Shinikizo Kubwa la Damu

 SHINIKIZO KUBWA LA DAMU 

Utangulizi 

Moyo unapopiga, husukuma damu kwenye mishipa ya damu ili isambae mwilini kote. 

Shinikizo la damu ni hali ambapo msukumo huu wa damu unazidi kiwango cha kawaida na unaweza kusababisha madhara mwilini. 

Madhara ya shinikizo kubwa la damu Shinikizo kubwa la damu linaweza kuleta madhara mbalimbali yakiwemo:

• Kupasuka kwa mishipa ya damu kichwani na kusababisha kuharusi. Kiharusi ni moja ya sababu kubwa za vifo vya watu wazima 
• Moyo kupanuka na hatimaye kushindwa kufanya kazi yake ya kusukuma damu. 
• Kuharibika kwa mishipa ya damu kwenye figo na hatimaye figo kushindwa kufanya kazi yake ya kusafisha damu. 
• Mishipa mikubwa ya damu kuharibika kwa sababu ya kuvuja kwa virutubishi vilivyo kwenye damu na kusababisha kiharusi, ugonjwa wa moyo au miguu kutopata damu ya kutosha. 


Dalili ya shinikizo kubwa la damu 
Wengi wa watu wenye shinikizo kubwa la damu hawana dalili zozote. Waliobaki wanaweza kuwa na dalili zifuatazo: 
• Kuumwa kichwa mara kwa mara. 
• Kutoona vizuri. 
• Kizunguzungu. 
• Moyo kupiga kwa nguvu au haraka haraka 
• Kutokwa na damu puani. 
• Maumivi ya kifua au kupumua kwa shida. 
• Uchovu wa mara kwa mara.

Ili kugundua kama una shinikizo kubwa la damu ni vyema kupima msukumo wa damu kila unapoenda kwenye kituo cha tiba au kupimaangalau mara moja kwa mwaka. 
Wakati mwingine, watu wenye shinikizo kubwa la damu gafla wanaweza kuwa na dalili za kiharusi kama ilivyoelezwa ukurasa unaofuata. Ni vyema ukiona dalili hizi usisite kutafuta msaada wamhudumu wa afya. 


Visababishi vya shinikizo kubwa la damu. Sababu zinazochangia mtu kupata shinikizo kubwa la damu ni pamoja na:- 

• Matumizi ya chumvi kupita kiasi hasa ya kuongeza mezani. 
• Utumiaji wa pombe kupita kiasi. 
• Utumiaji wa tumbaku na bidhaa zake. 
• Msongo wa mawazo kutokana na vitu kama vile majanga, unyanyasaji wa kijinsia, n.k. 
• Umri mkubwa (Miaka 60 na kuendelea). 
• Historia ya shinikizo kubwa la damu katika familia. 
• Uzito mkubwa kupita kiasi - kumbuka unene hauashirii hali nzuri ya maisha bali ni ugonjwa. 
• Kutokufanya mazoezi ya mwili. 
• Ugonjwa wa kisukari. 



Kuzuia shinikizo kubwa la damu Shinikizo kubwa la damu linaweza kuzuilika kwa kuzingatia yafuatayo: 
• Punguza matumizi ya chumvi: chumvi isizidi kijiko kidogo cha chai kwa mtu
• Epuka kunywa pombe kupita kiasi (angalia sura ya pombe). 
• Fanya mazoezi ya viungo mara kwa mara na kujishughulisha na kazi mbalimbali mradi mwili upate mazoezi ya angalau nusu saa kila siku (angalia sura ya mazoezi). 
• Epuka uzito mkubwa kupita kiasi na unene (angalia sura ya unene). 
• Epuka matumizi ya tumbaku na bidhaa zake (angalia sura ya tumbaku). 
• Kula matunda na mboga mboga kila siku (angalia sura ya ulaji unaofaa) 
• Punguza msongo wa mawazo (angalia sura ya msongo wa mawazo).



Comments

Anonymous said…
Hii nzuri
Stephen Mligo said…
Ahsante kwa makala njema zenye kutujenga

Popular posts from this blog

Mitindo Yetu Ya Ulaji.

Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.

MADHARA YA UTENGANO WA KIJAMII YALIYOSABABISHWA NA COVID19