UNYONYESHAJI WA MAZIWA YA MAMA PEKEE NA UTATUZI WA CHANGAMOTO ZAKE

UNYONYESHAJI

 "Thamini Unyonyeshaji, Weka Mazingira Wezeshi”


(Picha kutoka mtandaoni)

Unyonyeshaji ni kitendo cha kumpatia mtoto maziwa ya mama moja kwa moja kutoka ziwani. Ni njia bora kabisa ya kumlisha mtoto mchanga kwasababu:

  • Maziwa ya mama yana virutubisho vyote muhimu kwa ukuaji wa mtoto

  • Yana kinga dhidi ya magonjwa (hasa maambukizi ya tumbo na mapafu)

  • Hujenga uhusiano wa karibu kati ya mama na mtoto

  • Ni salama, safi na ya gharama nafuu

Aina za maziwa ya mama

  • Maziwa ya njano ya awali: Maziwa ya mwanzo yenye kinga mwili nyingi

  • Maziwa ya mpito: Hutokea siku chache baada ya kujifungua

  • Maziwa kamili: Maziwa kamili yenye virutubisho vyote.


Unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee (exclusive breastfeeding) unapendekezwa kwa miezi sita ya mwanzo bila kumpa mtoto maji, uji na vyakula vingine

HALI YA UNYONYESHAJI WA MAZIWA YA MAMA PEKEE.

Tafiti mbalimbali za kidunia na kikanda zinaelezea hali ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee. Wakati baadhi ya nchi unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa watoto ukiwa katika viwango vizuri kuna nchi zingine hali siyo ya kuridhisha.

Kidunia

Takribani 44% ya Watoto chini ya miezi sita hunyonyeshwa maziwa ya mama pekee. Lengo la Shirika la Afya Duniani (WHO) ni kufikia 50% ifikapo mwaka 2030 na kuendelea kuongezeka. Changamoto kubwa ni hizi:

  • Wanawake wengi wanarudi kazini mapema

  • Msongo wa Mawazo unaongezeka

  • Kutokunyonyesha mara kwa mara

Afrika

Kwa Afrika idadi ya watoto waliopo chini ya miezi sita wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee ni takribani 43%-47% baadhi ya nchi zinafanya vizuri zaidi ya asilimia 60% lakini zingine zipo chini sana kwa sababu:

  • Lishe duni kwa mama

  • Imani potofu

  • Ukosefu wa msaada wa kitaalamu

Tanzania 

Kwa mujibu wa tafiti kama ile ya TDHS(2022) takribani 58-60% ya Watoto hunyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa miezi 6. Tanzania iko juu sana tofauti na nchi nyingi za Afrika hii ni kwa sababu ya kampeni za lishe bora na afya ya mama na mtoto na pia ushauri wa wahudumu wa afya kwenye kliniki za wajawazito na Watoto ingawa kuna changamoto zifuatazo:

  • Elimu ya unyonyeshaji bado haitoshi kwa baadhi ya jamii

  • Wanawake wengine huanza kumpa mtoto chakula mapema

  • Uchovu na kazi nyingi za nyumbani hupunguza muda wa kunyonyesha


SABABU ZINAZOPELEKEA MAZIWA YA MAMA KUWA MACHACHE.

Sababu zinazopelekea baadhi ya wanawake baada ya kujifungua kuwa na maziwa machache ni pamoja na

  • Kunyonyesha mtoto mara chache au muda mfupi

  • Msongo wa Mawazo na uchovu. Hii hupunguza hali ya mwili kutengeneza maziwa kwa wingi.

  • Mtoto kushika ziwa vibaya(poor latch)

  • Lishe duni kwa mama

  • Magonjwa (mfano homoni na upungufu wa damu.

  • Kutumia maziwa ya kopo mapema (hupunguza uchochezi wa maziwa ya mama)


VYAKULA VINAVYOSAIDIA KUONGEZA MAZIWA

Hakuna chakula cha miujiza ambacho mtu akila basi maziwa yataanza kuwa mengi, lakini vyakula hivi husaidia kwa namna moja au nyingine kuchochea utengenezwaji wa maziwa mwilini mwa mama aliyejifungua.

