Msimu wa Baridi na Afya.

Kipindi cha mwezi wa sita na mwezi wa saba maeneo mengi sana ya hapa kwetu Tanzania huwa katika msimu wa baridi kali. Kuna sehemu zingine baridi huwa kali kiasi cha saruji/barafu huwepo juu ya ardhi.


Baridi hufanya sisi binadamu kuwa na tabia fulani ili tupate joto na kuishi kwa amani kipindi hiki. Tunabadili mavazi kutoka mepesi kwenda mazito, mabadiliko ya muda wa kulala na muda wa kuamka. Wengine kiwango cha usafi hupungua, kutokana usafi unategemea maji kwa sana na hayo maji kipindi hiki huwa ya baridi kiasi huogopwa. 

Kuna kundi la watu wao kipindi cha baridi hujikuta wanaanza kunywa pombe kali ili kuupa mwili joto bila kujali madhara ya muda mfupi na mrefu.

Juu ya yote kuna tabia moja kipindi hiki cha baridi ambayo sio mbaya lakini ikikosa umakini sio salama. Tabia ya kuota moto. Moto huupasha mwili joto, wapo wanaoota kwa makundi na waoota pekeyao. Unaweza ukawa moto wa kuni au mkaa.


Uotaji wa moto sio njia mbaya katika kuweka mazingira ya ujoto. Ukosefu wa umakini na kutokujua tahadhali wakati wa uotaji wa moto umesababisha ajali na vifo vya watu kadhaa.
Wapo watu ambao wakati wanaota moto walipitiwa na usingizi na kwa bahati mbaya sana kujikuta wanaangukia majiko au moto wenyewe kabisa.

Hatari nyingine, wapo watu ambao huchukua majiko ya mkaa na kujifungia nayo ndani huku hamna hewa inayoingia na inayotoka. Shida huwa pale mkaa unapotoa moshi na mtu kuuvuta ule moshi. 
Kiafya moshi ule ni (carbon-monoxide) ambao ni sumu na hatari kwa afya ya mwanadamu. Kibaiolojia mapafu huanza kuichukua ile sumu kabla ya oksijeni. Hivyo damu mwilini hutawaliwa na hewa yenye sumu, hali hii ikidumu kwa muda hupelekea kifo.

Msimu kama huu wa baridi mikoa ya Iringa, Mbeya na Rukwa huwa vinatokea vifo vinavyosababishwa na majiko ya mkaa. Ni kweli yanaleta joto, lakini ni muhimu kuwa makini nayo.


Kama mtu anaweza kutotumia mkaa basi asitumie ajikite kwenye uboreshaji wa miundombinu ya nyumba kama kuweka madirisha mazuri, silingi-bodi na blanketi zito.

Pale inapokuwa ngumu na kukulazimisha kutumia mkaa basi ni vyema jiko liingizwe ndani ya nyumba pale ambapo mkaa wote ndani ya jiko umekuwa rangi nyekundu na hautoi moshi.

Msimu wa baridi una mambo mengi, tukiendelea kuuongelea hatutamaliza kwa makala moja. Kwa mfano msimu wa baridi huwapelekea wengine kufanya sana vitendo vya ngono. Kwa leo tuishie hapa.



Ahsante kwa kupitia ukurasa wetu.
Sisi FASMO tunakupenda na kukuthamini.

Comments

Popular posts from this blog

Mitindo Yetu Ya Ulaji.

Nafasi ya Maziwa katika Afya Zetu.

MADHARA YA UTENGANO WA KIJAMII YALIYOSABABISHWA NA COVID19