SHAIRI: NJIA PANDA

NJIA PANDA
Nipo njia panda,
Mawazo yanizonga,
Kiza kimetanda,
Fikra zanigonga,
Wapi pa kwenda,
Kivipi nitasonga?

Niache shule,
Nikatumie kipaji,
Niwe kama yule,
Msanii mchezaji,
Nivume huku kule,
Kwa mdogo mtaji.

Nitakuwa maarufu,
Na hela kibao,
Sitaishi kwa hofu,
Yatakuwaje mafao,
Hawatoacha kunisifu,
Katika maongezi yao.

Nitajenga majumba,
Nakumiliki magari,
Kupitia kuimba,
Nitakuwa hodari,
Kwa udi uvumba,
Nitaiteka sayari.

Shule kitu nyeti,
Lakini mimi sielewi,
Kwanini wenye vyeti,
Nafasi hawapewi,
Kwenye viti waketi,
Haki hawatendewi.

Shule haina manufaa,
Wasomi maisha duni,
Sasa wanatuhadaa,
Kisiasa kuturubuni,
Kutuaminisha wanafaa,
Wajinufaishe kiuchumi.

Kipaji changamoto,
Nani wa kukusaidia,
Utaishia kwenye msoto,
Na kuchoka kuvumilia,
Utalia kama mtoto,
Ndoto zisipotimia.

Elimu bado hazina,
Kote ulimwenguni,
Kuiacha hapana,
Hata wakinirubuni,
Nitakosa maana,
Wataniita muhuni.

Shairi la watoto.....
Na
Nobel Edson Sichaleh
Fasmo Tanzania 
Childhood Development 
0783961492

23/06/2020

Comments

Anonymous said…
Kazi nzuri

Popular posts from this blog

Mitindo Yetu Ya Ulaji.

Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.

MADHARA YA UTENGANO WA KIJAMII YALIYOSABABISHWA NA COVID19