NAMNA VIRUSI VYA CORONA VINAVYOSABABISHA COVID19 HUPIMWA
NAMNA VIRUSI VYA CORONA VINAVYOSABABISHA COVID19 HUPIMWA
Mpaka sasa kuna vipimo (vitendanishi) vya aina kuu mbili vinavyotumika kupima covid-19 vinavyotumika sehemu nyingi duniani kutambua watu wenye maamumbikizi ya ugonjwa huu wa mlipuko uliosambaa sehemu karibu zote za dunia.
Aina ya kwanza ni kile kinacho pima covid-19 kwa kuangalia uwepo wa kinasaba cha kirusi chenyewe (RNA). Kipimo hiki hujulikana kama ‘Real-time Reverse Transcription Polymerase Chain Reaction’ (RT-qPCR) au al-maarufu PCR! Hiki ndio kipimo mashuhuri na ‘standard’ kinachotumika ulimwenguni kwa sasa. Sampuli zake huchukuliwa kwa kulambisha (swab) kijiti cha pamba (cotton swab) ndani-nyuma ya pua (nasophyaryngeal swab) na/au ndani-nyuma ya mdomo (oropharyngeal swab).
Aina ya pili ni ile inayopima kwa kuangalia kinga (antibody) inayozalishwa na muathirika pindi anapopata maambukizi ya kirusi cha corona. Kipimo hichi hujulikana kama ‘Immune Rapid Test, na vipo vya aina tofauti. Aina maarufu kwa sasa ni ya ‘strip’, kama ile strip inayopima ujauzito kwenye mkojo (UPT strip) – aina hii hujulikana kama “Lateral flow immunochromatographic assays” au lateral flow test! Kipimo cha aina hii sampuli yake ni damu inayochukuliwa kwenye kidole (finger prick) au kwenye mkono (venepuncture).
Kipimo hiki kwa sasa sio standard ila kuna kampuni mbalimbali duniani zinazalisha na zimepata vibali vya dharura kutoka FDA (USA) na mamlaka nyengine duniani kuingiza kwenye matumizi. Kwa maelezo hayo bila shaka Maabara yetu ya Taifa huchakata sampuli za covid-19 kwa kutumia kitendanishi ambacho ni standard – PCR. Kitendanishi ambacho sampuli zake huchukuliwa ‘swab’ ya puani/ mdomoni! Sio mate, mkojo, damu wala kinyesi kama wengine wanavyo dhani.
Namna Covid19 inavyopimwa kwa PCR
1. Sampuli ile, pamba (swab), hupokelewa maabara na kuandikishwa (registered) taarifa muhimu kama vile: taarifa za aliekusanya sampuli, taarifa za alieleta sampuli maabara, taarifa za aina ya sampuli (swab ya pua au mdomo), taarifa za aliechukuliwa sampuli n.k.
2. Sampuli hiyo (pamba) hupitishwa hatua tofauti kwa kutumia kitenganishi maalum cha kinasaba cha RNA, kwa jina la kitaalamu ni ‘Viral RNA Extraction Kit’: kama vile, kuosha pamba hiyo (kuondoa kirusi kwenye pamba kiwe kwenye tube), kukipasua kirusi (lysis) ili kutoa kinasaba (RNA) ndani ya kirusi, na mwisho ni kusafisha (purification) ili kubaki na kinasaba cha kirusi tu. Kabla ya kupeleka kwenye PCR, kinasaba (RNA) hicho kilichosafishwa huangaliwa ubora wake (quality)! Ubora wake huhusisha wingi (concentration) na usafi (purity). Kuna kiasi na usafi maalumu ambao kama sampuli haijafikisha hutakiwi kuendelea nayo kwa hatua ya PCR, maana ni ubora usiofaa kwa kutoa majibu sahihi! Kifaa kinachotumika kupima ubora wa kinasaba (RNA) ni ‘spectrophotometer’ – modo maarufu ni ‘Nanodrop’. Sampuli (extracted RNA) ikikidhi vigezo (quality) ya kuendelea kwenye PCR, hupelekwa kwa ajili ya kusomwa ili ijulikane ni kinasaba cha kirusi kinachosababisha covid-19 au la!
3. PCR, hutendanisha kinasaba (RNA) kwanza kwa kukigeuza kutoka RNA kwenda DNA, kisha hutoa kopi nyingi (amplification) kwa kulenga maeneo mawili maalumu ya kinasaba, maeneo ambayo humtofautisha kinasaba cha corona anaesabisha covid-19 na kinasaba cha kirusi chengine chochote hata vile vya jamii moja na yeye, kama virusi vinavyoosababisha MERS na SARS. Kukopika kwa maeneo haya muhimu husomeka moja moja kwenye mashine hii ya PCR na ikifika kiwango kinachokubalika – mashine husoma-positive. Kama kopi itakuwa ni ya eneo moja tu kati ya hayo mawili mashine husoma – indeterminate (inconclusive), na kama hakuna kopi ya eneo hata moja- mashine husoma negative. Kwa majibu ya inconclusive maana yake kunahitajika sampuli nyengine kurudia kipimo.
Muhimu: Sampuli ya mgonjwa mara zote husomwa pamoja na sampuli za kuendeshea (control samples) kwa ajili ya kuhakikisha kama PCR (mashine) inafanyakazi sawa sawa. Sampuli za kontroli hizi ni sehemu ya kinasaba cha kirusi cha covid-19 ambacho hutumika kama positive kontrol na maji maalum (buffer) yenye kila kilichowekwa kwenye sampuli halisi isipokuwa kinasaba (RNA) ambayo hutumika kama negative kontrol. Hivyo majibu hayo hapo juu hukubalika tu endapo postivive control itasoma positive na negative control ikisoma negative.
Kwanini PCR kiwe kitendanishi standard cha COVID-19?
PCR ina sifa mbili bora na muhimu za kipimo cha kimaabara zinazofanya kitendanishi hiki kiwe ndio standard:
1. ‘High Sensitivity’: (a) ‘High analytical sensitivity’ (uwezo kusoma hata kiwango kidogo cha virusi) kwa maana hata kukiwepo na uzi mmoja tu wa kinasaba (single RNA strand) basi PCR inaweza kutendanisha! (b) ‘High clinical sensitivity’ (>95%), kwamaana kama kuna watu 100 wenye covid-19 (positive), basi pasi na shaka PCR mashine itakupa majibu ya positive kwa watu wasiopungua 95 miongoni mwa hao 100! Ijulikane, mpaka sasa hakuna kitendanishi chenye clinical sensitivity ya 100%!
2. ‘High Specificity/Selectivity’: (a) ‘High analytical specificity’ kwa maana ina kopi maeneo mawili ya kinasaba, maeneo ambayo ni maalumu kwa nCov tu, hivyo hata kirusi cha familia moja na nCov hakiwezi kusomwa (haichanganyi), achilia mbali wale wa mbali kama HIV na wengine. (b) High clinical Specificity (99%), kwa maana kama watakuja watu 100 ambao hawana covid-19 (negative), basi pasi na shaka PCR mashine itakupa majibu ya negative kwa watu 99 miongoni mwa hao 100! Hivyo PCR ikisoma positive ujuwe ni positive kweli!
ENDELEA KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA CORONA. JILINDE NA MLINDE MWENZIO.
Kwa usaidizi mkubwa wa makala za......
Dr. Ally Mahadhy, Department of Molecular Biology and Biotechnology, University of Dar es Salaam.
Na
Charles Msigwa
Fasmo Tanzania
Comments