VIRUSI VYA KORONA KWA WAJAWAZITO NA WANAWAKE WANAONYONYESHA

Ugonjwa wa Coronavirus (COVID-19) ni ugonjwa unaoambukiza unaosababishwa na virusi vya corona. Virusi hivi hushambulia mfumo na hewa na kuleta madhara kadha wa kadha kwenye mwili wa mwanadamu na hata kupelekea kifo. 
Kumekuwa na nadharia na maswali mbalimbali juu ya virusi hivi kwa watoto wachanga, wajawazito na wanawake wanaonyonyesha juu ya namna ya uambukizaji na namna nzuri za kuzuia maambukizi.
Hadi sasa hakuna utafiti unaothibitisha maambukizi ya COVID-19 kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kupitia maziwa ya mama, maji maji katika mfuko wa uzazi (mtoto akiwa tumboni) au sampuli zingine kutoka kwa mama. Bado shirika la afya duniani linasema hakuna uthibitisho wa virus hai vya corona katika sampuli tajwa hapo juu.
Lakini mpaka sasa kinachofahamika ni kwamba watoto kadhaa wamepatikana na virusi vya corona baada tu ya kuzaliwa na haijulikani kama walivipata wakiwa tumboni au baada ya kuzaliwa. Pia vipo visa vya mtoto wa miezi sita, miezi kumi na moja na visa vingine vya watoto kupata virusi vya Corona chini ya umri wa miaka miwili.
Bado tafiti zinaendelea kufanyika kwa hiyo tunaweza kusikia lolote muda wowote kwa sababu hivi karibuni kuna utafiti umegundua uwepo wa virus vya corona katika mbegu za wanaume walioathirika na virusi hivi.

Shirika la afya duniani linapendekeza kipindi mwanamke akiwa na ujauzito adumishe usafi kwa kunawa kwa maji tiririka pamoja na sabuni, kuepuka mikusanyiko, kuepuka kujishika macho, pua na mdomo, kujiziba anapokohoa au kupiga chafya kwa kutumia kitambaa laini au kiwiko. Haya yote yatasaidia kupunguza maambukizi ya virusi vya corona kwa mama mjamzito
Shirika la Afya Duniani (WHO) linashauri mama ambaye anahisiwa au mwenye covid 19 aliyejifungua aendelee kumnyonyesha mtoto kwa sababu maziwa ya mama yatamsaidia kujenga kinga yake ya mwili na huku yakikidhi mahitaji ya virutubishi katika mwili wa mtoto ambavyo anavihiitaji kwa kiasi kikubwa ili aweze kukua vizuri.
Shirika la Afya Duniani linaendelea kusisitiza mama anapomnyonyesha mtoto aendelee kufata taratibu sahihi za ulishaji katika janga hili kama ifuatavyo, hakikisha usafi katika upumuaji (respiratory hygiene) na kuvaa barakoa (mask), osha mikono kabla na baada ya kumgusa mtoto, daima asafishe maeneo na vitu vyote anayotumia wakati wa unyonyeshaji wa mtoto. Hivi anaweza kusaidia kupunguza au kuzuia kabisa maambukizi ya corona virus kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Kama hali ya mama haimruhusu kumnyonyesha mtoto kutoka kwenye matiti yake, inashauriwa kukamua maziwa na kumnywesha mtoto kwa kutumia kikombe safi, kutumia maziwa ya mama mwingine ambayo yamekamuliwa (human donor milk) au kuanza tena kumnyonyesha mtoto baada ya mama kupona (relactation) au kupata nafuu bila kusahau kuendelea kuwa na ukaribu wa mwili na mtoto (skin to skin contact) na kukaa na mtoto katika chumba kimoja. Hii ni kulingana na mapendekezo ya shirika la afya duniani
Ikumbukwe kwamba hakuna utafiti unaothibitisha kuwa wanawake wajawazito wapo katika hatari ya kupata covid 19 zaidi ya watu wengine na hii ni kulingana na shirika la afya duniani (WHO). Ila juu ya yote kila mtu ana wajibu wa kujilinda ilivyo na kuwalinda wanaomzunguka ili kuiepusha jamii yetu dhidi ya gonjwa hili. CORONA IPO NA NI HATARI!!

Na 
Innocent Sanga
Nutritionist
Fasmo Tanzania
0688301558

Comments

Popular posts from this blog

Mitindo Yetu Ya Ulaji.

Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.

MADHARA YA UTENGANO WA KIJAMII YALIYOSABABISHWA NA COVID19