BABA KAMA BABA

Baba la Baba

Leo tarehe 21 June ndiyo siku ya wenye miji, watu wenye maamuzi nyumbani, watu wenye sauti popote pale ndani hata nje ya nyumba. Ni ukweli, leo ni siku ya watu ambao hawaoni shida kuvuja jasho ili wengine wafurahie leo na kesho yao. Kwa uthabiti kabisa na kuiweka familia nzima mabegani na kutembea huku kaibeba bila kujali hali ya nchi kiuchumi au iwe mvua liwe jua majukumu yake lazima atekeleze. Leo ni siku ya akina Baba Duniani, watu wenye mioyo yao.
Kwa muda sasa kumekuwepo kwa siku hii adhimu ya kuhadhimisha uwepo wa akina Baba na mchango wao katika maisha na ustawi wa wanafamilia. Baba ni mzazi wa kiume, baba ni kiongozi wa familia (kwa mila za sehemu nyingi duniani). 

Kutokana na tamaduni na hali ya maisha ya Afrika akina baba ndiyo wamekuwa watafutaji wakubwa wa mkate wa kila siku katika familia. Kipato hicho ndiyo kitagawanywa na kutumika kama chakula, kama ada, manunuzi ya nguo za wanafamilia, nauli za hapa na pale na matumizi mengine mengi yasiyo na idadi.

Kulingana na tamaduni za Kiafrika, mwanaume ndiyo hujikuta usukani katika shughuli nyingi za kifamilia. Uongozi wa familia kutokana na mama kubanwa na mila, utafutaji wa kipato, akiwaongoza wanafamilia wengine na pia akina baba ndiyo huwa katika jukumu la uongozi wa jamii. Ni rahisi sana kutokana na tamaduni zetu kumkuta Baba wa kiafrika ana majukumu mengi bila msaada. Hivyo hupelekea watoto wake hususani wale wa kwanza kuzaliwa kukaimu baadhi ya majukumu ya wazazi wao.

Kutokana na hali ya Afrika kiuchumi, kiteknolojia na kielimu ambazo kwa pamoja zinawaacha akina mama nyuma, akina baba wanajikuta pia wako na wajibu wa kusimama na kuongoza familia. Wanawake wengi wa Kiafrika hawana au hawakupata nafasi ya kwenda shule, hivyo hujikuta wanafanya kazi nyingi zisizo na kipato kizuri huku wakitumia teknolojia duni. Mchango wa mama kwenye familia unakuwa ni kulea watoto na huchangia kidogo kiuchumi tukilinganisha na mahitaji. Hivyo macho ya mama na watoto kwa pamoja huelekezwa kwa Baba ili amalize shida zote zilizopo. Na akina baba bila kupepesa macho au kujivuta husimama imara kama mnara na kuyafanya yote yawapasayo kadri ya uweo wao.
Hayo ni kwa uchache yanayopelekea uwepo wa siku hii ya leo. Siku ya Akina Baba duniani.
Leo ni siku ya kuheshimu michango mingi ya akina baba katika kutengeneza maadili ya familia.

Leo ni siku ya kuheshimu na kuthamini upendo wa akina baba kwetu sisi sote. Japo wao hupata muda mchache kukaa na sisi lakini daima tunaishi mioyoni mwao na kwa bahati mbaya sana Mungu hajawajalia hulka za kuongelea yanayowasibu.
Leo ni siku ya kuwashukuru akina Baba kwa jitihada zao katika familia zetu kadri ya uwezo wao.

Leo ni siku ya kukumbuka nasaha za akina baba wanazotuambia na walizotuambia katika malezi yetu ambazo zimekuwa miongozo maishani.

Leo ni siku ya vijana wakiume kutathmini jukumu la kuwa baba na vitu gani vya kuzingatia akiwa katika nafasi hiyo. Ikumbukwe ni rahisi kuwa baba mzazi na sio kuwa baba.

Leo ni siku ya kuwakumbuka akina baba wote waliotangulia mbele za haki. Mungu awape amani ya milele.

Leo ni siku ya kuwapost akina baba kwenye kila mtandao wa kijamii😄
Baba Mzazi.
Baba Mlezi.
Baba wa Mbinguni.
Baba wa Taifa.

Family Smile Organization  kwa pamoja na upendo tunawashukuru akina Baba wote ambao hawajawahi kukata tamaa kuzitunza familia zao. Tunatambua wapo akina Baba waliotelekeza familia zao kwa sababu kama umaskini au mama kujifungua mtoto mlemavu lakini haitoshi kuwasahau akina baba wengi ambao wapo kidete kusimamia familia zao. Mungu awabariki baba, daddies, washua, wadingi, wazee, fathers na majina mengine yote haha.

Na
Nobel Edson Sichaleh
Fasmo Tanzania

Comments

Popular posts from this blog

Mitindo Yetu Ya Ulaji.

Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.

MADHARA YA UTENGANO WA KIJAMII YALIYOSABABISHWA NA COVID19