukari, Saratani, Magonjwa katika Mfumo wa Damu na Upumuaji) ·
● Kuepuka matumizi ya pombe kupitiliza ·
● Kuepuka matumizi ya tumbaku na bidhaa zake hasa uvutaji wa sigara na kufikiwa na moshi wa mtu anaetumia bidhaa hizi
● Kuwa na uzito wa mwili unaofaa (pata ushauri kuhusu uzito wako kutoka kwa mtaalamu wa lishe) ·
● Fuata kanuni za mlo bora – epuka matumizi ya vyakula vyenye mafuta na sukari kwa wingi, nafaka zilizokobolewa, nyama zilizosindikwa.
● Tumia nafaka ambazo ni salama na hazijakobolewa, matunda na mboga za majani zenye rangi mbalimbali. (Pata ushauri Zaidi kutoka kwa mtaalamu wa lishe) ·
● Epuka vyakula vya nafaka, jamii ya kunde, karanga au korosho ambavyo havikuhifadhiwa vizuri. Vyakula hivi huota UKUNGU ambao husababishwa na fangasi ambazo hutoa sumu iitwayo sumu kuvu au AFLATOXIN. Sumu hii huweza kuongeza uwezekano wa kupata baadhi ya saratani.
● Fanya mazoezi/ Shughulisha mwili kwa kuzingatia ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya. ·
● Weka na fuata utaratibu wa kupima afya ya mwili: Mfano kupima uzito, mzingo wa kiuno, kiasi cha mafuta katika damu, shinikizo la damu, kiasi cha sukari n.k. Fuatilia na elewa maana ya majibu ya kila kipimo kutoka kwa wataalamu wa afya.
Jinsi ya kujikinga dhidi ya magonjwa mengine yasiyoambukiza ·
● Ni vyema kufuata taratibu na sheria za kiusalama katika matumizi ya vyombo vya usafiri ili kuepuka ajali ·
● Kuhakikisha uwepo wa vifaa vya huduma ya kwanza maeneo hatarishi ili kupambana na madhara pale yanapotokea.
● Kuwatembelea wataalamu wa afya ya akili mara kwa mara ·
● Kufanya vipimo ili kujua kama mtu ana amebeba na kuna uwezekano wa kupata mtoto mwenye magonjwa ya kijenetiki kama vile selimundu.
Magonjwa yasiyoambukiza, hasa yale yanayotokea kwa sababu ya mtindo wa maisha huanza taratibu na kulingana na taratibu za watu wengi kutokufatilia afya zao kwa sababu hawaoneshi dalili za kuumwa, hufanya wagundue kuwa ni wagonjwa kwa kuchelewa na katika hatua za mwisho, hivyo kufanya uwezekano wa kupona kuwa mdogo. Hali hii huwapelekea kulazimika kuishi na magonjwa haya kwa muda wote wa maisha uliobaki.
Hivyo basi ni vyema kuwa na utaratibu wa kufatilia mwenendo wa afya yako mara kwa mara kwani magonjwa haya ni hatari na idadi ya waathirika inaongezeka kwa kasi nchini na duniani kwa ujumla.
Imeandaliwa na:
Innocent Sanga.
Mtaalamu wa Lishe.
Comments