USIACHE KUONGEA NA WATU
USIACHE KUONGEA NA WATU.
Habari yako!
Ni matumaini yangu upo salama na unachukua tahadhari stahiki katika mapambano dhidi ya Korona. Unapojizuia kupata maambukizi pia wakumbushe wengine wajizuie. Usiache kuongea nao!
Viumbe hai vyote vina njia za mawasiliano. Namna ya kuwasiliana kati yao hususani pale wanapotekea familia moja. Kwa mfano Simba kwa simba, Nyani kwa Nyani, Siafu kwa siafu nk. Wakati viumbe vingine vyote vinatumia milio ya asili zao na ishara kuwasiliana baina yao binadamu yeye anatumia Lugha yaani mpangilio wa sauti kuwasiliana.
Binadamu anaongea. Katika kuongea kuna...
●Kuuliza
●Kueleza/Kufafanua
Katika maongezi yetu basi kuna mambo mawili tunayafanya nayo ni Kuuliza au Kueleza. Usiache kuuliza, usiache kueleza (kujieleza, kuelezea) vitu mbalimbali kwa watu waliokuzunguka.
Watu wana vitu wanapitia, wana vitu wamezoea, wana vitu wanapenda jitahidi waongeleshe. Waulize ilikuwaje hivi? Wape nafasi wajieleze kuliko kuhukumu na kulaumu. Hakuna mtu mjinga sana, ni huwa tunatofautiana mitazamo na mazingira ya kufanya maamuzi. Wenda wewe ungekuwa yeye katika mazingira yaleyale ungefanya maamuzi kama yake.
Catherine alimpata binti mmoja akampa kazi ya ufanyakazi wa ndani. Yule binti kila mara alikuwa akimaliza kupika ugali anasahau kuloweka sufuria baadae wanapata uhaba wa masufuria kwakuwa mengi yamelowe kwa kuchelewa. Catherine kila mara anamkumbusha yule dada. Kesho hatarudia kesho kutwa karudia.
Mpaka alipoamua kumuuliza Inakuwaje hii hali haikomi? Yule dada akajielezea hali ilivyo na kilichoonekana ni kwamba nyumbani kazi ni nyingi, karo la kulowekea lipo mbali na mbaya zaidi muda wa kupika ni muda wa kwenda kuchukua watoto shule. Hivyo hufanya harakaharaka. Basi Cathy akamwambia fanya mawili kati ya haya Wahi kupika au hakikisha kabla hujaanza kupika kuna maji mengi kando ya jiko ili ukiipua tu unaloweka hapo hapo. Kwanzia hiyo siku lile tatizo lilikwisha.
Kuwa tayari kwa maongezi na usiache kuongea nao, wasikilize kwa makini, jua hali zao, jua nini ni changamoto kwao, jua mawazo yao juu ya vitu kadha wa kadha.
Waulize huku ukionyesha shauku ya kujua nini kilitokea na sio kutaka sababu au hoja na kamwe usikebehi maelezo yao wanayotoa kupitia maelezo wanayotoa utajua mengi na mtaongea mengi zaidi katika mlengwa wa kujengana na sio kuhukumiana.
Pendelea majadiliano na sio mabishano. Majadiliano yatasaidia kujua kipi ni sahihi wakati mabishano yataishia kutambiana nani yupo sahihi. Ukipenda majadiliano itakuwa rahisi watu kukueleza hata mapungufu yako, watu kukupa pongezi, watu kukupa ushauri na watu kukupa ushirikiano katika kutafuta suluhu au njia za kufanikiwa katika jambo fulani.
Maongezi mazuri hujenga na kumsaidia mtu. Humpa faraja, maarifa na hata huondoa hasira kwa mtu. Maneno mazuri ni dawa.
Iwe kwa simu au ana kwa ana usiache kuongea nao,
Iwe sebuleni au kibarazani Usiache kuongea nao.
Iwe faragha au hadharani hakikisha unaongea nao.
Wape watu nafasi katika maongezi tena na tena hata kama wanakuangusha mara kadhaa. Usijivute kuanzisha maongezi na mtu ni kwenye maongezi ndio tunapata marafiki, kujua vitu na kusaidiana.
Watu huchoka lawama na masimango. Kama unaweza ukamsengenya mtu basi pia unaweza ukamsaidia kwakuwa unajua wapi anahitaji msaada. Ongea nae hata kama sio msikivu nenda nae taratibu watu hubadilika siku hadi siku. Usimpe mtu sababu ya kususia maongezi. Usiache kuongea na watu.
Na
Nobel Edson Sichaleh
Fasmo Tanzania
0783961492
Comments