  • Mboga za majani(mchicha na matembele)

  • Karanga, ufuta, dengu

  • Nafaka(uji wa mtama,ulezi ,shayiri(oats)

  • Maji ya kutosha (unywaji mwingi ni muhimu sana)

  • Vyakula venye protini kutoka kwa wanyama kama (mayai,Samaki, nyama)

  • Pia kunyonyesha mara nyingi ndio njia kuu ya kuongeza maziwa



HATARI YA KUMPA MTOTO MAZIWA YA WANYAMA AU VYAKULA MAPEMA

  • Kuharisha au maambukizi

  • Mfumo wa umengenyaji haujakomaa

Maziwa ya Ngombe yana protini nzito (casein nyingi) ambazo ni ngumu kumengenywa hii inaweza kusababisha maumivu ya tumbo, kuvimbiwa, na kuharisha.

  • Upungufu wa virutubisho muhimu

Maziwa ya Ngombe yana chuma ndogo sana (iron) husabisha upungufu wa damu pia hayana virutubisho muhimu vya ukuaji wa ubongo kama vile DHA.

  • Hatari ya mzio (allergy)

Baadhi ya wattoto hupata allergy kama vipele, kuharisha, kutapika

  • Hupunguza kunyonya maziwa ya mama


MBADALA KAMA MAZIWA YA MAMA HAYATOSHI KABISA AU MAMA HAYUPO

Kama maziwa hayatoshi kabisa au mama amefariki njia bora zaidi ni hizi

  1. Maziwa ya mama mwingine (wet nursing/donor milk)

  2. Maziwa ya kopo (infant formula)



Maziwa ya kopo

  • Yatayarishwe kwa usafi mkubwa

  • Yatumie maji salama yaliyochemshwa

  • Yafuate kipimo sahihi

Maziwa ya mama ni chakula bora kabisa kwa mtoto

Maziwa machache mara nyingi hutokana na mtindo wa kunyonyesha na lishe

Kunyonyesha mara nyingi + kula vizuri + kupumzika =huongeza maziwa

Kama haiwezekani maziwa ya kopo (infant formula) ndio mbadala.


NAMNA NZURI YA KUONGEZA HAMASA YA WANAWAKE KUNYONYESHA

Ili kuongeza hamasa ya wanawake kunyonyesha, ni muhimu kuzingatia mbinu zinazojumuisha elimu, msaada wa kijamii, na uboreshaji wa afya ya mama. Hii inahusisha hatua za kimwili, kihisia, na kimazingira ili kuhakikisha mama anajiamini na ana uwezo wa kutekeleza jukumu hili muhimu kwa afya ya mtoto. 

Ili kufikia lengo hili, hatua zifuatazao ni muhimu:

  1. Elimu na Uelewa: Ni muhimu kuwapa akina mama elimu sahihi kuhusu faida za kipekee za maziwa ya mama kwa mtoto na mama mwenyewe, ikiwemo ulinzi dhidi ya magonjwa na faida za kiafya za maisha. Elimu hii inapaswa kusisitiza kuwa maziwa ya mama ni chakula bora zaidi kwa miezi sita ya kwanza. 

  2. Msaada wa Kijamii na Kihisia: Kupunguza shinikizo la kujiwekea na kupata msaada kutoka kwa wenzi, familia, na marafiki ni muhimu sana. Hii inajumuisha kuruhusu wengine kusaidia kazi za nyumbani ili mama apate muda wa kupumzika na kunyonyesha kwa utulivu. 

  3. Uboreshaji wa Lishe na Afya: Mama anapaswa kuzingatia lishe bora inayojumuisha matunda, mbogamboga, protini, na nafaka zisizokobolewa, pamoja na kunywa maji ya kutosha ili kuongeza uzalishaji wa maziwa. 

  4. Mazingira ya Kunyonyesha: Kuunda utaratibu mzuri wa kulisha kwa mahitaji badala ya saa, kuhakikisha mtoto anashikana vizuri (latch), na kutumia mbinu kama mgusano wa ngozi kwa ngozi husaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa na kuimarisha uhusiano kati ya mama na mtoto. 

Hitimisho

Maziwa ya mama ni chakula bora kabisa kwa mtoto

Maziwa machache mara nyingi hutokana na mtindo wa kunyonyesha na lishe

Kunyonyesha mara nyingi+ kula vizuri +kupumzika =huongeza maziwa

Kama haiwezekani infant formula ndio mbadala.



Na 

Raheli Oisso

Mtaalamu wa lishe na sayansi ya mlaji

Fasmo Tanzania

#lishe #unyonyeshaji

Comments

Popular posts from this blog

Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.

KIFUA KIKUU: UPO KAMA HAUPO

Mfumo wetu wa mmeng’enyo wa chakula, je umesahaulika?