Shairi: BINTI MTOTO WA KIKE
Poem
Leo ndio ile siku yao,
Mabinti kusherekea,
Waongee vitu vyao,
Yatupasa vipokea,
Magumu waseme wao,
Yawapasa kuendelea.
Binti Mtoto wa kike, 
Amka kwa pambazuka,
Yenye tija uyashike,
Wakati wako umefika,
Kimaendeleo utumike
Wasiokuamini kuaibika.
Punguza kupiga soga,
Na umbea kila kukicha, 
Wahabarishe mashoga,
Waamke kumekucha,
Waachane na uoga,
Maendeleo kujiepusha
Kujituma iwe tabia,
Usingoje uhimizwe,
Jamii inakusubiria,
Ndoto zako utimize,
Yasokufaa kimbia,
Usisubiri yakuumize.
Mimba kabla ya ndoa,
Rafiki hilo usithubutu,
Kimaisha litakupopoa,
Na kushusha wako utu,
Haswa akikataa kukuoa,
Ndoto zako tapata kutu.
Wewe mtu adhimu,
Acha leo nikupashe,
Ndoto zako muhimu,
Usikubali usiziache,
Ongeza na nidhamu,
Sibwetekee uchache.
AMIN
Na 
Nobel Edson 
Fasmo Tanzania
0783961492
 
   
   
 
 
Comments