Watu wanaofaidika kupitia ujinga wako.
"Baba shuleni wametuagiza kesho wanafunzi wote tuwe na Amoeba. Amoeba inauzwa 50000....." Naimani umewahi sikia kauli hizo kwenye stori au hata kuhusika kuwapiga hela wazazi na ndugu kwa kupitia kile wasichojua. Ujinga hauna faida ila kuna watu watanufaika na ujinga wako.
Wahenga walikuwa sahihi sana waliposema "Wajinga Ndio Waliwao". Kupitia ujinga utaibiwa kizembe pasi matumizi ya silaha, utauziwa vitu kwa hati au risiti feki na baadae mambo yatageuka na utatapeliwa hutopata kile ulichonunua wala hela uliyonunulia haitorudi.
Viongozi, wanasiasa na baadhi ya viongozi wa dini wa Kiafrika wanatujua sana. Wanajua wengi wetu ni wajinga. Hivyo hutumia ujinga wetu kunufaika katika kupata nyadhifa au kupata mali. Atakuja kipindi cha kampeni atagawa pombe, vitenge, kofia na kutulisha pilau nyama tutahisi akipata uongozi hayo ndiyo yatakuwa maisha yetu ya kila siku na yeye ndiye mwarobaini wa matatizo yetu. Kura zote kwake, akishinda uchaguzi kuonekana kwake tena ni wakati wa kampeni. Sisi huku hatuna ari, kila kitu kipo kama kabla ya uhuru.
Ujinga unaumiza vizazi hadi vizazi kama hautoondolewa. Baba akifanya maamuzi bila kujua, maamuzi yale wanaweza kugharimu kizazi chote. Kwani uongo? Wazazi waliokataa kusomesha mabinti zao na kuishia kusomesha watoto wa kiume pekee walifaidika nini na kutosomesha mabinti? Vipi kama mabinti nao wangepata elimu sasa hivi si wazazi wangekuwa wanatumiwa hela za kununulia barakoa na vitakasa mikono, sasa hivi hata Bima za Afya wangekuwa nazo. Lakini mabinti waliishia kuozwa na kuwa tegemezi kwa wanaume zao. Kutokujua kunawaumbua sasa.
Waganga wakienyeji nao hufaidika sana na ujinga wetu. Watasema mbaya wako ni jirani yako kalete hiki na kile tena vingine ni vigumu sana kupatikana. Taarifa zinasema kwa sasa Mayai viza yanabei mara mbili ya mayai ya kawaida huko jijini Arusha kwa matumizi ya Uganga na ushirikina. Yote haya ni ujinga tu wanaosema watupe utajiri wao wapo kwenye tope la umaskini. Kutokujua mafanikio huja kwa kujituma na uwekezaji wa rasilimali na muda na sio jambo la kulala na kuamka likawa.
●Usikubali kuwa kitega uchumi cha mtu
●Usikubali kuwa chambo
●Usikubali kutumika kwa manufaa yao mapana
●Fanya tathimini ya kila hatua unayopiga, tathimini kila ofa unayoletewa, tathimini maneno yao.
●Jifunze kukataa sio tu kisicho na manufaa pia hata chenye manufaa ya kinyonyaji.
●Fikiria mbali kabla ya kufanya maamuzi
●Usikae meza moja nao, kama wao hawakuoni wewe ni kama wao.
Ujinga hauna faida yeyote ila kuna watu watafaidika na ujinga wako. AMKA TAFUTA MAARIFA!!
Na
Nobel Edson Sichaleh
Fasmo Tanzania
0783961492
Comments