Shairi: LISHE NAISHIKIA KIPAZA
Sauti yangu kuipaza,
Kuna kitu nataka kuongea,
Muda sasa cha nikwaza,
Wasio na sauti wataponea,
Rafiki yao nashika kipaza.
Ni kwa muda sasa,
Jamii yetu ii taabani,
Lishe yaonekana anasa,
Wakulaumiwa nani?
Viongozi wa kisiasa,
Au mitaala ya kizamani?
Tunazalisha mazao,
Hatujui kuyatumia,
Watu wala kikwao,
Vyakula hufakamia,
Shida huja afya zao,
Gharama kujitibia.
Laiti ingetolewa elimu,
Mitaani na darasani,
Wangejua umuhimu,
Nini kiwepo kwa sahani,
Magonjwa wangekuwa adimu,
Ukosefu wa vyakula fulani.
Bungeni ingekuwepo kamati,
Yenye uongozi makini,
Iliyojaa mipango mikakati,
Kuwafikia watu wa chini,
Na kuwawezesha kwa dhati,
Elimu ya lishe waushinde umaskini.
Lishe kwa mtoto na mama,
Ila sio kwa wao tu aisee,
Lishe ni jambo la maana,
Kwa vijana pia wazee,
Wote tuseme hapana,
Kula mlo mmoja pekee.
Mkulima ukitoka kuvuna,
Mavuno hifadhi vizuri,
Pindi yatapokuwa hakuna,
Ghala lako lisiwe sifuri,
Utaendelea kutafuna,
Ukifanya zingine shughuli.
Kutoka makundi mbalimbali,
Chakula bora kisikose mezani,
Kunywa maji mengi tafadhari,
Pombe sigara usiweke kinywani,
Jiwezeshe kwenye kila hali,
Waelimishe na wa nyumbani.
Hapa leo naishia,
Kipaza achukue mwingine,
Lishe bora kuipambania,
Tukutane siku nyingine,
Kwa wewe uliyenisikia,
Mpe ujumbe na mwingine.
A H S A N T E
Lishe Shairi😊
Na
Nobel Edson Sichaleh
MwanaLishe
Fasmo Tanzania
0783961492
Comments
Samahani kwa kuchelewa kujibu.